1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Macron aitumia G7 kuthibitisha umahiri wa diplomasia

Mohammed Khelef
26 Agosti 2019

Rais Macron amedhihirisha ubingwa wake kwenye diplomasia ya kimataifa akimkiuka Rais Trump kwenye suala la Iran na hivyo kuonesha uongozi kwenye sera za nje za Umoja wa Ulaya, anaandika Barbara Wesel.

https://p.dw.com/p/3OVkl
G7-Gipfel in Frankreich | Lustige Aufnahmen
Picha: AFP/L. Marin

Rais Emmmanuel Macron wa Ufaransa anaonekana aliwekeza pakubwa kwenye kazi za matayarisho na mtaji wa kisiasa ili mkutano wa mara hii wa mataifa yenye uchumi mkubwa wa viwanda, G7, usije ukawa kituko na alama nyengine ya kushindwa, ndio maana aliwaalika wageni wa ziada na kuongeza mada zaidi kwenye ajenda na kuvunja utaratibu wa kawaida. 

Kwa kufanya hivyo, amebeba pia jukumu la kuwa kiongozi wa sera za nje za Umoja wa Ulaya. Mafanikio yake kwenye kumpiku Trump si madogo hasa kwa kuzingatia namna ambavyo kwa mara nyengine rais huyo wa Marekani alivyojidhihirisha jinsi alivyo mgeni mbaya anayependa kuwapotosha waandishi wa habari na wapita njia - hasa kwenye masuala ya sera za kibiashara.

Wakati huo huo, Trump alililalamikia jinsi vyombo vya habari vilivyoripoti hali ya wasiwasi kwenye mkutano huo wa kilele. Kila neno la ziada lililoandikwa kuwa kugeuka njia, kukosekana kwa uwajibikaji na upotoshaji kutoka upande wa Trump kungelikuwa ni kupoteza tu. Alitenda kama atendavyo kila siku.

Rais Macron alimualika Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif kama mgeni wa mshangao na akazinduwa mkakati wa kidiplomasia kandoni mwa mkutano huo wa kilele - na aliyafanya hayo mbele ya macho ya Trump.

Barbara Wesel Kommentarbild App *PROVISORISCH*
Na Barbara Wesel/DW

Kisha Trump akaonesha wazi kuchukizwa kwake na hatua hiyo huku akisisitiza kwamba mkakati pekee sahihi ni muelekeo wa kibabe unaochukuliwa na Marekani. Lakini Macron hakuruhusu atishwe, na badala yeye mwenyewe binafsi akakutana na Zarif kuangalia uwezekano wa kuwa na njia za kidiplomasia kwa ajili ya suluhisho jipya.

Licha ya kwamba hakuna matumaini makubwa, lakini katika hali ambapo kuna hatari ya kuzuka kwa mzozo wa kijeshi, jitihada yoyote ile kwa ajili ya suluhisho la amani ni ya kukaribishwa. Hili linayahusu mataifa ya Ulaya yaliyosaini mkataba wa nyuklia na Iran ambao Rais Trump alijitoa kwa kishindo mwaka jana.

Muelekeo sahihi kuhusu moto wa Amazon

Macron pia alichukuwa muelekeo sahihi kwenye kulishughulia suala la moto unaouteketeza msitu wa asili wa Amazon. Alimtishia Rais Jair Bolsonaro kwa kukataa kuidhinisha mkataba wa kibiashara baina ya Umoja wa Ulaya na Brazil ikiwa Bolsonaro hakuwazuwia watu kuuchoma msitu huo ufahamikao kama mapafu kijani ya sayari ya dunia.

Kwenye mkutano huo wa kilele, aliwashajiisha pia washiriki wengine kuziahidi Brazil na majirani zake msaada wa kivitendo kusaidia kuuzima moto huo na uoteshaji mpya wa miti. 

Kwa kila hali, rais huyo wa Ufaransa alionesha kwamba ana mbinu muafaka za kuwashughulikia wanasiasa wanaoelemea siasa za hamasa na wanaopinga demokrasia.

Anazungumza na kila mtu, lakini pia anachukuwa misimamo mikali. Na kwa upande mwengine, Bolsonaro naye alithibitisha kwamba siasa za nyundo na kibuyu cha asali zinafaa, kwani alirejea nyuma kwenye siasa zake kuelekea moto wa msitu wa Amazon na akatuma wanajeshi kwenye kuuzima.

Hata hivyo, ili kumfanya kiongozi huyo wa Brazil kutekeleza sera madhubuti zaidi za mazingira, shinikizo zaidi linahitajika. Na katika kulifanikisha hilo, Umoja wa Ulaya, mashirika ya mazingira na watumiaji wote wana wajibu wa kuutekeleza kwa kuzigomea bidhaa kutoka Brazil.

Marekani ilighadhabishwa sana kwamba Macron aliweka mada za mabadiliko ya tabianchi na moto wa Amazon kuwa za juu kwenye ajenda za vikao. Ilijiona imekabwa koo, walisema wanadiplomasia.

Washington kwa mara nyengine ilidhihirisha kwamba inatenda mambo ya ovyo kabisa linapohusika suala la sera ya mabadiliko ya tabianchi na kwamba lazima iongozwe njia na wanachama wengine wa kundi la G7.