1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Hali ngumu kwa vyombo vya habari Tanzania

Mohammed Khelef
11 Agosti 2020

Kanuni mpya kuhusu ushirikiano baina ya vyombo vya habari vya ndani na vya nje zinalenga zaidi kuudhibiti ushirikiano huo kuliko kuuongoza, anaandika Mohammed Khelef kwenye maoni yake juu ya kanuni hizo.

https://p.dw.com/p/3gnOr
Tanzania President John Pombe Magufuli in Dar es Salaam
Picha: DW/S. Khamis

Kinachozusha mashaka zaidi kwenye kanuni hizo ni pale zinaposema kuwa chombo cha ndani kitabeba dhamana kwa "makosa" ambayo yamo kwenye kile kinachotangazwa na chombo cha nje kupitia matangazo yake, kwani tangu uanze, utawala wa Rais John Magufuli umetanuwa fasili ya "makosa" kwenye upana ambao unajumuisha chochote ambacho kiko kinyume na mtazamo wake binafsi – kuanzia takwimu za uchumi hadi za maradhi ya COVID-19, ugonjwa ambao ameshautangaza kitambo kwamba umepotea nchini mwake kutokana na maombi. 

Makosa kwake ni hata kauli za kulalamikia hali ngumu ya maisha kwa wananchi wa kawaida, maana Magufuli ni aina ya watawala wasiopenda kusikia sauti tafauti na yake.

DW Kiswahili | Mohammed Khelef
Mohammed Khelef, DW KiswahiliPicha: DW/L. Richardson

Tayari kuna watu wanaotumikia vifungo na wengine wenye kesi mahakamani kwa yale yanayoitwa "makosa ya kimtandao", ambapo kosa lao kubwa ni kuwa na mtazamo tafauti na wa serikali kuhusu masuala madogo madogo.

Katika utekelezaji wa kanuni hizi mpya, tayari kituo cha Star TV kimeshatakiwa na Mamlaka hiyo ya Mawasiliano kujieleza baada ya kurusha mahojiano yaliyofanywa na Idhaa ya Kiswahili ya BBC na kiongozi mashuhuri wa upinzani, Tundu Lissu, akizungumzia kuzuiwa kuuaga mwili wa rais wa zamani, Benjamin Mkapa, aliyefariki dunia mwezi uliopita. 

DW ambayo ina mamilioni ya wasikilizaji nchini Tanzania inaweza kujikuta imefanya "makosa" hayo kwa fasili ya serikali ya Tanzania, kwa kufanya mahojiano na mwanaharakati ambaye, kwa mfano, analiangalia suala la elimu ya wasichana kwa mtazamo tafauti na ule wa Rais Magufuli.

Nini kifanyike?

Redio washirika zinaporuhusu mahojiano hayo kuruka, zitakuwa moja kwa moja zimejihalalishia kuadhibiwa. 

Kwa hivyo, ili kuepuka adhabu ya dola, DW na redio hizo zitalazimika kuchaguwa moja kati ya matatu: ama, kwanza, kutokurusha kabisa matangazo ya DW na hivyo kuwakosesha mamilioni ya Watanzania haki yao ya kupata habari za kina na za uchambuzi kutoka DW.

Ama, pili, kuyarikodi matangazo na kuyachuja kwa kuondosha kila kile ambacho watakiona kinapingana na mtazamo wa serikali, na hatimaye kuwalisha Watanzania kilichosalia.

Na la, tatu, ni kwa DW yenyewe kujihariri na kujichuja kwa kutokutangaza chochote ambacho itaona kuwa kinahalifu mtazamo wa serikali ya Tanzania. Ikifika hapo, huo hautakuwa tena uandishi wa habari, na wala hii haitakuwa tena DW.

Ndiyo maana DW inapaswa kulisemea hili kwa upana wake. Kwamba japo ni muhimu sana kwa kila chombo cha habari kuheshimu kanuni zinazowekwa na mamlaka halali za kitaifa na kimataifa, ni muhimu zaidi kwa wawekaji wa kanuni hizo kutokiuka misingi ya kisheria kwenye kuandika kanuni zao.

Misingi hiyo ni ile inayolinda uhuru wa kikatiba na kilimwengu kwenye haki ya kutowa na kusambaza habari.