1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yuan yapunguzwa thamani

Admin.WagnerD13 Agosti 2015

Wahariri wanatoa maoni juu ya hatua iliyochukuliwa na China ya kuipunguza thamani ya sarafu yake ya Yuan.Na pia wanatoa maoni juu ya sera mpya ya Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras

https://p.dw.com/p/1GF0K
China yashusha thamani ya sarafu yake Yuan
China yashusha thamani ya sarafu yake YuanPicha: Reuters/J. Lee

Gazeti la "Westfalenpost" linaitilia maanani hatua iliyochukuliwa na China ya kuipunguza thamani ya sarafu yake ya Yuan. Mhariri wa gazeti hilo anasema wakati ambapo uchumi wa China ulikuwa unavuka ustawi wa asilimia 10 na hivyo kuzinufaisha nchi za Ulaya vile vile, umeshapita. Lakini mhariri wa gazeti la "Westfalenpost" anasema hayo siyo maafa.

Mhariri huyo anatilia maanani, kwamba kwa nchi yoyote kuipunguza thamani ya sarafu yake ni jambo la kawaida, ila tu ,anasema anatumai ,China haikuchukua hatua hiyo kwa lengo la kuweza kuuza zaidi katika nchi za nje.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linasema kuanguka thamani ya hisa, nchini Ujerumani kutokana na kupungua thamani ya Yuan, ni ishara ya tahadhari.

Mhariri huyo anaeleza kuwa kupunguzwa thamani ya sarafu ya China, mara mbili kulitosha kusababisha mitikisiko kwenye masoko ya hisa duniani. Na ghafla Ulaya imejikuta,inakwanyuka kutoka kwenye usonge wa sarafu yake ya Euro na kubainisha kuwa siyo kila jambo duniani linategemea na hali ya mgogoro wa Ugiriki. Mhariri anasema anatumai kwamba kupunguzwa thamani ya sarafu ya Yuan siyo mwanzo wa vita vya kisarafu duniani.

Ustawi wa uchumi ni muhimu zaidi
Mhariri wa gazeti la "Südwest Presse" anaelezea matumani kwamba China itafanya kila linalopasa ili kuepusha mshuko wa uchumi.Mhariri huyo anasema ni jambo moja tu linalowaleta pamoja viongozi wa serikali ya China; nalo ni ustawi thabiti wa uchumi.

Gazeti la "Süddeutsche" linasema Waziri Mkuu wa Ugiriki Tsipras amechukua hatua sahihi. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa Waziri Mkuu Tsipras ameirudisha Ugiriki katika udhibiti wake.Hatua ya kwanza muhimu aliyoichukua ni kuwaengua wapinzani wa sera yake mpya.

Mhariri huyo anatilia maanani kwamba Tsipras amewaondoa watu hao kutoka kwenye serikali yake. Tsipras amefanya kazi kubwa ili kuweza kufikia hatua ya kukubaliana na wakopeshaji wa kimataifa .

Gazeti linasema ni wazi kwamba hali ngumu itakuja nchini Ugiriki, lakini sera yake mpya Tsipras italeta haki.Matajiri watatozwa kodi na wale waliokuwa wanakwepa kulipa kodi hawataachiwa upenyo.

Mhariri wa "Süddeutsche" anasema jambo muhimu zaidi ni kwamba ,kutokana na sera mpya ya Waziri Mkuu Tsipras, Ugiriki itaendelea kuwamo katika sarafu ya Euro na hivyo kuendelea kuwamo katika Umoja wa Ulaya.

.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Iddi Ssessanga