1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashaka juu ya mkataba wa amani Sudan Kusini

27 Agosti 2015

Rais wa Sudan Kusini ameutia saini mkataba wa amani na waasi wenye lengo la kuvimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyochukua muda wa miezi 20. Lakini mwandishi wetu Ludger Schadomsky anasema bado pana mashaka

https://p.dw.com/p/1GMn2
Südsudan Präsident Salva Kiir
Rais wa Sudan Kusini Salva KiirPicha: picture-alliance/dpa/P. Dhil

Rais Salva Kirr hatimaye ameutia saini mkataba wa amani na waasi,lakini siyo kabla ya Marekani,kutoa shinikizo kwa kuwasilisha mswada wa vikwazo kwenye baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Rais Salva Kiir amelazimika kutia saini, lakini haina maana kuwa ameukubali .

Alipohudhuria duru ya mwisho ya mazungumzo Rais huyo alisema kwamba haifai kutia saini mkataba wa amani, ambao hauwezi kutekelezwa. Hasimu wake,Riek Machar yaani makamu wa Rais wa siku za usoni pia anayo mashaka juu ya jinsi atakavyoweza kufanya kazi pamoja na Salva Kiir, kutokana na matatizo ya hapo awali baina yao.

Pana wasi wasi mkubwa huenda mkataba huo pia usitekelezwe. Wachunguzi kadhaa wanasema makosa makubwa yaliyofanywa wakati wa kuzinduliwa nchi mpya ya Sudan Kusini mnamo mwaka wa 2011, yanatokana na mkataba wa amani uliotiwa saini baina ya Sudan na Sudan Kusini,CPA, mnamo mwaka wa 2005.

Makosa hayo ndiyo yaliyousababisha mgogoro wa Sudan Kusini.

Tathmini hiyo inaweza kuwa sahihi, lakini siyo kabisa.Mkataba wa amani wa mwaka wa 2005 baina ya Sudan na Sudan Kusini,ulitiwa saini baada ya mazungumzo ya muda mrefu na kutokana na shinikizo kubwa la Marekani na wapatanishi wengine.

Masuala kadhaa hayakutatuliwa,ikiwa pamoja na utajiri wa maliasilia ,na mgawanyo wa mamlaka. Hali kama hiyo wakati wote ni cheche inayoweza kuwasha moto, na siyo katika Sudan Kusini tu. Lakini iwapo pangelikuwapo na dhamira, ingeliwezekana kufikia mapatano juu ya kugawana mamlaka baina ya Rais Salva Kiir na aliekuwa makamu wake, Riek Machar.

Lakini dhamira hiyo haikuwapo kutokana na ujuvi wa Salva Kiir na ugeugeu wa makamu wake ,Riek Machar .Lakini sasa wanasiasa hao hawana udhibiti tena juu ya wafuasi wao.Majenerali wao wanaua wapendavyo na wanapora mali mtindo mmoja. Lengo lao ni kujitajirisha haraka haraka.

Majenerali hao wameshawasahau wananchi waliowaunga mkono wakati wa vita vya ukombozi, vilivyochukua miongo kadhaa katika Sudan. Kutokana na Sudan Kusini kujaa silaha pomoni, mizozo juu ya ardhi,maji na raslimali zingine, haraka sana husababisha umwagikaji wa damu. Makamanda wa wanamgambo, wanapigania mamlaka na himaya, baina yao na vikosi vya jeshi la serikali, na hivyo kusababisha maafa kwa wananchi.

Watu wa Sudan Kusini wanastahiki hali bora ya maisha.

Mgogoro wa Sudan Kusini umefikia viwango vya ukatili mkubwa.Wafungwa wanafanyiwa ukatili ,na hata watoto wanauawa. Matumaini yaliyoonekana wakati wa uhuru yametoweka. Vyombo vya habari vimenyamazishwa.

Rais Salva Kiir amesema mtu anapaswa kutia saini katika jambo litakalomletea manufaa. Lakini amesahau kusema kwamba watu wa Sudan Kusini hawajayaona manufaa ya uhuru wao.

Badala ya kusherehekea kwa nderemo kubwa, kutiwa saini mkataba wa amani, ,pande zilizoshiriki katika juhudi za usuluhishi, zinapaswa kuwa tayari kuchukua hatua mwafaka, endapo mapigano yatazuka tena: pande hizo zinapaswa kutayarisha vikwazo vya silaha na vya aina nyingine, endapo damu itamwagika tena.

Mwandishi:Ludger Schadomsky

Mfasiri:Mtullya abdu.

Mhariri: