1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mamilioni ya Waislamu waanza mfungo wa mwezi wa Ramadhan

Mohmed Dahman1 Septemba 2008

Mamilioni ya Waislamu duniani kote leo wameanza kufunga kwa ajili ya mwezi mtukufu wa Ramadhan ambapo hujizuwiya kula na kunywa kuanzia aljajiri hadi jua linapozama takriban siku 30 au 29 kutegemea na muandamo wa mwezi.

https://p.dw.com/p/F8Tg
Misikiti hufurika waumini wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.Pichani ni Waislamu wa Pakistan wakati wa Ramadhan.Picha: AP

Waislamu wanaamini kuwa huu ni mwezi wa kupatiwa msamaha na Mwenyenzimungu kwa hiyo huzidisha ibada kwa wingi na kuwa karibu na Mwenyeenzimungu.

Saudi Arabia mahala kulikozaliwa Uislamu pamoja na nchi kadhaa za Mashariki ya Kati,Ghuba na nchi nyingi za Kiislam ikiwemo Indonesia taifa lenye idadi kubwa kabisa ya Waislamu duniani na hapa Ulaya Waislamu wameanza kufunga leo hii kutimiza nguzo tano ya Uislamu mwezi ambao aya ya kwanza ya Q'uran iliteremshwa kwa Mtume Muhammad SAW.Ni wakati ambapo Waislamu hutafakari kwa undani kabisa matendo yao,kuwa wanyenyekevu zaidi kwa Mwenyeenzimungu kwa kufuata maamrisho yake na kuachana na maovu yote alilyoyakataza pamoja na kuweza kujizuwiya na matamanio ni mwezi uliojaa rehema na fadhila.

Waislamu wanasema huu ni mwezi wa toba wa kuomba msamaha kwa Mwenyeenzi mungu ili kufutiwa madhambi. Inaelezwa kwamba Mtume Muhammad SAW aliwaambia wafuasi wake kwamba milango ya pepo itafunguliwa kwa mwezi huu mzima na ile ya moto itafungwa kwa mwezi mzima.

Suala la kuonekana kwa mwezi ili Waislamu waweze kufunga mara nyingi limekuwa likizusha mashaka Afrika Mashariki ambapo utakuta nchi moja imefunga wakati jirani yake haikufanya hivyo.

Leo hii huko Zanzibar kuna waliofunga na kuna wasiofunga.

Kwa mujibu mwa mwanachuoni wa Zanzibar hapo jana radio moja ya kibinafsi ilitangaza kwamba leo ni Ramadhan baada ya kuonekana kwa mwezi huko Mombasa Kenya.

Mwezi pia umeonekana Afrika Kusini na Namibia.

Hata hivyo naibu kadhi alitangaza asubuhi yake kupitia sauti ya Tanzania Zanzibar kwamba leo sio Ramadhan kwa hiyo kuna waliofunga na kuna wasioufunga.

Kwa muhtasari Ramadhan kwa Waislamu ni mwezi wa aina yake ni mwezi wa ucha mungu na hukamilishwa baada ya mwezi mmoja kwa sherehe za Idd el Fitr.