1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni kuhusu EPAs yatofautiana serikalini Ufaransa

P.Martin25 Aprili 2008

Ufaransa ikijitayarisha kupokea wadhifa wa rais wa Umoja wa Ulaya katika mwezi wa Julai,mada mojawapo kuu katika ajenda yake itahusika na Mkataba wa Ubia wa Kiuchumi(EPAs).

https://p.dw.com/p/DoOs
French President Nicolas Sarkozy looks on as he speaks during a press conference following a two-day EU summit in Brussels, Friday, March 14, 2008. European Union leaders insist at summit talks that the costly fight against climate change will not come at the expense of their economies, with France warning that countries that don't sign up to international anti-pollution rules should face trade sanctions. (AP Photo/Michel Euler)
Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy akizungumza katika mkutano wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels.Picha: AP

Msimamo rasmi wa Ufaransa kuhusu EPAs bado haujulikani wazi wazi,licha ya kuwa ni muda mfupi tu uliobaki kabla ya nchi hiyo kushika wadhifa wa rais wa Umoja wa Ulaya unaozunguka kila miezi sita.Kawaida ni Kamisheni ya Ulaya mjini Brussels iliyo na mamlaka ya kuujadili Mkataba wa Ubia wa Kiuchumi pamoja na ACP yaani nchi za Afrika,Karibea na Pacifik,kwa niaba ya wanachama wote wa Umoja wa Ulaya.

Hiyo basi inatumiwa na Ufaransa kama sababu ya kutounga mkono wala kupinga midahalo inayohusika na EPAs anasema Jean-Denis Crola,afisa wa tawi la OXFAM nchini Ufaransa linalogombea haki ya kiuchumi.Anasema, nchi za ACP zinatiwa vishindo na Kamisheni ya Ulaya kutia saini Mkataba wa Ubia wa Kiuchumi.

Rasmi,sera za Ufaransa kuhusu nchi za ACP hupendelea maendeleo ya kiuchumi katika mataifa ya kanda hizo.Juu ya hivyo,serikali hii ya Ufaransa imejiepusha kujibu masuala yanayohusika na EPAs.Hata hivyo,afisa mmoja katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa amesema,Ufaransa inapendelea kuzipatia nchi za ACP hali bora za kuingiza mazao yake katika masoko ya Ulaya kulingana na sheria za Shirika la Biashara Duniani-WTO.

Lakini kuambatana na mfumo unaopendekezwa na Brussels,masoko ya bidhaa na huduma za nchi za Umoja wa Ulaya na zile za ACP yatafunguliwa kwa pande zote mbili.Hiyo humaanisha kuwa uchumi wa nchi za ACP utashindana moja kwa moja na mazao na makampuni ya nchi za Ulaya.

Suala hilo ndio linawatia wasiwasi wakosoaji wa EPAs na bado halijashughulikiwa rasmi na Ufaransa.Hali inachanganyika zaidi kwa sababu nchini Ufaransa wizara nyingi zina usemi kuhusu Mkataba wa Ubia wa Kiuchumi.Hizo ni wizara za Mambo ya Nje;Kilimo na Biashara ya Nje.Isitoshe,maoni ya wizara hizo yanatofautiana pia.

Lakini yadhihirika kuwa sasa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa imeingiwa na wasiwasi kwa sababu ya ghasia zilizozuka hivi karibuni katika nchi za ACP kuhusika na chakula.Kwa mujibu wa wizara hiyo,Ufaransa ingependa pia kujadili suala la usalama wa chakula katika midahalo ya EPAs.Suala hilo lina umuhimu mkubwa mno hasa wakati huu ambapo vyakula huzidi kupanda bei.

Lakini haijulikani vipi na lini Ufaransa itasuluhisha tatizo hilo itakaposhika wadhifa wa rais katika umoja wa Ulaya. Kwani wizara ya kilimo ya nchi hiyo imeeleza msimamo wake waziwazi.Wizara hiyo inataka Mkataba wa Ubia wa Kiuchumi utiwe saini kama ulivyo,kwa sababu wizara hiyo inataka masoko zaidi kwa mazao ya Ufaransa.Hata maoni ya Wizara ya Nje ya Ufaransa na yale ya Kamisheni ya Ulaya yanatofautiana.

Wizara ya Nje ya Ufaransa inasema,Ufaransa inaunga mkono jitahada za baadhi kubwa ya nchi za ACP na vile vile hupendelea kuujadili Mkataba wa Ubia wa Kiuchumi pamoja na nchi za maeneo hayo.Lakini mkakati wa Brussels ni tofauti kabisa anasema Frederic Viale wa shirika moja la Kifaransa ATTAC.Kwa mujibu wa shirika hilo lisilo la kiserikali,Umoja wa Ulaya unataka kujadiliana na kila nchi mikataba mbali mbali kuhusika na bidhaa na huduma tofauti.Sasa mpira ndio upo kona ya Ufaransa itakayoshika wadhifa wa rais wa Umoja wa Ulaya kwa muda wa miezi sita kuanzia Julai.