1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mamia ya polisi kuhudhuria mazishi ya maafisa waliouwawa Marekani

27 Desemba 2014

Mamia ya maafisa wa polisi nchini Marekani watajiunga na makamu wa rais Joe Biden leo(27.12.2014)mjini New York kwa mazishi ya mmoja wa maafisa wawili wa polisi waliouwawa na mtu aliyekuwa na silaha wiki iliyopita.

https://p.dw.com/p/1EAUq
New York zwei Polizisten erschossen 20.12.2014
Polisi waliouwawa watazikwa mjini New YorkPicha: picture-alliance/dpa/J. Taggart

Meya Bill de Blasio na kamishna wa polisi William Bratton pia wanatarajiwa kuhudhuria mazishi ya Rafael Ramos, mwenye umri wa miaka 40, aliyeuwawa katika shambulio la kushitukiza Desemba 20 pamoja na mwenzake, Wenjian Liu, aliyekuwa na umri wa miaka 32.

Kiasi ya maafisa 730 wanatarajiwa kuhudhuria mazishi hayo, wakikubali pendekezo la kusafiri bure kwa ndege ya shirika la ndege la Jet Blue lenye makao yake makuu mjini New York. Shirika hilo la ndege limetoa nafasi ya kuwasafirisha bure kiasi ya polisi wawili kutoka kila kituo nchini humo ili waweze kuwaunga mkono wenzao , amesema msemaji wa shirika hilo la ndege.

New York zwei Polizisten erschossen 20.12.2014 - PK Bill de Blasio
Meya wa mji wa New York Bill de BlasioPicha: Reuters/S. Keith

Waomboleza

Maelfu ya watu wametoa heshima zao katika kanisa ambalo mwili wa Ramos umehifadhiwa katika kitongoji cha Queens leo Jumamosi, vimeeleza vyombo vya habari nchini humo.

Ramos na Liu wameuwawa na Ismaaiyl Brinsley, ambaye aliapa katika taarifa alizotuma katika mitandao ya kijamii kwamba atamuua polisi ili kulipiza kisasi cha mauaji ya wamarekani wawili weusi mikononi mwa polisi.

Mmarekani huyo mweusi mwenye umri wa miaka 28, aliyempiga risasi na kumjeruhi mpenzi wake wa zamani muda mfupi kabla ya kwenda mjini New York, alijiuwa baadaye katika kituo cha treni ya chini ya ardhi.

New York zwei Polizisten erschossen 20.12.2014 - Ismaaiyl Brinsley
Ismaaiyl Brinsley aliyewauwa polisi wawiliPicha: picture-alliance/Zuma Press

Familia yake imesema amekuwa na matatizo ya kiakili ambayo hayajapatiwa matibabu, na mkuu wa upelelezi wa mji huo amesema taarifa zilizowekwa katika mtandao wa internet zinaonesha kwamba Brinsley alikuwa amekata tamaa kabisa.

Mazishi yacheleweshwa

Mazishi ya Liu yamecheleweshwa hadi wanafamilia watakapoweza kufanya mipango ya kusafirisha mwili wa marehemu kwenda nyumbani China, zimesema taarifa za vyombo vya habari. Jet Blue pia imekubali kusafirisha familia ya Liu kutoka China kwenda mjini New York , Johnston amesema.

Meya aomba maandamano yasitishwe kwa muda

De Blasio amewaomba watayarishaji wa maandamano dhidi ya mbinu za hatua kali za polisi kuahirisha hatua yao hadi mazishi yatakapomalizika, lakini wameendelea na hatua yao. Mamia ya waandamanaji wameingia mitaani siku ya Jumanne usiku mjini New York kuandamana.

US-Vizepräsident Joe Biden in Brasilia
Makamu wa rais wa Marekani Joe BidenPicha: picture-alliance/AP

Michael Skolnik , mhariri mkuu wa globalgrid.com, amekiambia kituo cha televisheni cha MSNBC kwamba waanadamanaji wanahisi huruma kwa kupotelewa na afisa wa polisi, lakini hawatatekeleza ombi la meya.

Maandamano ya kuonyesha hisia za kutambua athari za matumizi ya nguvu yanayofanywa na polisi yamefanyika nchini Marekani tangu Agosti mwaka huu, ambapo afisa wa polisi mzungu alimuua kijana Mmarekani mweusi ambaye hakuwa na silaha Michael Brown mjini Ferguson, Missouri.

USA Proteste gegen Polizeigewalt in New York Demonstranten
Maandamano yanaendelea mjini New York dhidi ya matumizi ya nguvu ya polisiPicha: Reuters/S. Lam

Maandamano yalisambaa katika miji mingine na kuongezeka zaidi baada ya jopo la wazee wa baraza katika kesi ya Brown na katika kesi ya Eric Garner , ambaye alifariki wakati polisi mjini New York walipomkaba hadi kufa , halikuwaona maafisa hao wa polisi kuwa wanaweza kufikishwa mahakamani.

Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae

Mhariri: Amina Abubakar