1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Marekani miaka 20 baada ya Septemba 11

11 Septemba 2021

Septemba 11, 2001 ilileta mabadiliko makubwa. Kujiondoa kwa Marekani huko Afghanistan miaka 20 baadaye ni uthibitisho kwamba Washington sasa inaweka masilahi ya ndani juu ya kila kitu, anasema mwandishi wa DW, Ines Pohl.

https://p.dw.com/p/40Aal
USA | Terroranschlag am 11. September 2001
Picha: Chao Soi Cheong/AP/picture alliance

Shambulio la kigaidi la Septemba 11 2001, liliiiumiza Marekani moyoni kwa namna tofauti. Shambulio la ukubwa huu halikuwahi kutokea katika ardhi ya nchi hiyo hapo kabla. Siyo tu kwa kuzungumzia idadi ya watu waliokufa ama waliojeruhiwa. Lakini pia usahihi wa namna magaidi walivyoangamiza alama za uwezo wa kiuchumi na kijeshi wa nchi hiyo duniani, ndani ya saa moja. Pengine ni juhudi tu za abiria wenye ujasiri ndizo zilizosaidia hata ndege ya nne ikashindwa kuwa ndege ya kifo kwa kuishambulia ikulu ya White house au majengo ya bunge, Capitol. 

Leo ni miaka 20 baadaye. Mshtuko wa mashambulio ya Septemba 11, ungeweza kuwa umeshasahaulika hasa kwa watu wenye chini ya umri wa miaka 30 ambao hawana kumbukumbu nzuri ya siku ya tukio. Lakini kwa Wamarekani wengine wanaoishi mbali na miji ya New York ama Washington, matukio yamekuwa sehemu ya historia.

04 | Interview Armin Laschet, Ines Pohl
Ines Pohl wa DWPicha: DW/R. Oberhammer

Tahadhari za kiusalama katika viwanja vya ndege, huenda bado zinakera, lakini imewapasa watu kuzoea misururu mirefu, kuvua viatu kwa hiyari na wako tayari kulipa dola nne kwa ajili ya chupa ya maji katika wakati wa ukaguzi.

Kwa msingi huo, kumbukumbu ya miaka  20 ya mashambulizi ya kigaidi ya mwaka 2001 ingeweza kubadilika kama Rais wa sasa Joe Biden asingehusisha suala la kuondolewa kwa wanajeshi nchini Afghanistan na tarehe hii. Aliitaja Septemba 11 kama siku ambayo wanajeshi wote wa Marekani wangekuwa wamekwishakuondoka kwenye taifa hilo. Bila shaka ilikuwa ni kwa nia ya kuashiria kuwa operesheni hiyo imekwisha kwa mafanikio.

Kwa kuangalia picha za sasa za Kabul, ni ngumu kuzungumzia mafanikio ya sera za kigeni. Na siasa za ndani za namna ya kuwashughulikia wakimbizi wa Afghanistan, zimefufua upya hofu na chuki dhidi ya Uislamu zilizokuwepo katika siku za awali baada ya shambulio la Septemba 11.

Sasa inaanza kuwa dhahiri kuwa Waislamu watafanywa kuwa mpira wa kisiasa na kampeni chafu katika uchaguzi wa katikati ya muhula. Picha za zamani za kutisha zitatumiwa hasa kwa sababu hiyo.

Ili kufahamu kinachoendelea sasa, mara nyingi kutazama ya nyuma kunasaidia. Septemba 2001, ulikuwa ni mwaka wa kwanza wa George W. Bush madarakani kama Rais wa Marekani. Alipokea pongezi nyingi kwa kutangaza kwamba atamuwinda mhusika mkuu wa shambulio la September 11 yaani Osama bin Laden

USA | Terroranschlag am 11. September 2001
Timu ya uokozi wakati wa tukio la Septemba 11Picha: Ron Agam/Getty Images

Kwa miaka mingi mabilioni ya fedha yameelekezwa kwa kile kinachoitwa vita dhidi ya ugaidi, na kwa pamoja, taasisi ya ujasusi na jeshi vimeboreshwa. Imekuwa hadithi iliyokubalika kuwa Marekani inatishiwa kutoka nje na kila kitu kinapaswa kufanyika ili kuondoa kitisho hicho mara moja.

Lakini kila miaka inavyokwenda, taswira za majengo yaliyoanguka katika shambulio la kigaidi la Septemba 11 zinavyozidi kufifia, ndivyo ulivyopungua utayari wa kuangamiza maisha ya watu wengi na kutumia mabilioni kwa ajili ya vita ambavyo vilionekana kama visivyokwisha. Ili kuhalalisha vita, angalau kuuwawa kwa Osama Bin Laden mwaka 2011, kimsingi hakukuwa tena kuhusu mapambano dhidi ya mitandao ya kigaidi.

Jambo la msingi lilikuwa kuunga mkono demokrasia kwa lengo la kuifanya Afghanistan iwe nchi yenye serikali yenye muundo wa kimagharibi. Ndoto hii imekwisha kwani sasa Joe Biden anaonesha bila mashaka kuwa Marekani inawasilisha shughuli za sera yake ya kigeni kwa ajili ya maslahi yake yenyewe. Ushiriki wake wa kijeshi katika mataifa mengine utaendelea kupunguzwa zaidi. Rais Biden atajikita zaidi kwenye mahitaji ya kisiasa ya nchini mwake kama vile kuboresha miundombinu,  na vita dhidi ya janga la mabadiliko ya tabia nchi.