1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Chanjo ya AstraZeneca isiondolewe kabisa

Grace Kabogo
17 Machi 2021

Mamlaka zinachukua hatua kwa uangalifu kuzuia chanjo ya virusi vya corona ya AstraZeneca. Lakini hilo halimaanishi kuwa chanjo hiyo sio salama, anaandika mwandishi wa DW, Fabian Schmidt.

https://p.dw.com/p/3qkxF
Symbolbild Injektionsflasche mit Spritze AstraZeneca
Picha: Christian Ohde/CHROMORANGE/picture alliance

Ni kweli, watu wawili wamekufa kutokana na damu kuganda na wengine wametibiwa hospitali. Na ndio, visa vyote vimetokea baada ya watu hao kuchomwa chanjo ya AstraZeneca iliyotengenezwa na kampuni hiyo ya dawa nchini Uingereza kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Oxford.

Lakini kuhitimisha kwamba chanjo hiyo ni hatari, kunaweza kuwa mapema sana. Kwanza, haijulikani iwapo damu kuganda kweli kuna uhusiano wowote na chanjo. Na pili, sisi binadamu tunakabiliwa na hatari kubwa ya damu kuganda siku baada ya siku kuliko tunavyoweza kukutwa na tatizo hilo kama matokeo ya chanjo.

Sababu au uhusiano?

Kwanza, jambo muhimu zaidi: Baadhi ya watu wana matatizo ya damu kuganda, iwe kwa kupata chanjo au bila ya chanjo. Iwe ni bahati mbaya au ikiwa kuna uhusiano na chanjo, kwa kawaida huoneshwa kwa takwimu. Swali ni je: Kuna ongezeko lisilo la kawaida kwa visa vya watu damu kuganda baada ya chanjo?

Kutokana na kile tunachojua hadi sasa, sivyo ilivyo kwa chanjo ya AstraZeneca. Kwa kweli, madaktari nchini Uingereza pekee tayari wametoa zaidi ya dozi milioni 11 za chanjo. Visa vitatu vya damu kuganda vimeripotiwa. Kumekuwa na visa saba kati ya watu milioni 1.6 waliochanjwa nchini Ujerumani.

Schmidt Fabian Kommentarbild App
Fabian Schmidt wa DW

Hii ni sawa na visa vinne kwa chanjo milioni moja tangu chanjo ya Astrazeneca ilipoanza kutumika nchini Ujerumani mwanzoni mwa mwezi Februari. Hata hivyo, aina hii ya damu kuganda inatokea mara mbili hadi tano kwa watu milioni moja kwa mwaka katika idadi jumla ya watu hata bila ya chanjo.

Visa hivyo vilitokana na kundi ambalo lilijumuisha jumla ya dozi milioni moja. Hata hivyo ni sawa kwa mamlaka za udhibiti kwa mara nyingine tena kuchunguza matokeo yote ya utafiti na takwimu zilizopo, kwani tafiti nyingi hazijakamilika vizuri kwa sababu ya uharakishaji wa taratibu za kutoa idhini.

Hatari kubwa ya damu kuganda kwenye maisha ya kila siku

Chanjo inaweza kukukinga na ugonjwa fulani, lakini haiwezi kukukinga dhidi ya sababu nyingine ambazo zinaweza kusababisha kifo. Kwa sasa watu wazee zaidi na wagonjwa sana wanapokea chanjo za COVID-19. Watu ambao tayari wako hatarini, huenda wakafa kutokana na sababu zingine.

Yote haya sio sababu ya kuogopa. Katika mfano unaojulikana na uliothibitishwa kisayansi, kwa kila wanawake milioni moja wanaotumia vidonge vya uzazi wa mpango, takriban 1,100 wanapata matatizo ya damu kuganda. Juu ya hilo, mazingira kadhaa tuliyonayo au tabia yanaongeza hatari mara mbili zaidi ya kupata matatizo ya damu kuganda.

Hayo ni pamoja na unene kupita kiasi, kusafiri: hasa safari ndefu za ndege, gari, mabasi au treni pamoja na kuvuta sigara. Sababu yote hizi zimethibitishwa kisayansi, lakini uwezekano wa uhusiano na chanjo haujathibitishwa kabisa.

Chanjo zinaokoa maisha

Tuko mwanzoni mwa wimbi hatari la tatu la maambukizi ya virusi vya corona. Kwa Ujerumani, wataalam wa afya tayari wanatabiri viwango vya zaidi ya visa 300 kwa wiki kati ya wakaazi 100,000. Chanjo zote zilizoko sokoni kwa sasa zinaonyesha kufanya kazi.

Hiyo inamaanisha zinazuia sababu zote mbaya za magonjwa na kulazwa hospitalini, hata kama kwa sasa kuna aina mpya ya virusi vya corona. Chanjo zinaokoa maisha. Na AstraZeneca pia inaokoa maisha. Zamu yangu itakapofika, nitafurahi pia kuchoma chanjo ya AstraZeneca.

(DW https://bit.ly/3loM1Da)