1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Rais Jonathan 'ajikosha' kwa sheria dhidi ya ushoga

15 Januari 2014

Wiki chache tu baada ya bunge kuupitisha mswaada wa kupiga marufuku ndoa za jinsia moja, Rais Goodluck Jonathan ameusaini kuwa sheria yumkini akitaka Wanigeria wamkumbuke angalau kwa hili ikiwa si kwa mengine yote.

https://p.dw.com/p/1Aqjv

Badala ya kufanya siasa kwa ajili ya nchi yake, amekuwa akipambana kwa miezi mingi sasa dhidi ya majaribio ya kumzuia kugombea tena urais kwenye uchaguzi wa mwaka 2015.

Kwa kusaini sheria hii, hatimaye Rais Jonathan anaweza kuwa anatafuta ridhaa ya watu. Hata hivyo, sheria hiyo ni mbaya hata kama Wanigeria wengi wanaamini kinyume chake.

Mkuu wa Idhaa ya DW Kihausa, Thomas Mösch.
Mkuu wa Idhaa ya DW Kihausa, Thomas Mösch.Picha: DW

Kwanza, suala sio kwamba sheria hiyo inakataza ndoa za jinsia moja. Hilo si jambo la ajabu kwa Nigeria, ambako hakuna anayeichukulia ndoa hiyo kuwa sahihi. Lakini sheria hiyo inaitafsiri ndoa ya jinsia moja kama mahusiano yoyote yale kati ya wanaume wawili au wanawake wawili.

Fasili hii ya jumla jamala inaingilia maisha binafsi ya mtu, kwani kinachofanywa na watu wazima wawili nyumbani mwao, si suala la serikali. Kuwa na idadi kubwa ya watu wanaopinga jambo hilo, hakuwapi haki ya kuwazuia wachache kufanya wayapendayo kwenye maisha yao binafsi.

Adhabu kwa kila mtu

Pili, sheria hii mpya inatishia kuwaadhibu wale wanaowaunga mkono wenye mahusiano hayo au jumuiya zinazopigania haki zao. Hili ni hatari kwa marafiki na familia ambazo zinalazimishwa kuwakana watoto wao kwa sababu tu wao ni mashoga.

Zaidi inavunja haki za watu ambao watataka kujikinga na Virusi vya Ukimvi na maradhi mengine yasambazwayo kwa ngono, kwa sababu hawatakiwi kuzungumzia waziwazi baadhi ya mambo fulani.

Kwa ujumla, mtu anaweza kujiuliza sheria hii imekusudiwa kumtumikia nani, katika nchi ambayo tayari matendo ya kishoga yanaadhibiwa kwa vifungo vya muda mrefu gerezani. Katika majimbo ya Kiislamu, kaskazini mwa nchi hiyo, shoga anaweza hata kuhukumiwa kifo.

Hapa wanasiasa wanalitenga zaidi kundi ambalo tayari limeshatengwa na jamii, ili kujikosha na kuporomoka kwao wenyewe kimaadili. Kwa lengo la kutimiza dhamira hiyo, wanasiasa wa Nigeria wametumia kila uongo na upotoshaji.

Visingizio vya wanasiasa

Mfano mmoja ni kusema kwamba serikali za Magharibi zinatulazimisha kuhalalisha ndoa za jinsia moja. Lakini ukweli ni kuwa hakuna nchi ya Magharibi iliyoitaka Nigeria kuhalalisha ndoa hizo. Zinalolipinga ni kuwatupa watu gerezani au kuwauwa kwa sababu tu wamechagua kuwa na mahusiano yasiyopendwa na wengi kwenye jamii.

Mfano mwengine ni kusema kwamba dini zote kuu zinakataza vikali mahusiano ya kimapenzi ya jinsia moja. Hilo linaweza kuwa kweli nchini Nigeria na katika nchi nyengine nyingi za Kiafrika, lakini si kwa dunia nzima.

Afrika ya Kusini, kwa mfano, Kanisa Anglikana limekuwa likiwakubali waumini mashoga kwa muda mrefu sasa, kama ilivyo kwa makanisa mengi ya Kiprotestanti barani Ulaya. Hata Papa Francis ameliomba Kanisa Katoliki liwatazame mashoga kwa jicho la huruma na sio la chuki.

Wanasiasa wa Nigeria wana mambo matatizo makubwa zaidi ya kuyashughulikia. Lini bunge litalazimisha kuchukuliwe hatua za haraka za kuhakikisha utajiri wa nchi hiyo hauwafaidishi wachache tu, huku kukiwa na ombaomba tele mitaani, na watu wengi wakishindwa kulipia elimu na afya?

Tangu kumalizika uchaguzi wa mwaka 2011, hakuna ahadi yoyote ya kampeni iliyotekelezwa. Sheria dhidi ya ushoga ambao tayari umeshaharamishwa nchini humo, haibadilishi kitu.

Mwandishi: Thomas Mösch
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman