1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

....

Abdu Said Mtullya4 Februari 2015

Wahariri wa magazeti wanazungumzia juu ya mgogoro wa madeni makubwa ya Ugiriki na juu ya uamuzi uliotolewa na mahakama ya kimataifa kuhusu mashtaka ya mauaji ya kimbari yaliyowasilishwa na Kroatia na Serbia

https://p.dw.com/p/1EVLg
Waziri wa fedha wa Ugiriki Varoufakis ziarani mjini Frankfurt
Waziri wa fedha wa Ugiriki Varoufakis ziarani mjini FrankfurtPicha: Reuters/K. Pfaffenbach

Juu ya Ugiriki gazeti la "Darmstädter Echo" linasema mawazo yaliyotolewa na Waziri wa fedha wa nchi hiyo juu ya kuubadilisha utaratibu wa malipo wa deni la nchi yake yanastahili kutiliwa maanani. Mhariri huyo anaeleza kwamba kutokana na mawazo hayo itawezekana kwa Umoja wa Ulaya kuisikiliza serikali ya Ugiriki.


Mhariri wa gazeti la "Neue Osnabrücker" pia anaitilia maanani kauli ya Waziri wa fedha wa Ugiriki juu ya deni la nchi yake. Mhariri huyo anaafiki kwamba kauli ya Waziri huyo ni ya busara na anafafanua kwamba Wagiriki walijua walichokuwa wanakifanya walipoichagua serikali yao.

Ugiriki yaubadilisha msimamo

Serikali hiyo ilianza kuyatekeleza iliyoyaahidi ,katika kampeni za uchaguzi.Na kwa kufanya hivyo ilitarajia kuona tufani likitifuka katika Ukanda wa sarafu ya Euro.Lakini baada ya kutambua kwamba mambo yameendelea kuwa maenge ,viongozi wa serikali ya Ugiriki wameanza kuubadilisha mtazamo wao wa hapo awali.Badala ya kutaka deni lao lipunguzwe, sasa wanaomba utaratibu wa malipo ubadilishwe.

Mazungumzo ndiyo jawabu nchini Ukraine

Gazeti la "Braunschweiger" linasisitiza katika maoni yake kwamba mgogoro wa Ukraine unaweza kutatuliwa kwa njia moja tu:nayo ni ile ya kufanya mazungumzo. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kwamba katika mapambano yanayoendelea mashariki mwa Ukarine, hakuna tena tofauti kati ya usiku na mchana. Hata hivyo tofauti inaweza kuletwa ikiwa pande zinazohusika na mgogoro zitafanya juhudi ili kuepusha vifo vya raia. Lakini ili lengo hilo lifikiwe mchango wa Urusi unahitajika sana.

Hayakuwa mauaji ya kimbari
Mahakama ya Kimataifa ya mjini The Hague iliamua hapo jana kwamba hakuna upande uliofanya mauaji halaiki wakati wa vita vya miaka ya1990 baina ya Kroatia na Serbia.

Gazeti la "Die Rheinpfalz" linasema juu ya hukumu hiyo kwamba serikali za Kroatia na Serbia zimefurahi juu ya uamuzi huo kwani umeziepusha serikali za nchi hizo na mzigo wa kulipa fidia. Serikali hizo zingelilipa mamilioni ya fedha.

Sasa kilichobakia ni kuwashughulikia watu ambao bado wanatafutwa mpaka leo na vile vile inapasa kulishughulikia suala la mali zilizoporwa na kila upande. Lakini hayo yanaweza kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo.


Mwandishi:Mtullya Abdu.Deustche Zeitungen.

Mhariri: Josephat Charo