1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Ushindi wenye utata

Andrea Schmidt29 Oktoba 2015

Uchaguzi Tanzania ulifanyika kwa amani. Lakini tume ya uchaguzi kisiwani Zanzibar ilibatilisha matokeo. Katika maoni yake Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili, Andrea Schmidt, anasema Tanzania imo katika njia ya hatari.

https://p.dw.com/p/1GwTI
Watanzania wapiga kura
Watanzania wapiga kuraPicha: DW/P. Kwigize

Kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania umefanyika uchaguzi ambapo wagombea John Magufuli wa CCM na Edward Lowasa wa upinzani walienda takriban sambabamba na hivyo kuwepo uwezekano mkubwa wa chama cha CCM kuondolewa madarakani baada ya kutawala kwa muda wa zaidi ya nusu karne.

Uchaguzi waTanzania ungeliweza kuwa mfano barani Afrika. Baada ya mabadiliko ya mamlaka yaliyofanyika kwa amani nchini Nigeria, Tanzania ingeliweza kuwa mfano mwingine wa kutia moyo wa maendeleo ya demokrasia barani Afrika.

Schmidt Andrea Kommentarbild App
Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili Schmidt Andrea

Lakini siku moja tu baada ya watu kupiga kura ,umoja wa vyama vya wapinzani, UKAWA ulitoa madai kwamba chama cha mapinduzi kilifanya udanganyifu mkubwa wa kura! Ukawa inataka kura zihesabiwe tena.

Hali nchini Tanzania ni ya wasi wasi mkubwa. Kila upande umesimama kidete. Hakuna anaekubali kushindwa. Kila upande unadai kuwa mshindi.

Swali sasa ni iwapo kura zitahesabiwa tena au chama tawala, CCM kitasonga mbele kwa nguvu zote na hesabu za sasa, na kujitangaza mshindi wa uchaguzi? Na ikiwa kweli kura zitahesabiwa tena nani atahakikisha kwamba kazi hiyo itafanyika kwa njia ya uwazi ili kila upande uweze kuridhika na matokeo?

Mvutano kisiwani Zanzibar

Hali ya kisiwani Zanzibar pia ni ya mvutano.Wagombea wakuu wa uchaguzi ,Rais Ali Mohamed Shein wa Chama cha Mapinduzi na Seif Sharif Hamad wa chama cha upinzani CUF, pia walienda sambamba.

Chama hicho kikuu cha upinzani,kisiwani Zanzibar ,tayari kilishalalamika juu ya udanganyifu mkubwa katika chaguzi za miaka ya 1995, 2000 na 2005. Chama hicho kilihisi kuwa kiliibiwa ushindi.

Wakati watu walipojiandikisha kupiga kura palikuwapo na vitisho na wale wanaounga mkono upinzani walishambuliwa. Hata hivo kwa jumla katika siku ya kupiga kura mambo yalikuwa shwari kisiwani Zanzibar.

Matokeo yabatilishwa

Baada ya Kiongozi wa upinzani Seif Sharif Hamad Jumatatu kujitangaza mshindi, na kuitaka tume ya uchaguzi safari hii iutambue ushindi wake, wanajeshi na polisi waliizingira tume ya uchaguzi. Waangalizi wa kimataifa pia walifungiwa ndani ya ofisi ya tume hiyo kwa masaa kadhaa.

Yumkini hatua yake ya kujitangaza mapema kuwa mshindi ilimrudisha nyuma .Kazi ya kuhesbu kura ilisuasua na tume ya uchaguzi ilitangaza kwamba palikuwapo na udanganyifu mkubwa wa kura uliofanywa na wapinzani na kwamba Sharif alijitangaza mapema kuwa mshindi. Kwa hivyo matokeo yamebatilishwa na kwamba uchaguzi mwingine ufanyike mnamo muda wa siku 90.

Lakini chama cha upinzani kinaupinga uamuzi huo na kimesimama kidete na kushikilia kuwa ni mshindi. Lakini hata ikiwa uchaguzi utafanyika tena baada ya siku 90, linakuja swali:jee vipi tume ya uchaguzi itaweza kurejesha imani, na vipi itahakikisha kwamba udanganyifu haufanyiki?

Katika mazingira hayo ya mvutano jambo la kipaumbele ni kudumisha amani. Jumuia ya kimataifa inao wajibu wa kuzishinikiza pande zote ilikuepusha mambo kuwa mabaya zaidi. Hayo hayapaswi kutokea katika nchi kama Tanzania ambayo kwa miaka yote imekuwa nanga ya utulivu na pepo ya amani.

Hali haitakuwa ya hatari kwa Tanzania na watu wake tu bali sambamba na migogoro ya Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kanda yote inaweza kuyumbishwa

Mwandishi: Andrea Schmidt

Mfasiri: Mtullya Abdu.