1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya Mkataba wa Schengen

Abdu Said Mtullya27 Aprili 2011

Rais Sarkozy wa Ufaransa na Waziri Mkuu wa Italia Berlusconi wataka mageuzi ya mkataba wa Schengen. Wahariri wa magazeti watoa maoni yao

https://p.dw.com/p/114it
Waziri Mkuu wa Italia Silvio Berlusconi kushoto, na Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa kuliaPicha: picture-alliance/dpa

Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa na waziri Mkuu wa Italia Silvio Berlusconi wanataka mkataba wa Schengen ufanyiwe mageuzi.Mkataba huo uliotiwa saini na nchi 25 za Ulaya ulianzisha utaratibu wa kuacha mipaka yote wazi baina ya nchi hizo.

Mhariri wa gazeti la Volkssitimme anasema ikiwa waziri Mkuu wa Italia Berlusconi na Rais wa Ufaransa Sarkozy wanataka mkataba wa Schengen ufanyiwe mageuzi, na hasa wanapotumai kuungwa mkono na Tume ya Umoja wa Ulaya, hayo ni matokeo ya hali halisi.Kwani mpaka sasa nchi za Umoja wa Ulaya zinazopakana na mabara mengine ndizo hasa zimekuwa zinaubeba mzigo wa wakimbizi. Lakini aghalabu zimeachwa peke yao zibebe mzigo huo.Nchi nyingine kama Ujerumani zilizopo mbali na mipaka hiyo zinatoa kauli za maliwazo tu.!

Mhariri wa gazeti hilo la Volksstimme anauliza, jee hali itakuwaje ikiwa mapinduzi ya umma yatatokea nchini Morocco? Ndiyo kusema Uhispania nayo itapaswa kutangaza hali ya hatari au itapaswa kujenga ukuta?

Lakini mhariri wa gazeti la Kieler Nachrichten anaeleza kuwa ,kwa mujibu wa mkataba wa Schengen, yaani wa kuacha mipaka wazi, hakuna nchi inayoruhusiwa kuweka taratibu za udhibiti mipakani, bila ya ridhaa ya tume ya Umoja wa Ulaya. Na kuhusu Italia na Ufaransa mhariri huyo anafafanua kwamba hakuna mazingira yoyote yanayoonyesha kuwa usalama wa nchi hizo umehatarishwa. Kwa hiyo msimamo wa viongozi wa Italia na Ufaransa juu ya kutaka ,mkataba wa Schengen ufanyiwe mageuzi unathibitisha jinsi Umoja wa Ulaya ulivyokuwa lege lege katika miezi iliyopita.

Gazeti hilo linaeleza kwamba tokea nchi za Ulaya zikumbwe na mgogoro wa mabenki, kila nchi inazingtia maslahi yake ya kitaifa.Kwa hiyo Berlusconi na Sarkozy pia wanataka kunufaika kifedha kutoka kwenye mfuko wa Umoja wa Ulaya. Hali hiyo haitaleta manufaa katika siku za usoni.

Gazeti la General -Anzeiger linasema msimamo wa Italia na Ufaransa siyo mfano mzuri juu ya kuendeleza uelewano na ushirikiano miongoni mwa nchi za Umoja wa Ulaya. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa kutaka mkataba wa Schengen ufanyiwe mageuzi maana yake ni kuidhoofisha hati hiyo.Na matakwa hayo yanatolewa, pale panapotokea mfumuko mkubwa wa wakimbizi, kama waziri Mkuu wa Italia Berlusconi anavyolalamika, kana kwamba anaigiza kwenye jukwaa la tamthilia!

Lakini mhariri wa Saarbrücker anatilia maanani kwamba Berlusconi na Sarkozy ni viongozi waliobanwa katika nchi zao, na anaeleza kuwa Serikali za Ufaransa na Italia zipo chini ya mashinikizo ya vyama vya mrengo mkali wa kulia. Vinataka serikali zao zijitoe kwenye mkataba wa Schengen. Kwa hiyo,kwa kutaka mkataba huo ufanyiwe mageuzi, Berlusconi na Sarkozy wanaziwinda kura watu fulani katika nchi zao.Kwani viongozi hao wamezama mnamo migororo mikubwa!

Mwandishi/Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri/-Othman Miraj,