1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Obama arudi nyuma

29 Mei 2014

Licha ya Rais Barack Obama kutandika upya misingi ya sera yake ya nje na usalama kuwajibu wakosoaji wake, Gero Schließ anasema bado Marekani haijalijua jukumu lake kwenye dunia inayobadilika kwa kasi.

https://p.dw.com/p/1C8mn
Gero Schließ wa Deutsche Welle, Washington.
Gero Schließ wa Deutsche Welle, Washington.Picha: DW/P. Henriksen

Miaka miwili na nusu kabla ya kumaliza kipindi chake cha urais, Obama anazidi kujiweka kwenye eneo la kujibu shutuma. Sio tu kwamba wanajeshi wa Kimarekani wanarudi nyuma, bali hata amiri jeshi mkuu wao.

Kwa hotuba yake hiyo kwenye Chuo cha Kijeshi cha West Point, Obama anajaribu kubadili mbinu na kuamsha imani mpya miongoni mwa washirika wake. Bahati mbaya, nalo hakufanikiwa.

Lakini kilicho wazi ni namna Rais Obama anavyojikuta kwenye hali mbaya sana kuufahamu ulimwengu. Ameitoa Marekani katika vita viwili vyenye gharama kubwa sana na anajitahidi kupambana na ushawishi wa kuiingiza nchini hiyo kwenye operesheni nyengine za kijeshi, lakini anachopata ni kukosolewa vikali ndani na nje ya nchi yake. Viwango vya kukubalika ndani ya Marekani viko mashakani, na havionekani kuwa vizuri kwenye heshima yake kimataifa.

Kujishuku na kujificha

Hotuba yake haikuwa na mvuto – si kwa hisia, si kwa hoja. Bado maswali mengi yamebakia bila majibu juu ya mustakabali wa sera yake ya nje na usalama. Rais huyu anayeonekana kuwa na kihoro, alitumia muda mrefu kuangaza nyuma badala ya mbele.

Kama ambavyo imewahi kutokea mara kadhaa katika hali kama hii, Obama alionekana kujilinda tu.

Ni kweli, amefanya kama alivyoahidi katika suala la kuvimaliza vita vya Iraq, na hadi mwishoni mwa kipindi chake cha urais, idadi ndogo kabisa ya wanajeshi watakuwa wamesalia nchini Afghanistan.

Lakini matokeo yake ni yapi? Iraq inatumbukia kwenye ghasia na machafuko, na Afghanistan inatishia kumalizikia kwenye jaala hiyo hiyo.

Dunia inabadilika kwa kasi

Kilicho kweli pia ni kwamba hii dunia inabadilika kwa kasi ya haraka, na utatuaji wa migogoro na mizozo umekuwa changamano sana.

Kwa kauli kwamba “Marekani lazima iendelee kuongoza kwenye jukwaa la kilimwengu,” Obama alikuwa anaendelea kusisitiza kwamba nchi yake inaendelea kuwa na wasta mkubwa duniani, licha ya kuondosha wanajeshi na kujirejesha yenyewe nyuma kutoka safu ya mbele ya medani za kivita.

Lakini Marekani chini ya Obama sio tena taifa lenye umuhimu mkubwa namna lilivyokuwa wakati aliyekuwa waziri wa mambo ya nje Madeleine Albright, alipoyapa maana maneno haya.

Nchi hii, ambayo imebakia kuwa taifa kubwa, bado haijaliona jukumu lake kwenye dunia hii inayobadilika. Safari hii, ndani ya hotuba ya Obama mtu anaweza kugundua mashaka na ukosefu wa uhakika zaidi kuliko wakati mwengine wowote hapo kabla.

Na huo sio uongozi.

Mwandishi: Gero Schließ
Tafsiri:Mohammed Khelef
Mhariri: Oummilkheir Hamidou