1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mameya wa zamani Rwanda washtakiwa Ufaransa

Sylvia Mwehozi10 Mei 2016

Mameya wawili wa zamani wa nchini Rwanda wanapandishwa kizimbani katika mahakama nchini Ufaransa kwa shutuma za makosa ya kibinadamu na kushiriki mauaji ya halaiki ya mwaka 1994.

https://p.dw.com/p/1IkzT
Symbolbild - Ruanda Opfer des Bürgerkriegs
Picha: Getty Images/C. Somodeville

Mameya wawili wa zamani wa nchini Rwanda lwanapandishwa kizimbani katika mahakama nchini Ufaransa kwa shutuma za makosa ya kibinadamu na kushiriki mauaji ya halaiki ya mwaka 1994. Octavian Ngenzi na mwenzake Tito Barahira kwa pamoja wanatuhumiwa kuwa na mchango wa moja kwa moja katika mauaji hayo.

Kesi hii ya pili kufunguliwa na mahakama maalum iliyoundwa na Ufaransa kwa ajili ya kuwashitaki watuhumiwa wa Kinyarwanda waliokimbilia nchini humo, inatarajiwa kubainisha mwelekeo wa mahusiano baina ya nchi hizo mbili.

Kwa miongo miwili sasa, Rwanda imekuwa ikiituhumu Ufaransa kwa ushiriki katika mauaji ambayo yaliwaua raia laki nane, ikisema kuwa Ufaransa iliisaidia serikali ya wakati huo iliyokuwa ya Kihutu. Miaka miwili baadaye katika kumbukumbu ya miaka 20 ya mauaji hayo, rais wa nchi hiyo Paul Kagame aliwatuhumu waziwazi wanajeshi wa Ufaransa sio tu kwa kusaidia bali kwamba walihusika moja kwa moja katika mauaji hayo.

Na sasa Octavian Ngenzi na Tito Barahira wanapandishwa kizimbani kwa ushiriki wao wa moja kwa moja wa kuwaua mamia ya wakimbizi wa Kitutsi waliokuwa wamejihifadhi katika kanisa mnamo aprili 13 mwaka 1994 huko mashariki mwa mji wa Kabarondo.

Wawili hao wamewahi kuhukumiwa kifungo cha maisha mwaka 2009 na mahakama za kiraia nchini Rwanda, zilizoitwa Gacaca (Gachacha). Wote waliiongoza wilaya ya Kabarondo kwa mihula tofauti. Watuhumiwa wote wanakanusha tuhuma hizo za kushiriki "mauaji ya halaiki" na "kusimamia mpango wa kuangamiza" kabila la Watutsi.

Mojawapo ya izilizokuwa mahakama za kiraia Gachacha
Mojawapo ya zilizokuwa mahakama za kiraia (Gachacha ) nchini RwandaPicha: AP

Mawakili wanaowatetea Philleppe Meilhac na Francoise Mathe wameonyesha "utata" katika ushahidi uliowasilishwa. Mtuhumiwa Barahira yupo katika hali mbaya kiafya akisumbuliwa na ugonjwa wa figo ambapo anahitajika kufanya uchunguzi mara tatu kwa wiki.

Mauaji ya Kabarondo , mji ulioko mpakani na Tanzania yanatajwa kuwa yalichukua kasi kubwa.Yalihitimishwa mwishoni mwa mwezi April baada ya waasi wa Kitutsi wa Rwanda ambao ndio walioko madarakani kwa sasa FPR kudhibiti eneo hilo.

Kesi hii ya mameya wa zamani wa Rwanda itakayosikilizwa kwa wiki zipatazo nane na inakuja baada ya ile ya Pascal Simbikangwa , kapteni wa zamani wa jeshi la Rwanda ambaye alihukumiwa miaka 25 jela kwa kuhusika katika mauaji hayo.

"Kwa kesi hii ya pili, tutashughulika zaidi na ushahidi thabiti wa mauaji, tukiwa na wahanga" anasema Alain Gathier, rais wa mahakama ya pamoja ya madai CCPR. "Wapo mashahidi 50 kutoka Rwanda" ameongeza rais huyo.

Mashihidi wanasema kwamba , asubuhi ya kuamkai April 13 mwaka 1994, walimuona Barahira katika eneo la uwanja wa mpira akiwa na mkuki aliposema amekuja kufanya "kazi", akiashiria kuwaua watutsi. Baadae mamia ya wakimbizi waliowasili jana yake walivamiwa na kuuawa katika saa chache zilizofuata, hayo ni kwa mujibu ya wahanga wa mauaji hayo.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef