1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mamia waandamana Misri kupinga sheria ya halai ya hatari

11 Mei 2010

Mamia ya watu leo wameandamana hadi katika jengo la bunge la Misri, kupinga muswaada wa kurefushwa kwa sheria ya halai ya hatari nchini humo.

https://p.dw.com/p/NLSE
Rais Hosni Mubarak wa MisriPicha: picture-alliance/dpa

Sheria hiyo ambayo iliyopitishwa mwaka 1981, inatoa nafasi kwa mtu kutiwa kizuizini bila ya kipindi maalum, kuzuia mkusanyiko wa zaidi ya watu watano na kutoa nafasi kwa raia kushtakiwa katika mahakama za kijeshi.

Makundi kadhaa ya upinzani yalishiriki katika maandamano hayo, kikiwemo chama kinachoongozwa na mkuu wa zamani wa shirika la kimataifa la nguvu za Atomiki, Mohamed El Baradei cha National Coalition for Change na chama kikuu cha upinzani nchini humo cha Muslim Brotherhood.

Polisi walilazimika kuweka ulinzi mkali kuwadhibiti waandamanaji hao ambao walikuwa wamebeba mabango pamoja na kuimba nyimbo zenye kuilaani sheria hiyo na utawala wa Rais Mubarak.

Ndani ya bunge, wabunge walikuwa wakiendelea na mjadala kabla ya kuupigia kura muswada huo uliyowasilishwa na serikali kutaka sheria hiyo ya hali ya hatari irefushwe kwa kipindi cha miaka miwili zaidi.Hali kadhalika muswaada wa sheria za kupambana na ugaidi pamoja na biashara haramu ya dawa za kulevya.

Katika taarifa yao ya pamoja makundi hayo ya upinzani yalisema kuwa kurefushwa kwa sheria hiyo ya hali ya hatari ni kuwadhalilisha wananchi wote wa Misri na inatakiwa kupingwa na wale wote waliyoathiriwa na sera mbovu za uchumi pamoja na sera za kisiasa za kidikteta.

Waziri Mkuu wa nchi hiyo Ahmed Nazif aliliambia bunge kuwa serikali inataka miaka miwili kwa sheria hiyo kuendelea, ili kukabiliana na ugaidi pamoja na biashara haramu ya dawa za kulevya.

Lakini akizungumza wakati wa maandamano hayo,Saad al-Katatny ambaye ni mbunge binafsi lakini mwanachama wa chama kikuu cha upinzani cha Muslim Brotherhood amesema, serikali ina ajenda ya siri katika kutumia sheria hiyo, ikiwa na nia ya kuendelea kuongoza na kuudhoofisha upinzani.

Chama hicho cha Muslim Brotherhood kimsingi kimepigwa marufuku kushiriki katika shughuli za kisiasa nchini Misri, Lakini wanachama wake wamekuwa wakiwania na kuingia bungeni, kama wagombea binafsi.

Naye kiongozi wa chama kingine cha upinzani cha al-Ghad, Ayman Nour amesema, serikali ya Misri katika kipindi chote ilichokaa madarakani imekuwa ikitumia kivuli cha sheria hiyo kuweza kuendelea kukaa madarakani na kwamba haiwezi kutawala bila kuwepo kwa sheria hiyo.

Kiongozi huyo wa upinzani amekwishatangaza nia yake ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwakani, ijapokuwa kisheria aruhusiwi, kutokana na mashtaka ya udanganyifu yanayomkabili ambayo anatuhumiwa kuyatenda wakati wa kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.

Mbunge mwengine asiyekiwakilisha chama chochote bungeni, Jamal Zahran amesema hii ni mara ya tatu kwa serikali kuwasilisha muswaada wa kurefushwa kwa sheria hiyo ya hali ya hatari tokea mwaka 2005 na kuongeza kuwa kila mara imekuwa ikidai kuwa itakuwa mara ya mwisho kurefushwa kwa muda wa kuwepo kwa sheria hiyo.

Kwa upande wake Heba Morayef kutoka Shirika la Kimataifa la Haki za Binaadamu la Human Right Watch, nchini Misri, ameunga mkono akisema hilo si jambo jipya kwa serikali kutaka kurefushwa kwa sheria hiyo.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/DPA

Mhariri:Abdul-Rahman