1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Manchester City yafunga dirisha la usajili kwa kishindo

Liongo, Aboubakary Jumaa3 Septemba 2008

Timu ya Manchester City ya Uingereza imeweka historia ya usajili kwa kumnunua kwa dau kubwa mbrazil Robinho

https://p.dw.com/p/FAbZ
Tajiri wa timu iliyopanda daraja katika bundesliga ya Hoffenheim 1899 Dietmar-Hopp ambaye fedha zake zimesaidia kuinyua timu hiyo ya kijijiniPicha: picture-alliance/ dpa

Dirisha  la usajili barani Ulaya lilifungwa kwa uhamisho uliyoweka historia katika soka la Uingereza, ambapo mshambuliaji chipukizi wa kibrazil Robinho amenunuliwa na Manchester City kwa kitita cha paundi  millioni 32.5 kutoka kwa mabingwa Uhispania Real Madrid.


Dirisha hilo litafunguliwa tena mwanzoni mwa mwezi January mwakani. 


Ikiwa ni siku chache tu baada ya kununuliwa na kampuni kubwa la Abu Dhabi, Manchester City imeonesha kuwa sasa itakuwa katika jukwaa moja na timu kama Manchester United, Chelsea, Liverpool na Arsenal.


Toka ilipotwaa ubingwa wa ligi kuu ya Uingereza mwaka 1968, Manchester City imekuwa ikiishi katika kivuli cha Manchester United, huku ikishindwa kabisa kufurukuta, ambapo hali ilikuwa mbaya kabisa mwaka 1999 wakati iliposhuka hadi daraja la tatu.


Lakini kwa ujiyo wa waarabu hao, kumewafanya washabiki wao sasa kuanza kuwa na matumaini ya kutembea vifua wazi kwani dalili zimekwishaanza kuonekana kwa kumnunua Robinho.


Manchester City imeizidi mbio Chelsea ambao nao walikuwa wamefungua pochi yao kwa ajili ya Robinho.


Hata hivyo Manchester City walizidiwa kete dakika za mwisho na jirani zao United, katika kumsajili mshambuliaji wa Totenham  Dimitar Berbatov kwa kitita cha paundi millioni 30.75.


Kabla ya kufungwa kwa dirisha hilo pia kulishuhudia uhamisho wa wachezaji wengine kadhaa kama vile Luis Saha aliyekuwa Manchester United na ambaye amejiunga na  Everton.


Kwa ujumla ada ya uhamisho kwa wachezaji katika duru hii ya kwanza huko Uingereza imegharimu kiasi cha paundi millioni 500 ambazo ni sawa na dola millioni 894.


Kiwango hicho kinaifanya ligi kuu ya Uingereza kuwa ligi iliyotumia fedha nyingi kabisa barani ulaya.Msimu uliyopita ligi hiyo ilitumia kiasi cha paundi millioni 470 katika uhamisho wa wachezaji.


Mfano ni ligi kuu ya Ujerumani Bundesliga mbayo wakati dirisha la usajili likifungwa hapo jumatatu, jioni ilikuwa imetumia kiasi cha euro millioni 150, ikiwa pungufu na kiasi cha euro millioni 194 zilizotumika mwaka jana.


Mabingwa watetezi wa bundesliga, Bayern Munich ndiyo timu pekee inayotumia kiasi kikubwa cha fedha katika usajili, lakini mwaka huu haikutumia hata senti moja kwani haikusajili mchezaji mpya, ingawaje imemchukua kwa mkopo beki wa AC Milan ya Italia Massimo Oddo na pia kiungo wa Bremen Tim Borowski ambaye alikuwa mchezaji huru.


Msimu uliyopita ilitumia kiasi cha euro millioni 70 kwa ajili ya kuwanasa majogoo kama Frank Ribbery na Luca Toni.


Hamburg ndiyo timu iliyojaribu kutumia fedha kiasi, katika msimu huu ambapo ilimsajili mbrazil Thiago Neves kwa kitita cha euro millioni 9,beki wa Bayern Munich Marcell Jansen kwa euro millioni 8 na mbrazil mwengine Alex Silva kwa euro millioni 6.2


Tukiachana na soka katika masumbwi, bingwa wa zamani wa uzito wa juu nchini Uingereza James Oyebola amepigwa risasi na kuawa hapo jana baada ya kutokea ugomvi katika klabu moja ya usiku mjini London.


Chanzo cha ugomvi huo ilikuwa ni baada ya bondia huyo wa zamani kuwataka vijana waliyokuwa karibu naye kuacha kuvuta sigara ambapo baadaye walimfyatulia risasi shingoni na kumuua.


Oyebola alikuwa bingwa wa uzito wa juu nchini Uingereza mwaka 1994 ambapo alitwaa medali shaba mwaka 1986 katika michezo ya jumuiya ya madola mjini Edinburgh  baada ya kupigwa na Lenox Lewis katika nusufainali.