1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya Iran na Kenya

Abdu Said Mtullya26 Septemba 2013

Wahariri wanazungumzia juu ya uhusiano baina ya Iran na nchi za magharibi na hasa na Marekani.Wahariri hao pia wanayatupia macho matukio ya nchini Kenya

https://p.dw.com/p/19oqu
Rais wa Iran Hassan Rohani
Rais wa Iran Hassan RohaniPicha: Isna

Juu ya juhudi za kidiplomasia za Iran katika medani ya kimataifa gazeti la "Nordbayerischer Kurier" linasema Iran sasa inatoa ishara ya siasa ya maridhiano Lakini gazeti hilo linasema inapasa kuwa na tahadhari.

Hata hivyo mhariri wa gazeti la "Nordbayerischer Kurier" anasema ishara inayotolewa na Iran inachangia katika kuleta matumaini katika eneo la migogoro la Mashariki ya Kati.

Mhariri wa gazeti la "Döbelner Anzeiger " anasema Iran na Marekani ni nchi mbili zinazohitajiana na anafafanua kwa kueleza kwamba hotuba mbili za Iran kwenye Baraza kuu la Umoja wa Mataifa hazitoshi kujenga msingi wa imani.Lakini mpaka sasa hapajawahi kutokea fursa kubwa .

Tofauti na Rais wa hapo awali, Rais mpya wa Iran hakutema sumu dhidi ya Marekani na Israel. Na kwa upande wake Rais wa Marekani anataka kujaribu njia ya kidiplomasia ili kuutatua mzozo wa nyuklia na Iran. Mambo mawili yaliyojificha katika muktadha wa kauli za maridhiano. Iran na Marekani zinahitajiana.

Iran inaitaka Marekani itoe ishara kwa nchi nyingine za magharibi juu ya kuondolewa kwa vikwazo dhidi yake. Na kwa upande wake Marekani inaihitaji Iran katika kuutatua mgogoro wa nchini Syria.

Magharibi itoe ishara:

Mhariri wa gazeti la "Hannoversche Allgemeine" anazitaka nchi za magharibi nazo zitoe ishara ya wazi kwa Iran. Anaeleza, kwamba wakati sasa umefika kwa nchi za magharibi kuwa na sera mpya juu ya Iran. Mhariri huyo anashaurikuwa nchi za magharibi nazo zinapaswa kutoa chochote kwa Iran. Kwa mfano kwa kuzifungulia fedha za Iran, ili zitumike kwa ajili ya kununulia dawa kwa wagonjwa nchini Iran.Huo ungelikuwa mchango wa nchi za magharibi katika juhudi za kibinadamu ili kuidumisha kasi inayotokana na kuchaguliwa kwa Rais mpya wa Iran

Gazeti la "Saarbrücker" linasema utayarifu wa Rais Obama wa kukutana na Rais wa Iran ni jambo la kulitilia maanani,baada ya miaka 30 ya mvutano mkubwa baina ya Marekani na Iran.

Jumuiya ya kimataifa ipambane na ugaidi kwa dhati

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linazungumzia matukio ya nchini Kenya.Gazeti hilo linasema mashambulio ya kigaidi nchini Kenya yamefungua ukarasa mpya wa ugaidi. Mashambulio hayo yanathibitisha kwamba jumuiya ya kimataifa bado haijachukua hatua za kutosha ili kuikabili vurumai ndani ya Somalia.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman