1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkakati wa Marekani

Admin.WagnerD26 Mei 2015

Wahariri wanatoa maoni ya mkakati wa Marekani dhidi ya wapiganaji wanaoitwa dola la Kiislamu nchini Iraq. Pia wanazungumzia juu ya mgogoro wa mashariki mwa Ukraine

https://p.dw.com/p/1FWW8
Majeshi ya Iraq yaanza mashambulio dhidi ya IS
Majeshi ya Iraq yaanza mashambulio dhidi ya ISPicha: picture-alliance/AP Photo

Gazeti la "Frankfurter Rundschau" linasema mkakati wa Marekani wa kupambana na magaidi wa Daish ,Dola la Kiislamu una mapungufu.

Mhariri wa gazeti hilo inaikosoa vikali Marekani kwa mapungufu yaliyomo katika mkakati unaotumiwa na nchi zilizofungamana kijeshi dhidi ya magaidi hao.Mhariri huyo anasema tokea mwanzo kabisa ilikuwa wazi kwamba misuli ya kijeshi peke yake haitafua dafu.

Mhariri wa gazeti la "Frankfurter Rundschau" anasema jumuiya ya kimataifa imeweza kujifunza kutokana na vita vya nchini Afghanistan dhidi ya Taliban. Majeshi ya kimataifa, yaliyoongozwa na Marekani, yalianza kupata mafanikio baada ya kushirikiana na wananchi katika ujenzi wa Afghanistan,kisiasa,kiuchumi na kijamii. Mhariri wa "Frankfurter Rundschau" anasema mkakati kama huo unahitajika pia katika kupambana na Dola la kiislamu nchini Iraq.

Ni mazungumzo yatakayoutatua mgogoro wa Ukraine

Gazeti la "Nürnberger Nachrichten" linatoa maoni juu ya kipindi cha mwaka mmoja madarakani, cha Rais Petro Poroshenko nchini Ukraine, katika muktadha wa mgogoro wa mashariki mwa nchi hiyo.

Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kwamba Rais Poroshenko na Waziri wake Mkuu Yatsenyuk, wanategemea sana msaada wa nchi za magharibi. Lakini mgogoro wa mashariki mwa Ukraine unaweza kutatuliwa, kwa njia ya mazungumzo.

Rais wa Urusi,Vladimir Putin ameeleza wazi kwamba msingi wa kuleta mapatano ni kwa mfungamano wa kijeshi wa Nato kuacha kujitandaza katika nchi ambazo ni jirani wa Urusi. Bila ya hilo kufanyika, damu itaendelea kumwagika mashariki mwa Ukraine.

Katika uchaguzi wa serikali za mitaa nchini Uhispania, mwishoni mwa wiki iliyopita, chama kinachotawala, cha Waziri Mkuu, Mariano Rajoy, kilipata pigo.Kwa nini?

Mhariri wa gazeti la "Münchner Merkur" anaeleza matokeo ya uchaguzi ni ishara ya kupinga ufisadi unaofanywa na vyama vya jadi nchini Uhispania. Wananchi hawana imani tena. Sasa wanawasikiliza wanasiasa wa mrengo wa kushoto wanaoipinga sera ya kubana matumizi.

Hilo ni jambo la kutisha. Sababu ni kwamba chama cha wapinga sera ya kubana matumizi kimeingia madarakani nchini Ugiriki, na matokeo yake ni vurumai na wasi wasi juu ya mustakabal wa nchi hiyo.

Gazeti la "Südwest Presse" linazungumzia juu ya harakati za Ujerumani katika kupambana na wanaokwepa kulipa kodi.Lakini mhariri wa gazeti hilo anatilia maanani kwamba mkakati unaotumika una mapungufu.

Anasema juhudi za kuwawinda wanaokwepa kulipa kodi ni jambo sahihi ,kwani serikali ya Ujerumani inaibiwa mabilioni ya fedha. Hata hivyo bila ya benki kukubali kufichua siri za wenye akiba, juhudi za kupambana na wahalifu hao zitakuwa za mashaka.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Josephat Charo