1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Manchester na Chelsea leo uwanjani

6 Novemba 2009

Munich na schalke ipi itatamba ?

https://p.dw.com/p/KQEd
Berbertov wa Manu atiwa munda na Chelsea.Picha: picture alliance/dpa

Katika Premier League,leo ni leo,(Jumamosi) asemae kesho muongo:Chelsea inaumana na Manchester United-timu 2 za kileleni .Katika Bundesliga,swali ni je,Munich itatamba nyumbani mbele ya Schalke ?Chipukizi 2 wa Bundesliga-Thomas Mueller wa Bayern Munich na Aaron Hunt wa Werder Bremen,wameteuliwa kuichezea timu ya Taifa wiki ijayo, Ujerumani itakapocheza na Chile mjini Cologne na Ivory Coast,mjini Gelsenkirchen.

BUNDESLIGA NA PREMIER LEAGUE:

Macho ya mashabiki wa Bundesliga yanakodolewa Olympic Arena, mjini Munich kuangalia iwapo Bayern Munich iliokandikwa mabao 2:0 na Girondins Bordeaux ya Ufaransa hapo juzi katika Kombe la ulaya la Champions League ,itaweza kuzima vishindo vya Schalke 04 ikitaka kutoroka na pointi 3 kutoka Olympic Arena.

Munich inaazimia hadi X-masi iwe imeshaparamia kileleni mwa ngazi ya Bundesliga,lakini siku hizi hakuna timu inayoiogopa Munich na Schalke ina jogoo lake Kevin Kuranyi ambalo llinaendelea kuwika.

Mpambano mwengine wa kusisimua jioni ya leo, ni kati ya mabingwa Wolfsburg waliotamba katika champions League dhidi ya Besiktas Istanbul na chipukizi Hoffenheim, timu iliohanikiza mno msimu uliopita.Borussia Moenchen gladbach ilioitungua Hamburg kileleni mwishoni mwa wiki iliopita iko nyumbani na mahasimu wao leo, ni Stuttgart.Stuttgart imeanza kuimarika baada ya kumudu sare nyumbani mwishoni mwa wiki iliopita kati yake na Bayern Munich na sare tena dhidi ya Sevilla ya Spain katika champions League. Lakini ,Borussia inahitaji pointi 3 nyumbani leo.

Mapambano mengine leo ni kati ya Mainz na Nuremberg na Bochum na Freiburg.

Kesho mapambano 3 yatakamilisha kalenda ya mwishoni mwa wiki hii ya Bundesliga:

Hannover itaikaribisha nyumbani Hamburg wakati FC Cologne inabidi kufunga safari hadi Berlin, kwa miadi yake na Hertha Berlin .Hii ni changamoto ya timu 2 za mkiani mwa Ligi.Mpambano kati ya Werder Bremen iliotamba kati ya wiki kwenye Kombe la mabingwa la ulaya -League-champions na Borussia Dortmund, utakamilisha msisimko wa Jumapili hii.

PREMIER LEAGUE:

Zahama ni leo katika Premier League:kwani timu mbili za kileleni zinaumana:Chelsea na Manchester United zina miadi ya kunyan'ganyia usukani wa Ligi.Wakati Arsenal na Manchester City, zaania kuziba mwanya wao na timu hizo mbili za kileleni,Manu na Chelsea, zinakumbana katika mechi kali ya msimu huu.

Arsenal inacheza na Wolves hampton wakati Manchester City iliopo pointi 3 kutoka ilipo Arsenal, ina miadi na Burnley.Tottenmham Hotspur ikiwa nafasi ya 5 inaikaribisha Sunderland nyumbani . Liverpool,ikiwa pointi 1 nyuma na nafasi ya 6 katika orodha ya Premier League, inanatumai pointi 3 kutoka lango la Birmingham City.

KOMBE LA DUNIA 2010:

Algeria ina miadi na Misri,mabingwa wa Afrika hapo Novemba 14 kuamua nani kati yao, atatoroka na tiketi ya Afrika kusini kwa Kombe la dunia, Juni ,2010.Kocha wa Algeria , Rabah Saadane, ameshateua kikosi chake cha kuivamia Misri, mabingwa wa Afrika hapo novemba 14:Kinajumuisha kipa Fawzi Chaouchi,Majid Bougherra wa (Rangers) na Antar Yahiya anaechezea Bochum katika Bundesliga.

Nae Kocha mpya na wa zamani wa Bafana Bafana,Afrika Kusini,mbrazil Carlos Parreira, amemuita tena Benni MacCathy, kumpigia beni katika mechi za kirafiki zinazokuja kwa maandalio ya kombe la dunia.

Nae kocha wa Timu ya Taifa ya Ujerumani, Joachim Loew, amemchagua chipukizi wa Bayern Munich, Thomas Mueller na stadi wa Werder Bremen, Aaron Hunt katika kikosi cha Ujerumani kitakacho pambana na Chile, Novemba 14, mjini Cologne na Ivory Coast,baadae.

Mwandishi: Ramadhan Ali/RTRE

Mhariri:Abdul-Rahman