1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Maafa yaendelea Sudan Kusini

11 Julai 2016

Miaka mitano baada ya kujipatia uhuru Sudan Kusini bado ni nchi ya maafa makubwa. Katika maoni yake mwandishi wetu Daniel Pelz anasema hali hiyo haitaweza kubadilishwa bila ya viongozi wa nchi hiyo wenyewe kubadilika

https://p.dw.com/p/1JM0K
Miaka mitano ya uhuru wa Sudan Kusini
Miaka mitano ya uhuru wa Sudan KusiniPicha: picture-alliance/dpa/M. Messara

Serikali ya Sudan Kusini imeamua kuahirisha sherehe za kuadhimisha siku ya uhuru. Ni hatua adilifu katika nchi inayotawaliwa na wanasiasa wanaojali maslahi yao tu badala ya watu wao.

Waziri wa habari wa nchi hiyo amesema serikali imeamua kuzitumia raslimali chache zilizopo kwa ajili ya mambo muhimu zaidi badala ya kuziponda raslimali hizo kwa ajili ya tafrija.

Ni uamuzi wa busara na hasa kwa sababu umechukuliwa na serikali ambayo katika miaka iliyopita ilitumia fedha kwa ajili ya mambo mengine, badala ya yale muhimu.

Kwa mfano serikali hiyo ilikuwa inalikimu jeshi kubwa kupita kiasi badala ya kuwekeza fedha katika sekta za elimu na afya.

Hakuna la kusherehekea

Miaka mitano ya uhuru ilikuwa migumu kwa taifa hilo jipya na katika kipindi cha miaka miwili iliyopita mambo yalizidi kwenda mrama. Na sasa ishara zote zinaonyesha kuwa Sudan Kusini inaelekea kwenye mkwamo.

Sudan Friedensabkommen Südsudan unterzeichnet
Siku za neema nchini Suda KusiniPicha: picture-alliance/dpa/S. Morrison

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa thuluthi moja ya watu wa nchi hiyo wamo katika hatari ya kukumbwa na njaa. Mamilioni bado ni wakimbizi wa ndani na wanahofia kurejea makwao.Sarafu ya Sudan Kusini inaendelea kupoteza thamani kwa kiwango kikubwa.

Na kana kwamba mazatizo hayo hayatoshi sasa pana kundi la waasi linalowasumbua watu katika sehemu ya magharibi ambayo hapo awali ilikuwa tulivu. Waasi hao wamewatimua raia 700,000 kutoka majumbani mwao.

Yumkini litakuwa jambo la kikatili kusema kwamba hayo ni mambo ya kawaida kwa watu wa Sudan Kusini. Washambuliaji ni watu tofauti lakini mashambulio ni yale yale. Hakuna watu wengine, kwingineko duniani wanaonyimwa haki zao kama watu wa Sudan Kusini, haki ambazo kila mwanadamu anastahili kuzipata: haki ya kuishi kwa amani na haki ya kupata chakula cha kustosha, haki ya kupata elimu na afya.

Maafa ya watu wa Sudan Kusini yalianzia tangu siku za kupigania uhuru. Lakini uhuru umeleta amani inayoyumba yumba na angalau kiwango fulani cha maendeleo katika sehemu nyingi za nchi. Lakini sasa kila kitu kinasambaratika.

Lakini viongozi wa nchi hiyo hawataki kusikia chochote na badala yake wanatumia nadharia za uzushi juu ya nani ameyasababisha maafa yanayotokea - Umoja wa Mataifa, vyombo vya habari vya kimataifa na wengine.

Lakini endapo busara ingetumika, hali ingeliweza kubadilishwa.Suluhisho sahili limekuwa linatumika kwa miaka mingi; ikiwa watu wako wanakabiliwa na matatizo basi omba msaada wa jumuiya ya kimataifa. Lakini mkakati huo haufai tena.

Viongozi wa Sudan Kusini wanapaswa kuongoza juhudi za kuibadilisha hali ya nchi yao. Hakuna mtu mwengine wa kuifanya kazi hiyo. Haitoshi kuunda serikali ya umoja wa kitaifa tu.Viongozi hao wanapaswa kuziweka kando tofauti zao na waandae mpango wa kuindeleza nchi yao.

Mwandishi: Pelz Daniel

Mfasiri: Mtullya Abdu

Mhariri: Mohammed Khelef