1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kwa msaada wa Emmanuel Macron Umoja wa Ulaya bado una nafasi

Yusra Buwayhid
11 Mei 2018

Akipokea tuzo ya Charlemagne Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameusisitiza Umoja wa Ulaya kufanya mabadiliko. Mwandishi wa DW Bernd Riegert anasema katika uhariri wake hakuna muda wa kupoteza katika kutekeleza wito huo.

https://p.dw.com/p/2xWSA
Deutschland Emmanuel Macron in Aachen
Picha: DW/A. Noll

Ni mwaka mmoja tu tokea kuingia madarakani, lakini anastahili kupokea Tuzo ya Kimataifa ya Charlemagne ya mjini Aachen. Katika hotuba yake Rais huyo wa Ufaransa Emmanuel Macron ameonyesha kwamba ana malengo ya wazi kabisa kwa ajili ya Umoja wa Ulaya, na ana nia na uwezo wa kuleta mabadiliko katika umoja huo. Akiwa na miaka 40 pekee, mwanasiasa huyo kwa kweli ana uwezo wa kuhamasiha hadhara inayomsikiliza, kama ilivyoshuhudiwa katika ukumbi wa mji wa magharibi mwa Ujerumani wa Aachen na katika viwanja vya nje ya ukumbi huo ambako watu walikusanyika wakimuangalia mubashara kupitia televisheni. Macron anajua namna ya kuwafanya watu wamkubali; na wanahamasishwa sana na mawazo yake.

Anaposema Umoja wa Ulaya hauwezi kuwa dhaifu ikizingatiwa changamoto unazokabiliana nazo juu ya sera zake za ndani na za kigeni, basi ni kitu kinachoonekana dhahiri. Umoja wa Ulaya unapaswa kuchukua hatua za kuwa na mwanzo mpya, na unatakiwa kuchukua hatua hizo hivi sasa. Hio ndiyo nadharia ya msingi ya Macron. Na Umoja wa Ulaya hautakiwi kuwa na hofu. Na kwa kusema hivyo Macron pia alikuwa anajaribu kuwahamasisha wale raia wa barani Ulaya ambao wameanza kukata tamaa. Macron amesema mshikamano miongoni mwa watu wa umoja huo lazima ujengwe upya, iwe juu ya masuala ya kiuchumi au uhamiaji. Hisia kali za uzalendo lazima zizuiliwe, na utaratibu wa ulimwengu wa kimataifa unaohusisha nchi mbalimbali unapaswa kuanzishwa. Macron anajiangalia kama chaguo mbadala kwa Rais wa Marekani Donald Trump.

Wito wa mshikamano

Mwito wake wa kuutaka Umoja wa Ulaya kutokubali kugawanywa ni wa kweli na wa kuaminika. Vitisho vya hivi karibuni dhidi ya mshikamano wa Umoja wa Ulaya vinajitokeza katika mchakato wa Brexit wa Uingereza kujiondoa katika umoja huo,  na vuguvugu jipya la utaifa za utaifa linalojitokeza  nchini Poland na Hungary, na sasa nchini Italia pia. Macron, ambaye alishinda uchaguzi nchini Ufaransa mwaka jana kwa kuahidi kuwa muaminifu kwa bara la Ulaya, anaweza kuwa fursa ya mwisho kwa umoja huo kupata mtu wa kuunganisha.

Riegert Bernd Kommentarbild App
Riegert Bernd mwandishi habari wa DW kutoka mjini Brussels, Ubelgiji

Kilichoonekana wazi zaidi katika sherehe hizo za Tuzo ya Charlemagne ilikuwa ni kwamba Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alikubaliana na Macron juu ya karibu kila kitu. Aliahidi kuwa Ujerumani na Ufaransa zitazirejesha tena pamoja nchi za Umoja wa Ulaya.

Mapendekezo ya Macron ni thabiti, ya Maerkel bado hayajulikani wazi. Ameahidi kuyaweka wazi wakati wa mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya utakaofaynika mwishoni mwa mwezi Juni. Ujerumani na Ufaransa zote mbili zimekubali kwamba Umoja wa Ulaya lazima uchukuwe jukumu kubwa zaidi kupitia sera zake za kigeni – hasa katika eneo la Mashariki ya Kati. Makubaliano ya kinyuklia na Iran lazima yadumishwe kwa uwezo wote. Merkel amerudia kauli yake kwamba Ulaya haiwezi tena kuitegemea Marekani kama msaidizi wake katika masuala ya usalama na Ulinzi.

Wito dhidi ya uzalendo

Katika hotuba yake, Macron kwa mara nyingine tena ameweka wazi kabisa kwamba kutakuwepo na kazi kubwa katika kuendeleza maendeleo  ya Umoja wa Ulaya.  Ujerumani lazima iachane na upinzani wake dhidi ya kile kinachojulikana kama ‘uhamisho wa umoja’ - ambapo malipo huweza kutoka katika nchi tajiri kwenda nchi maskini ndani ya Umoja wa Ulaya. Ufaransa lazima iachane na upinzani wake na iwe tayari kukubali mabadiliko ya mkataba wa EU, yaani iwe tayari kujitolea kidemokrasia.

Hii ni njia ya kijasiri, lakini Macron amegundua kwamba kama hakutokuwepo na hali ya kujitolea na kujiweka hatarini basi hakuna kitakachopatikana. Rais wa Ufaransa alifanikiwa kuwavuta upande wake wageni wote waalikwa katika hafla ya tuzo ya Charlemagn,e wenye kuunga mkono kuendelezwa kwa Umoja wa Ulaya. Na sasa lazima awashawishi wale wenye wasiwasi na umoja huo ikiwa ni amoja na Poland, Hungary, Italy na kwengineko. Na hilo ni jukumu gumu zaidi kuliko kutoa hotuba ya kusisimua.

Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban aliichagua Alhamis miongoni mwa siku zote, siku ya hafla ya kutolewa Tuzo ya Kimataifa ya Charlemagne, kuthibitisha mwisho wa “demokrasia ya kiliberali.” Hatua hiyo inasisimua mwili. Ilipokaribia mwisho wa hafla ya tuzo ya Charlemagne, kila mmoja aliekuwepo Aachen alitambua  kwamba: Tunahitaji watu zaidi kama Macron barani Ulaya.

Mwandishi: Yusra Buwayhid

Tahariri: Bernd Riegert

Mhariri: Daniel Gakuba