1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano ya Ulaya na Afrika ni chui wa karatasi

Ludger Schadomsky/Mohammed Khelef9 Juni 2016

Mkuu wa Idhaa ya Kiamhara ya DW, Ludger Schadomsky, anasema makubaliano kati ya Ulaya na mataifa kudhibiti wahamiaji yanalenga tu kuwazuwia watu kuingia barani Ulaya na sio kurekebisha mfumo wa uhamiaji.

https://p.dw.com/p/1J3Qo
Mashua ya uokozi ya walinzi wa Italia baada ya kuwaokoa wahamiaji kutoka Afrika.
Mashua ya uokozi ya walinzi wa Italia baada ya kuwaokoa wahamiaji kutoka Afrika.Picha: Reuters/Marina Militare

Mwanzoni mwa wiki hii, Umoja wa Ulaya ulifikia makubaliano na mataifa kadhaa ya Afrika ili kudhibiti mmiminiko wa wahamiaji wanaokimbilia barani Ulaya, ambapo Umoja huo utatoa euro bilioni 8 kwa mataifa ya Niger, Nigeria, Senegal, Mali na Ethiopia, miongoni mwa mataifa mengine, ikiwa ni msaada wa maendeleo, usalama na sera ya viza, nayo mataifa hayo yawachukuwe wakimbizi waliokataliwa hifadhi barani Ulaya.

Kwa hivyo, sasa Umoja huo unatumia mbinu ya kutoa kwa mkono wa kulia na kutwaa kwa mkono wa kushoto, au kama ambavyo Kamisheni ya Umoja huo ilivyosema mwanzoni mwa wiki hii: "ni nyenzo za mchanganyiko baina ya nzuri na mbaya".

Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini, alifikia umbali wa kuyapa makubaliano hayo jina la "Mapinduzi ya Corpenica" kwenye sera ya nje ya Umoja huo. Ni kweli pia kuwa mawazo ya kimapinduzi ya Copernicus yanatambuliwa miaka 200 baada ya kifo chake.

Lakini ukweli ni kuwa makubaliano haya yanayotukuzwa kama mpango mkuu, ni kukiri kwa Umoja wa Ulaya kwamba sera yake ya wakimbizi hadi sasa imeshindwa vibaya sana, hasa linapohusika suala la Afrika.

Tatizo si kukosekana mipango

Hakujawahi kuwapo na upungufu wa miradi na mipango, ikiwa na majina ya kupendeza kama Mchakato wa Khartoum au Tamko la Valletta, ambayo inatazamiwa kulimaliza kabisa suala la mmiminiko wa wahamiaji. Kwa bahati mbaya, haifanyi kazi hata chembe.

Kwa mfano, Umoja wa Ulaya unasema ushirikiano na Libya lazima uimarishwe, lakini kwani si waziri wa mambo ya nje wa nchi ameshatangaza kuwa haiko tayari kuwachukuwa wakimbizi wanaorejeshwa kwa namna yoyote ile? Na, juu ya yote, ni Libya ipi hiyo kati ya Libya tele ndogo ndogo zilizopo sasa, ambayo wanaizungumzia?

Hapana, kwa hakika si viongozi wa Ulaya ambao sasa wanatumia mbinu ya kutowa na kupoka, bali ni watawala wa kiimla barani Afrika ambao bila aibu wanautumia mmiminiko wa wakimbizi kama njia ya kupata wakitakacho kutoka Ulaya.

Umoja wa Ulaya haujawa tayari kukomesha uhamiaji haramu

Brussels haijaelewa mpaka sasa kuwa hao inaowaita washirika wake barani Afrika hawana haja yoyote ya kuwazuwia wahamiaji, wengi wao wakiwa vijana wa kiume, kuhama makwao. Bali ni kinyume chake: nchini Eritrea, wanajeshi wa ngazi za juu, kwa mujibu wa vyanzo vya uhakika, wanajitengeneza fedha nzuri tu, kwa kufanya biashara ya kuwatorosha watu wao wenyewe.

Wengi nchini Somalia, kama ilivyo kwa tabaka la wanasiasa mafisadi huko, wanaishi kwa fedha zinazotumwa kwao na ndugu zao walio barani Ulaya. Kwengine Afrika, watawala wanafurahikia sana kuwaaga vijana wasio na ajira, ambao kwao ni waleta fujo wasiodhibitika.

Makubaliano hayo ya siku ya Jumanne yaliyotokana na mawazo ya Kikopernika kwa maafisa wa uhamiaji, yakiambiwa yana lengo la kuimarisha maendeleo ya kiuchumi kwenye mataifa wanayotokea wahamiaji, na hivyo kuwapa watu matumaini ya kuwa na mustakbali mzuri huko huko waliko bila kuzihama nchi zao, ni makongwe kama lilivyo suala la misaada kwa bara la Afrika. Nalo limeshindwa vibaya.

Umoja wa Ulaya unapoambatanisha makubaliano hayo na kitisho cha nchi kupoteza makubaliano yake ya kibiashara na Ulaya, endapo itashindwa kuyatimiza, ni kichekesho. Maana, baada ya yote, ni makubaliano hayo ya kibiashara yasiyo ya haki ambayo ni sehemu ya sababu za maelfu ya wakulima na wavuvi wa Kiafrika kuacha majembe, ndoana, na majumba yao na kukimbilia Ulaya.

Mwandishi: Ludger Schadomsky
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Bruce Amani