1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mamia wauwawa katika mapigano Sudan Kusini

10 Julai 2016

Takriban wanajeshi 150 kutoka makundi yanayohasimiana nchini Sudan Kusini wameuwawa katika mapigano katika mji mkuu wa Juba na kuzusha wasi wasi wa kuheshimiwa kwa mchakato dhaifu wa amani.

https://p.dw.com/p/1JMKm
Picha: Reuters

Milio ya risasi,maguruneti na mizinga ilisikika hapo Ijumaa jioni karibu na Ikulu ambapo Rais Salva Kiiri alikuwa akikutana kwa mazungumzo na makamo wake wa rais Riek Machar. Viongozi hao wote wawili ambao huo nyuma walikuwa mahasimu wamesema hawajuwi kile kilichochea mapigano hayo kati ya makundi yao na wametowa wito wa kuwepo utulivu.

Chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya Mafunzo mjini Juba ambayo ni hospitali kuu ya serikali imepokea zaidi ya maiti tisini za askari na raia ambapo kwa mujibu wa daktari mmoja katika hospitali hiyo ambaye amekataa kutajwa jina lake amesema nyingi ya maiti zilikuwa za wanaume.

Jeremiah Young mfanyakazi wa misaada wa shirika la hisani la World Vision aliyeko Juba amesema "kuna watu wanaotembea mitaani lakini wana wasi wasi mkubwa na kwamba kuna uwezekano wa hali kuzidi kuwa mbaya."

Hali ni shwari Juba

Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini Lul Ruai Koang amesema hali katika mji mkuu huo inarudi kuwa ya kawaida.Wakati James Gatdet msemaji wa Machar amevilaumu vikosi vya usalama vya Kiir kwa kuzuka kwa mapigamo hayo ambapo amesema viliwashambulia walinzi wa Machar.

Riek Machar (kushoto)baada ya kula kiapo cha kuwa makamo wa rais kufuatia kurudi kwake Juba hapo mwezi wa Aprili (kulia) ni Rais Salva Kiir.
Riek Machar (kushoto)baada ya kula kiapo cha kuwa makamo wa rais kufuatia kurudi kwake Juba hapo mwezi wa Aprili (kulia) ni Rais Salva Kiir.Picha: Getty Images/AFP/S. Bol

Kwa upande wake Gatijach Deng msemaji wa kitengo cha kijeshi katika kundi la Machar amesema mapigano hayo yalitokea karibu na Ikulu na katika kambi za kijeshi.Deng amesema hapo asubuhi walikusanya maiti 35 kutoka upande wa kundi la (SPL-IO) la Machar na themanini kutoka vikosi vya serikali.Amesema yumkini idadi ya vifo ikaöngezeka kwa upande wa kundi la Machar kutokana na kwamba majeruhi wengi wako mahtuti.

Takriban wanajeshi watano waliuwawa hapo Alhamisi katika mapambano kama hayo kati ya pande hizo mbili.

Taifa hilo changa kabisa barani Afrika linaibuka kutoka vita vya wenyewe kwa wenyewe vilioanza hapo mwezi wa Disemba mwaka 2013 baada ya Kiir kumtimuwa Machar katika wadhifa wa makamo rais.

Vita hivyo vilipiganwa kwa kiasi kikubwa chini ya misingi ya kikabila ambapo Kiir alikuwa akiungwa mkono na kabila lake na Dinka na Machar akiungwa mkono na kabila lake la Nuer.

Makubaliano ya amani

Makubaliano ya amani yaliofikiwa mwezi wa Augusti yalikomesha vita hivyo lakini Kiir na Machar bado hakuviunganisha vikosi vyao kipengele muhimu katika makubaliano hayo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon na Rais Salva Kiir mjini Juba.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon na Rais Salva Kiir mjini Juba.Picha: Reuters/J. Solomon

Mapigano hayo ya Alhamisi na Ijumaa ni kuibuka kwa matumizi makubwa ya nguvu kuwahi kushuhudiwa mjini Juba tokea Machar arudi katika mji mkuu huo hapo mwezi wa Aprili baada ya kumchaguwa tena kama makamo wa rais wake.

Shuhuda wa shirika la habari la Uingereza amesema hapo Jumamosi kwamba Juba iko shwari lakini kuna wasi wasi mkubwa ambapo katika baadhi ya barabara kumewekwa vizuizi vya barabara. Magari makubwa ya kijeshi yameonekana yakipiga doria na takriban shughuli zote za kibiashara zimefungwa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amewahimiza viongozi wa nchi hiyo kutekeleza makubaliano hayo ya amani na kwamba kinachojidhihirisha hakuna kujitolea kwa dhati katika makubaliano hayo.

Sudan Kusini ambapo vita vyake vya wenyewe kwa wenyewe vimesababisa kushuka kwa uzalishaji wake wa mafuta vimefuta sherehe za kuadhimisha siku ya uhuru wa nchi hiyo kutokana na ukosefu wa fedha.

Mwandishi : Mohamed Dahman/dpa/Reuters

Mhariri : Sudi Mnette