1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini.

Mtullya, Abdu Said11 Juni 2008

Katika maoni yao leo magazeti ya Ujerumani yanazungumzia juu ya ziara ya rais G.W. Bush nchini Ujerumani.

https://p.dw.com/p/EHnU
Rais G.W.Bush wa Marekani katika ziara ya kuaga nchini Ujerumani akiwa pamoja na Kansela Angela Merkel.Picha: AP

Rais George W.Bush wa Marekani anafanya ziara ya buriani nchini Ujerumani, yumkini ya mwisho katika wadhifa wake kama rais.

Katika maoni yao leo wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanazungumzia juu ya ziara hiyo.

Gazeti la Nordwest-Zeitung linasema rais Bush amekuja Ujerumani kuaga. Lakini hakuna anaeangusha kilio.Gazeti linasema pana tofauti kubwa baina yake na baba yake. Bush Baba ,alitoa mchango mkubwa katika kuwawezesha wajerumani waungane tena; kwa usemi mwingine alitoa mchango mkubwa katika kuondolewa kuta la Berlin.

Lakini Bush mtoto amejenga kuta jipya kutokana na siasa zake.


Gazeti la Thüringische Landeszeitung pia linazungumzia juu ya ziara ya rais Bush nchini Ujerumani kwa kusema kuwa jina la rais huyo siku zote litaambatanishwa na matukio mabaya.

Gazeti hilo linayataja matukio hayo kuwa ni vita vya Irak ambapo Marekani imeshindwa, pia linataja jela ya Guantanamo ambapo mahubusi wanawekwa katika mazingira yanayokiuka utu. Jina la rais Bush pia litaambatanishwa na kashfa ya jela ya Abu Ghraib nchini Irak.

Gazeti pia linatamka wazi kuwa hakuna anaetafuta leso, ili kufuta machozi kwa ajili ya George Bush.


Lakini gazeti la Flensburger Tageblatt linasema yapo mambo mazuri ambayo Bush amefanya.

Mhariri wa gazeti hilo, anaeleza kuwa Bush aliilazimisha Korea ya Kaskazini kufanya mazungumzo, aliweka mkazo katika suala la wapalestina,ameisaidia Afrika na ameikemea Iran.