1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya Korea ya Kaskazini,

Abdu Said Mtullya13 Februari 2013

Wahariri wa magazeti wanazungumzia juu ya jaribio la nyuklia la Korea ya Kaskazini.Lakini pia wanatoa maoni juu ya mtu atakaemfuatia Papa Benedikt wa 16

https://p.dw.com/p/17dLu
Majaribio ya silaha za nuklia, Korea ya Kaskazini
Majaribio ya silaha za nyuklia, Korea ya KaskaziniPicha: picture-alliance/dpa

Gazeti la "Landeszeitung" linasema jaribio la nyuklia ,lililofanywa na Korea ya Kaskazini mapema wiki hii limeyaondoa matumaini yote kwamba kiongozi wa sasa wa nchi hiyo Kim Jong Un angelikuwa na tabia tofauti na baba yake.

Kim Jong Un pia anatumia turufu ya silaha za nyuklia ,kila panapotelewa kitisho cha vikwazo dhidi ya nchi yake Korea ya Kaskazini.Mwisho wa mchezo huo wa hatari haujulikani.

Gazeti la Märkische Allgemeine" linasema jumuiya ya kimataifa haina njia thabiti ya kuibana Korea ya Kaskazini.Hata hivyo ni lazima kuiwekea nchi hiyo vikwazo.

Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa ni lazima jumuiya ya kimataifa iweke vikwazo ili kuionyesha Korea ya Kaskazini kwamba,vitendo vya uchokozi vinaweza kuwa na gharama kubwa.Wakati huo huo nchi za magharibi zitapaswa kuieleza Korea ya Kaskazini wazi kabisa kwamba ikiwa itaacha kufanya majaribio ya silaha za nyuklia, malipo yake yatakuwa msaada mkubwa wa kiuchumi,na kuthaminiwa kisiasa duniani.

Mhariri wa gazeti la"Badische" anahoji kwamba njia pekee ya kuweza kuibana Korea ya Kaskazini ni kwa Marekani na China kusimama pamoja,badala ya kuvutana. Mhariri wa gazeti hilo anafafanua kwa kusema, kutokana na hofu ya kushtadi kwa mvutano,jirani wa Korea ya Kaskazini wanakubali kufanya mazungumzo na kujaribu kuipa nchi hiyo misaada ili kuituliza. Korea ya Kaskazini inayatambua hayo vizuri sana, na ndiyo sababu inaendelea na majaribio ya silaha za nyuklia.Kwa hivyo,ili kuondokana na kizungumkuti hicho,itazipasa Marekani na China zishirikiane,badala ya kudonyoana!

Mhariri wa gazeti la "Mitteldeutsche"anasema Korea ya Kaskazini inatumia majaribio ya silaha za nyuklia kama shinikizo la kisiasa.Ni Urusi na China zinazoweza kusaidia kuiweka sawa nchi hiyo.

Jee nani atakuwa mrithi wa Papa Benedikt wa16? Kwa sasa hakuna anayejua. Lakini mhariri wa gazeti la "Cellesche Zeitung" ana maoni yafuatayo.

"Haidhuru ni nani atamfuatia Papa Benedikt wa16,hakuna atakaemwonea kijicho" Gazeti linaeleza kwamba mtu huyo atakuwa na kazi ya kuzileta pamoja pande mbalimbali za kanisa katoliki,atapaswa kuwasiliana na wawakilishi wa dini nyingine na pia atakabiliwa na changamoto ya kuurejesha wajihi halisi wa Kanisa Katoliki.

Majukukmu hayo yatakuwa mazito pia kwa Baba Mtakatifu ataekuwa na umri wa chini ya miaka 85.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deustche Zeitungen.

Mhariri:Josephat Charo