1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Man City wavunja rekodi, Barca hoi katika La Liga

14 Mei 2018

Nchini England Manchester City wameweka rekodi kwa kumaliza ligi hiyo wakiwa na pointi mia moja. Hakuna timu nchini humo ambayo ishawahi kumaliza msimu na kiwango kama hicho.

https://p.dw.com/p/2xhy9
UEFA Championsleague | Manchester City v FC Basel
Picha: Reuters/A. Yates

City walifikisha kiwango hicho baada ya kuwalaza Southampton goli moja bila hapo jana bao lililotiwa katika sekunde za mwisho za mechi na mchezaji wa akiba Gabriel Jesus.

City waliishinda Ligi Kuu ya England wakiwa alama 19 mbele ya mahasimu wao Manchester United waliomaliza kwenye nafasi ya pili. Timu zitakazoshiriki Champions League nchini humo ni Manchester City, Manchester United, Tottenham Hotspur ambao wameufunga msimu katika nafasi ya tatu na Liverpool ndiyo timu ya mwisho kucheza katika ligi hiyo ya mabingwa. Kumbuka Liverpool wao wanajiandaa pia kucheza na Real Madrid kwenye fainali ya Champions League tarehe 26 huki Kiev. Chelsea na Arsenal watacheza Europa League.

Tukiwazungumzia Liverpool, mshambuliaji wao ambaye amechaguliwa kuwa mchezaji bora katika Ligi Kuu ya England msimu huu Mohammed Salah kutoka Misri, alipewa tuzo ya kiatu cha dhahabu jana kwa kumaliza akiwa mfungaji bora baada ya kutikisa wavu mara 32 magoli mawili mbele ya mshambuliaji wa Tottenham Hotspur Harry Kane aliyekuwa na mabao 30.

Rekodi ya Barcelona ya kutofungwa yavunjwa na Levante

Huko Uhispania nako katika La Liga Barcelona ndio mabingwa ila wameumaliza msimu kwa njia ambayo hawakuipendelea kwani kwenye mechi yao ya mwisho jana walizidiwa kete na Levante magoli 5 - 4. Lionel Messi alipumzishwa katika mechi hiyo ila kazi ilifanywa na Philipe Coutinho aliyepachika mabao matatu pekeyake ila hayakutosha kuwapa ushindi na rekodi yao ya kutofungwa msimu mzima ilifikishwa mwisho katika hiyo mechi yao ya mwisho wa msimu.

Ernesto Valverde
Kocha wa Barcelona Ernesto ValverdePicha: picture-alliance/NurPhoto/G. Maffia

Mchezaji wa Ghana Emmanuel Boateng ambaye ni mchezaji wa Levante yeye pia alifunga mabao matatu kwenye mechi hiyo iliyoshuhudia jumla ya mabao tisa. Mara ya mwisho Barca kufungwa kabla mechi ya jana ilikuwa Aprili 8 mwaka jana walipolazwa mbili bila na Malaga. Lakini hii ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kabisa Barcelona kukubali mabao matano langoni mwao katika La liga tangu wafungwe na Malaga tena mabao matano kwa moja Desemba mwaka 2003.

Real Madrid ndiyo timu ya kwanza kumaliza msimu bila kufungwa huko Uhispania na hiyo ilikuwa katika msimu wa mwaka 1931-1932. 

Mwandishi: Jacob Safari/AFPE/DPAE/APE

Mhariri: Iddi Ssessanga