1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mamlaka za Urusi zawaonya wanaotaka kuandamana

Lilian Mtono
22 Januari 2021

Mamlaka za usalama nchini Urusi zimewaonya watu wanaotaka kuandamana wanaomuunga mkono mkosoaji wa rais Vladmir Putin anayeshikiliwa kizuizini Alexei Navlany na kuahidi hatua kali.

https://p.dw.com/p/3oIC8
Russland Moskau | Flughafen Scheremetjewo | Alexej Nawalny
Picha: Polina Ivanova/REUTERS

Mamlaka nchini Urusi zinaendelea kuwachukulia hatua kali wafuasi wa kiongozi wa upinzani na mkosoaji mkubwa wa ikulu ya Kremlin Alexei Navalny aliyekamatwa akiwa uwanja wa ndege mjini Moscow siku ya Jumapili wakati anarejea kutokea Ujerumani alikokuwa akitibiwa kufuatia shambulizi la sumu inayoharibu mishipa ya fahamu. 

Msemaji wa Navalny Kira Yarmysh ameandika kwenye ukurasa wa Twitter kwamba usiku wa jana aliwekwa kizuizini baada ya kutoa mwito wa maandamano na kuongeza kuwa mahakama iliamua asalie kizuizini kwa siku tisa. Waratibu wa tawi la wafuasi wa Navalny katika miji ya Vladivostok, Krasnodar na Kaliningrad pia waliwekwa vizuizini.

Maandamano dhidi ya hatua ya kushikiliwa Navalny pamoja na ukandamizaji unaofanywa na serikali chini ya utawala wa Rais Vladimir Putin yanatarajiwa kufanyika katika takriban miji 70 ya Urusi kesho Jumamosi.

Russland St. Petersburg | Verhaftung bei Protest für Alexej Nawalny
Waratibu wa matawi ya wafuasi wa Navalny wanashikiliwa na polisi katika miji mbalimbali nchini Urusi.Picha: Alexander Demianchuk/TASS/picture alliance

Msemaji wa ikulu ya Urusi, Dmitry Peskov amewaonya watu kutoshiriki maandamano hayo yaliyopigwa marufuku.

''hatuna shaka kwamba kuna baadhi ya vitendo vinavyohusiana na matukioa haramu, na ni kawaida kwamba huwa kuna maonyo kuhusu athari zinazoweza kujitokeza iwapo watu watashindwa kuheshimu sheria."

Navalny, alihukumiwa kifungo cha siku 30, kufuatia mashitaka yanayomkabili ya kukikuka masharti ya msamaha wa kifungo cha awali baada ya kwenda Ujerumani kwa matibabu kusikilizwa kwa dharura siku ya Jumatatu.

Rais waBaraza la Ulaya Charles Michel ameurejea mwito wa umoja huo kwa rais Putin hii leo wa kumuachilia huru Navalny. Ameandika kupitia ukurasa wake wa Twitter kwamba Urusi inatakiwa kuendeleaza uchunguzi huru na wa haki kuhusiana na jaribio la mauaji dhidi ya mpinzani huyo wa Putin.

TikTok App Smartphone Handy Symbolbild
Tiktok ni miongoni ya mitandao inayotumiwa kuhamasisha maandamano nchini Urusi ya kupinga ukandamizaji wa serikali ya Putin.Picha: Drew Angerer/Getty Images

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema anaamini miito hiyo ni ya haki na inapaswa kutekelezwa mara moja.

Suala la kifungo cha Navalny pia lilijitokeza katika mazungumzo baina ya Rais wa Finland Sauli Niinisto na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin, ambapo Niinisto amemweleza Putin kuwa kuendelea kushikiliwa kwa mpinzani wake kutaathiri mahusiano baina ya Urusi na Umoja wa Ulaya.

Idara ya polisi ya mji wa Moscow imeonya kuhusu maandamano hayo na kusema haitasita kuwachukulia hatua kali watu watakaoandamana kesho na kuongeza kuwa vikosi vya usalama vitachukua hatua mara moja iwapo kutakuwa na ukiukaji wowote ili kuhakikisha usalama.

Pamoja na onyo hilo, bado kunaongezeka miito ya kushiriki maandamano hayo ya kesho hata kwenye mitandao ya kijamii ikiwa ni pamoja na Tiktok, ambao ni maarufu kabisa kwa vijana.

Mashirika: DPAE/AFPE