1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Myanmar yapongezwa kwa uchaguzi wa amani

10 Novemba 2015

Matokeo ya awali katika uchaguzi wa kihistoria nchini Myanmar yanaonesha chama cha upinzani cha NLD kinaelekea kupata ushindi wa kishindo.

https://p.dw.com/p/1H3TD
Myanmar Parlamentswahl Sieg Aung San Suu Kyi
Wanachama wa chama cha NLD nchini Myanmar wakishangiria ushindiPicha: Reuters/J. Silva

Lakini sio tu chama cha NLD ambacho kimeshinda anasema hivyo Rodion Ebbighausen katika uhariri wake.

Mapambano bila kutumia nguvu nchini Myanmar ya miongo kadhaa chini ya uongozi wa mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel Aung San Suu Kyi yanaonekana kuelekea kufikia malengo yake.

Kwa mara ya kwanza katika historia, chama cha Suu Kyi , cha National League for Democracy (NLD) , kitakuwa na fursa ya kulibadilisha taifa hilo la kusini mashariki mwa bara la Asia kwa mujibu wa mtazamo wake.

Chama tawala cha Muungano wa mshikamano na maendeleo , Union Solidarity and Development (USDP) kimeshindwa vibaya katika uchaguzi huo. Lakini pamoja na hayo chama hicho kinastahili kiwango fulani cha sifa.

Wakubali kushindwa

Baadhi ya wanachama wake maarufu tayari wamekubali kushindwa na kusisitiza kwamba watakubali matokeo ya uchaguzi , bila kujali matokeo. Hii haikuwa hivyo hapo zamani wakati taifa hilo lilipofanya uchaguzi wa serikali , kama historia ya nchi hiyo inavyioonesha.

Wakati huo huo , mtu hapaswi kusahau kwamba , kwa hakika ilikuwa jeshi na chama cha USDP ambavyo vilianzisha hatua za mabadiliko ya kisiasa. Kwa hiyo wao wameweka kipengee kulinda maslahi yao.

Ebbighausen Rodion Kommentarbild App
Mwandishi wa maoni Rodion EbbighausenPicha: DW

Kwa mfano , asilimia 25 ya viti vya bunge vimetengwa kwa wawakilishi wa jeshi, wakitoa kwa watu hao wanaovalia sare za jeshi haki ya kuzuwia mabadiliko katika katiba ya nchi hiyo.

Kuachia madaraka, hata kama ni kwa kiasi kidogo, si jambo dogo. Hivi sasa mtu anatumai kwamba jeshi litaendelea kutekeleza sheria ilizoweka, na kwamba huenda taratibu kutakuwa na nafasi zaidi za kufanya mageuzi.

Hata tume ya uchaguzi imeshinda. Licha ya ripoti za awali za mapungufu na uchelewesho, wengi wa waangalizi wa uchaguzi wamesema uchaguzi huo umeandaliwa vizuri na kwamba ulikuwa huru na wa haki.

Ushindi wa wananchi

Lakini washindi wakubwa ni watu wa Myanmar. Idadi ya watu asilimia 80 waliojitokeza kupiga kura inaonesha jinsi watu wanavyoangalia maslahi ya baadaye ya nchi yao. Mtu anaweza kuona jinsi gani watu wa Myanmar walivyokuwa wanajiamini wakati wakipiga kura. Kwa fahari kubwa na kujiamini walipiga kura kutaka mageuzi.

Na watu wanapaswa kuendelea kujiamini na bila wasi wasi , kwa kuwa kiwango cha mabadiliko yaliyoahidiwa na chama cha NLD, na kile kinachotarajiwa kufutia ushindi wa uchaguzi , hayatakuwa rahisi kufikiwa.

Miongoni mwa changamoto za kupambana nazo , sio tu haki maalum ambayo katiba inatoa kwa jeshi, lakini pia maendeleo ya mfumo uliolenga kuunda nafasi mpya za kazi , kupambana na rushwa na kuimarisha mfumo wa kutoa huduma ya afya pamoja na ujumuisho mzuri wa watu wa jamii za wachache kwa upande wa makabila na kidini.

Licha ya kwamba watu wa Myanmar watapaswa kuwa wavumilivu, matarajio hayajawahi kuwa mazuri katika miongo kadhaa.

Mwandishi : Rodion Ebbighausen / ZR / Sekione Kitojo

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman