1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Wasiwasi watanda Kenya

Abdu Said Mtullya8 Machi 2013

Wasiwasi na hisia za mtamauko zinazidi kuwa kubwa miongoni mwa wapigakura nchini Kenya wakati wagombea wakuu, Uhuru Kenyatta na Raila Odinga, wakizozana juu ya kura zilizoharibika.

https://p.dw.com/p/17tNM
Schmidt, Andrea Multimediadirektion REGIONEN, Afrika - Kisuaheli DW2_8372. Foto DW/Per Henriksen 18.10.2012
Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili Andrea SchmidtPicha: DW

Wagombea wote waliapa kabla ya kuifanyika kwa uchaguzi kwamba watayatambua matokeo. Lakini sasa wote wameanza kupiga kelele.

Ishara zimesimama katika mkondo wa dhoruba, amani ambayo tayari ipo kwenye hatihati katika nchi hiyo yenye makabila mengi, imo katika hatari ya kutenguka: hali hiyo imesababishwa na mushkeli katika mitambo ya kupigia kura na kuchelewa kuhesabiwa kwa kura.

Miungano yote miwili ya wagombea wakuu, CORD unaoongozwa na Raila Odinga na Jubilee unaongozwa na Uhuru Kenyatta, inazungumzia juu ya kutokea udanganyifu wa kura.

Raila Odinga, ambaye sasa ana umri wa miaka 68 na anayehisi kuwa aliibiwa ushindi katika uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2007, anahofia kutokea tena kwa mizengwe kutokana na kusita kuhesabiwa kwa kura.

Miaka mitano iliyopita zilitokea ghasia nchini Kenya zilizosababisha vifo vya watu 1,200 na maelfu ya wakimbizi wa ndani - jeraha ambalo limeendelea kukaa katika roho za Wakenya hadi leo.

Utata ulipo

Muungano wa Odinga umesema unataka zoezi lote la kuhesabu kura lisimamishwe.

Kulingana na utaratibu wa uchaguzi wa rais nchini Kenya, mshindi anapaswa kupata wingi wa zaidi ya asilimia 50 ya kura na pia anapaswa ashinde katika kaunti 25 kati ya 47. Idadi kubwa ya kura batili imetokana na matatizo ya kompyuta. Vikaratasi vya kura na visanduku viliandikwa kwa rangi.

Hata hivyo, kura 400,000 ziliingia katika visanduku ambavyo havikulengwa na wapiga kura. Endapo kura hizo zitatiwa katika hesabu, uzito wake kwenye mzani utaubonyeza upande wa Kenyatta na kuwa na maana ya upande huo kushindwa.

Kwa Kenyatta na mgombea mwenza, William Ruto, mengi yamewajaa vifuani. Wote wanakabiliwa na mashtaka ya uhalifu dhidi ya ubinadamu kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu mjini The Hague.

Waangalizi wasifu upigaji kura, lakini matokeo je?

Waangalizi wa uchaguzi zaidi ya 23,000, ikiwa pamoja na 2,600 kutoka nje wametoa kauli nzuri, yaani za matumaini juu ya uchaguzi, na wamesema kwamba hawakubaini njama zozote.

Ndiyo kusema pande zote zinapaswa mara moja kuacha kuonyoosheana vidole kabla ya kutolewa kwa matokeo ya kweli. Wagombea wote pia wanapaswa kutoa wito wa amani kwa watu wao ambao sasa wana joto matumboni mwao ili kuepusha umwagikaji wa damu mithili ya miaka mitano iliyopita.

Ikiwa yatatokea machafuko nchini Kenya, yanaweza kuenea kote na kusababisha madhara makubwa katika uchumi unaotegemea sana utalii. Tayari nchi jirani: Uganda, Rwanda na Burundi zina wasiwasi wa kuathirika tena na vurumai zinazoweza kutokea nchini Kenya. Pamoja na hayo yote, Kenya ndiyo injini ya uchumi katika Afrika Mashariki.

Wapiga kura nchini Kenya waliofikia asilimia 70 na kumiminika kwenye vituo vya kupigia kura baada ya kusimama katika kilomita za foleni waliitumia haki yao ya kidemokrasia, japo hadi leo bado wana jeraha la rohoni kufuatia uchaguzi wa mwaka wa 2007.

Watu hao sasa wanayo haki ya kuyaona matokeo sahihi na pia wanayo haki ya kuona kwamba wanasiasa wao wanayakubali matokeo hayo.

Jumuiya ya kimataifa pia inapaswa kutimiza dhima yake haraka kwa kuimarisha shinikizo kwa mahasimu wakuu ili kuepusha kushtadi kwa hali mbaya.

Mwandishi: Schmidt Andrea/DW Kiswahili
Tafsiri: Mtullya Abdu
Mhariri: Mohammed Khelef