1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini.

Mtullya, Abdu Said4 Juni 2008

Magazeti ya Ujerumani yatoa maoni juu ya Barack Obama.

https://p.dw.com/p/EDTC
Seneta wa jimbo la Illinois Barack Obama katika juhudi za kuwania fursa ya kugombea urais nchini Marekan.iPicha: AP

Masuala  yanayozungumziwa leo duniani kote ni mkutano wa mjini  Rome ambapo wajumbe  wanajadili njia za kupambana na  tishio la njaa, na juu ya seneta  Barack  Obama.

Magazeti  ya Ujerumani pia  yanazingatia masuala hayo katika maoni yao.

Juu ya seneta  Obama gazeti  la Ostthüringer linasema  vijana kati ya umri wa miaka18  na 35 ,  nchini Marekani  wameweza   kushuhudia kampeni ya seneta huyo kama hatua ya kihistoria na  mwanzo mpya  wa mustakabal  wa nchi yao. Gazeti linasema vijana hao hawajioni kuwa ni sehemu ya chama bali wanajiona  kuwa ni sehemu ya mchakato.  Mhariri wa gazeti la Ostthüringer anasema  vijana hao ni rika la Obama.

Mhariri huyo anaeleza  kuwa hadi  sasa hakuna  mwanasiasa  wa  Marekani alieweza  kuwahamasisha  vijana  wengi kama seneta Obama.

Gazeti la Kölner Stadt-Anzeiger linatoa maoni juu  ya  mshindani  wa  Obama-seneta  Hillary Clinton ambae kimsingi ameshindwa kufikia  lengo lake.


Gazeti hilo linasema ,wamerekani waliotaka kushuhudia  tukio la kihistoria katika nchi yao-yaani kumwona mwanamke wa kwanza  akigombea urais, wameingiwa uchungu.Hatahivyo gazeti  linaeleza kuwa, huo ni ujumbe mzuri kwa demokrasia ya  Marekani. Tawala za  kifamilia, iwe ni akina Bush au akina Clinton, siyo jambo linalotakiwa katika  demokrasia.


Mkutano  juu ya mgogoro wa  chakula duniani  unaohudhuriwa na wakuu wa nchi unaendelea mjini Roma. Gazeti la Der neue Tag limetoa  maoni yake juu ya mkutano huo kwa kusema  kuwa kuwapo kwa  mgogoro  wa  chakula duniani ni kashfa.

Gazeti hilo linaeleza katika maoni yake kuwa miongoni  mwa  wanaowajibika, hakuna anaeweza  kukwepa  lawama, iwe katika  nchi  zinazokabiliwa  na mgogoro huo au katika nchi  tajiri za magharibi.