1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Hongera Emmanuel Macron!

Zainab Aziz
26 Aprili 2018

Ziara ya kiserikali ya rais wa Ufaransa Emmanuel Macron imekuwa ya mafanikio. Hotuba yake iliyolisisimua bunge la Marekani imeonesha kwamba urafiki wa kibinafsi hauwezi kumzuia kuzikosoa sera zaTrump.

https://p.dw.com/p/2whK2
USA Capitol Hill in Washington | Emmanuel Macron, Präsident Frankreich
Picha: Reuters/B. Snyder

Baada ya kuifuatilia awamu ya kwanza ya ziara ya Macron, mtu anaweza kuhisi kwamba Trump hakumchukulia Macron kama ni kiongozi sawa na yeye. Ilikuwa ni vigumu kuacha kumuonea huruma rais huyo wa Ufaransa, kwa sababu baada ya Trump kumpa sifa nyingi mwenzake huyo mwenye umri mdogo na kumkaribisha kwenye dhifa ya chakula cha jioni ndani ya ikulu,Trump hakusita kutangaza hadharani mapendekezo yake yote.

Sehemu ya pili ya ziara ya Macron ni hotuba yake bungeni. Rais huyo wa Ufaransa aliitumia hotuba hiyo kuelezea tofauti baina ya sera zake na zile anazozitetea raisTrump. Macron alitilia mkazo masuala ya demokrasia, uhuru, uvumilivu, haki za binadamu na ushirikiano wa kimataifa, kwa kuzingatia maadili ya nchi za Magharibi.     Rais huyo wa Ufaransa ameyafanya hayo katikati ya demokrasia ya Marekani tena mbele ya bunge linalodhibitiwa na wajumbe wa chama kikongwe cha Republican, jambo ambalo limeiongezea uzito hotuba ya Macron. Lakini je ziara ya rais wa Ufaransa bado inaweza kuhesabika kuwa imefanikiwa, ingawa hakuna uhakika kwamba amefaulu kuubadili msimamo wa Trump juu ya masuala muhimu?

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron
Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Reuters/J. Ernst

Ikiwa jibu litakuwa ndio basi itakuwa ni kutokana na sababu mbili ya kwanza ni kuhusu ikulu ya Trump, ambapo mtu atapaswa kushukuru iwapo atafanikiwa atakapofika huko. Kwa mfano ilishuhudiwa baada ya ushindi wa kushangaza wa bwana Donald Trump kulikuwepo na majadiliano ya kejeli katika mji mkuu wa Marekani, Washington kwamba labda waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban angelialikwa kwenye ikulu ya nchi hiyo kama kiongozi wa kwanza kumtembelea bwana Trump.

Waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban
Waziri mkuu wa Hungary Viktor OrbanPicha: picture-alliance/AP Photo/G. Vanden Wijngaer

Waziri huyo mkuu wa Hungary anajulikana kwa msimamo wake mkali dhidi ya wahamiaji, lakini ikumbukwe kwamba mwanasiasa wa kwanza wa kigeni kumtembelea Trump alikuwa kinara wa (Brexit) Nigel Farage kutoka Uingereza, wakati huo Trump alikuwa bado ni rais mteule. Ikumbukwe pia katika wiki hii tu Trump huyo huyo amemtaja kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un kuwa ni mtu mwenye "heshima sana."

Kushoto: Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron. Kulia: Rais wa Marekani Donald Trump
Kushoto: Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron. Kulia: Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Reuters/J. Ernst

Na kulingana na misingi hiyo, kualikwa kwa Macron, rais wa nchi mshirika wa jadi wa Marekani nchi ambayo pia ni mwanachama muhimu na mtetezi wa Umoja wa Ulaya, halikuwa ni jambo rahisi. Hayo kwa hakika ni mafanikio makubwa kwa Macron mwenyewe na kwa Brussels pia.

Pili, Macron ameitumia ziara yake, na hasa hotuba yake mbele ya bunge la Marekani, kuelezea na kutetea maadili ya nchi za Magharibi na juu ya umuhimu wa Umoja wa Ulaya. Kwa hisia na  ufasaha, ameelezea ndoto yake kuhusu ulimwengu ambayo inaweza kuwa suluhisho dhidi ya mtazamo wa Trump kuhusu ulimwengu. Mawazo yake mbadala yanakaribishwa na pia ni ya  muhimu sana.

Mwandishi: Zainab Aziz/ Knigge, Michael/p.dw.com/p/2wg19

Mhariri: Caro Robi