1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Ushindi wa Kenyatta una maana gani?

12 Machi 2013

Licha ya mbinu za Uhuru Kenyatta kumletea tija, nini tafsiri ya ushindi wa rais huyo mteule kwa Kenya na zipi changamoto zinazomkabili rais huyo wa nne wa taifa hilo, anayetuhumiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu?

https://p.dw.com/p/17uqT

Mtoto huyo wa baba wa taifa la Kenya, Jomo Kenyatta, alishirikiana katika uchaguzi huu na hasimu yake mkubwa, William Ruto. Kiroja cha matokeo ya uchaguzi huo ni kwamba wanasiasa wote hao wawili wanatuhumiwa na Mahakama ya Kimataifa ya mjini The Hague kuhusika na uhalifu dhidi ya ubinaadamu.

Wanatuhumiwa kuwachochea wafuasi wao wafanye fujo baada ya uchaguzi wa mwaka 2007,ambapo zaidi ya watu 1,200 walipoteza maisha yao na malaki kuyapa kisogo maskani yao.

Kawaida Wakenya huwapigia kura watu wanaotokana na makabila yao. Na safari hii wamefanya hivyo hivyo. Mipango ya vyama iliwekwa nyuma. Wakenya wengi wanafaidika kutokana na ile hali kwamba watawala hadi wakati huu wakiwatanguliza mbele watu wa makabila yao na kuwapatia nyadhifa muhimu za kiuchumi na kisiasa.

Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili, Andrea Schmidt.
Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili, Andrea Schmidt.Picha: DW

Kenyatta ni kiongozi wa kisiasa wa watu wa kabila la Kikuyu - kabila kubwa kabisa nchini humo. Makamu wake, William Ruto, ni wa kabila la Kalenjin - kabila la nne kwa ukubwa nchini Kenya.

Katika muungano wa Jubilee,"Uhuruto"- kama wanasiasa hao wawili wanavyoitwa nchini Kenya, walishirikiana kuwazinduwa wafuasi wao. Kwa namna hiyo walitaka kumzuwia mgombea wa pili mkuu wa kiti cha urais, Raila Odinga, ambaye ni wa kabila la Luo asishinde.

La Odinga, uchaguzi na mahakama

Hii ilikuwa mara ya tatu kwa Odinga kugombea kiti cha urais. Kama ilivyokuwa katika uchaguzi wa mwaka 2007, na safari hii pia anahisi kumefanyika udanganyifu - anataka kwenda mahakamani ili kubisha uhalali wa matokeo ya uchaguzi.

La muhimu kwa sasa ni kwa mahakama kushughulikia dhana za udanganyifu na kuhakikisha kila upande unayatambua matokeo ya uchaguzi. Utulivu na umoja wa taifa hilo la mchanganyiko wa makabila tofauti ndio kipaumbele ili amani ipate kuimarishwa nchini humo.

Kenyatta ni rais wa nne na kijana zaidi wa Kenya. Si Wakenya oeke yao wanapmkodolea macho, bali ulimwengu mzima unachunguza nini kitatokea. Kiongozi huyo inabidi adhihirishe kwamba yeye si rais wa watu wa kabila lake tu, bali rais wa Wakenya wote.

Anabidi autunze ushirikiano wake pamoja na Ruto, na kuendeleza mageuzi - kama ilivyotajwa katika katiba. Muhimu zaidi ni kuvifanyia mageuzi vikosi vya polisi vinavyotuhumiwa kuhusika na visa vibaya kabisa vinavyokiuka haki za binaadamu na ambavyo hadi sasa havijaandamwa kisheria.

Changamoto mbele ya jumuiya ya kimataifa

Ushindi wa Kenyatta, mwenye umri wa miaka 51, aliyesomea uchumi katika Chuo Kikuu mashuhuri kabisa cha Amherst nchini Marekani, unaweza kuzusha madhara ya kidiplomasia na kiuchumi kwa nchi hiyo.

Mwakilishi wa serikali kuu ya Ujerumani anayeshughulikia masuala ya Afrika, Günter Nooke, amesisitiza hadi hukumu itakapotolewa, Kenyatta sawa na wote wengine wanaotuhumiwa na ICC, aanasalia hawana hatia.

Kesi yao ambayo awali ilikuwa ifanyike mwezi wa Apriil imeakhirishwa, ya Ruto itasikilizwa Mei na ya Kenyatta mwezi wa Julai. Wakitiwa hatiani, basi jambo hilo linaweza kuitumbukiza Kenya katika hali ya mtafaruku, nchi hiyo inayotegemea sana utalii.

Si utalii tu, na vita dhidi ya ugaidi na uwekezaji

Kenya ni muhimu kwa utulivu wa eneo lote. Kutokana na mpaka wake mrefu pamoja na Somalia, inaangaliwa kama ngome ya mapambano dhidi ya wanamgambo wa al-Shabaab. Kenya inaweza kujikuta katika hali kama ile ya Sudan, ambayo ni nchi pekee yenye rais anayesakwa na ICC.

Mbali na kesi dhidi ya Kenyatta na Ruto, suala la dhulma katika kugawanywa ardhi ni tatizo jengine kubwa linalomkabili rais huyo mpya. Katika miezi iliyopita, mapigano yaliripuka na damu kumwagika kwa sababu ya ardhi. Ukoo wa Kenyatta unamiliki, mbali na makampuni makubwa makubwa ya kutengeneza maziwa, hoteli za kifahari, vyombo vya habari, benki na ardhi kubwa kupita kiasi.

Lakini, juu ya yote hayo, Kenyatta itabidi adhihirishe kwamba yeye ni rais wa Wakenya wote. Hofu za watu wa makabila mengine ni kubwa. Kwa wafuasi wake Kenyatta ni shujaa. Kwa wengine yeye ni kitambulisho cha wasomi waliobobea kwa rushwa nchini humo.

Hivi sasa kwa mara nyengine tena kauli mbiu inabidi iwe Harambee - kama ilivyohanikiza miaka 50 iliyopita wakati nchi hiyo ilipojipatia uhuru wake kutoka Uingereza.

Mwandishi: Andrea Schmidt
Tafsiri: Hamidou Oummilkheir
Mhariri: Mohammed Khelef