1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya mwaka mmoja wa serikali ya mseto.

Abdu Said Mtullya26 Oktoba 2010

Wahariri wa magazeti leo wanatoa maoni yao juu ya kutimia mwaka mmoja wa serikali ya mseto nchini Ujerumani.

https://p.dw.com/p/PoCR
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na makamu wake Guido Westerwelle.Picha: AP

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya mwaka mmoja tokea kuundwa serikali ya mseto hapa nchini na juu ya mkataba wa Umoja wa Ulaya wa kuhakikisha nidhamu katika bajeti za nchi za Umoja huo.

Naam leo unatimia mwaka mmoja tokea vyama vya CDU,FDP na CSU vilipotia saini mkataba wa serikali ya mseto. Jee serikali hiyo imefanya nini?

Mhariri wa gazeti la Lausitzer Rundschau anasema katika maadhimisho hayo hapatakuwa na mvinyo, kwa sababu hakuna la kusherehekea. Mhariri huyo anasema vyama hivyo vitatu havikuonyesha upendo baina yao na wala hakuna heshima miongoni mwao.

Kilichoonekana katika kipindi cha mwaka mmoja ni dhamira ya vyama hivyo ya kujaribu kwa namna yoyote ile kuendelea kubakia madarakani.Mhariri wa Lausitzer Rundschau anaeleza kuwa kulinganisha na matarajio yaliyokuwapo mwaka mmoja uliopita, yaliyotimizwa na serikali ya vyama hivyo, ni finyu sana.

Gazeti la Sttutgarter pia linasema kuwa serikali ya vyama vya CDU,FDP na CSU imeshindwa kujenga imani ya msingi na mpaka sasa haina jawabu juu ya suala hilo.Mhariri wa gazeti hilo anafafanua kwa kusema kuwa serikali ya mseto ya vyama hivyo vitatu imeshindwa kuhamasisha imani, siyo tu kwa sababu wenyeviti wa FDP, Westerwelle na Horst Seehofer wa CSU hawajajimuisha na serikali hiyo. Wanasiasa hao wanasababisha tofauti ndani ya serikali, kama njia ya kuendelea kuwa hai kisiasa.

Lakini wanayafanya hayo kwa madhara ya wenzao wa CDU.Wanauyumbisha mfungamano ambao tokea "hapo ati," umeshindwa kujenga imani ya pamoja.

Gazeti la Süddeutsche Zeitung linalalamika kwamba serikali ya mseto ya CDU, FDP na CSU imevunja ahadi yake. Na linasema kuwa Serikali hiyo inashawishiwa na wenye sauti kubwa-mawakala wa ushawishi. Ushuhuda ni kodi watakayotozwa wavuta sigara. Gazeti linasema hayo hayakuwamo katika kampeni za uchaguzi- yaani kupandisha kodi ya kuwabana watu wa chini tu, na kuziachia dohani za wakubwa ziendelee kutoa moshi.

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani pia wametoa maoni yao juu ya mvutano uliosababishwa na Ujerumani na Ufaransa kuhusiana na mkataba wa Umoja wa Ulaya.

Ujerumani na Ufaransa zinataka mabadiliko ya mkataba huo ili kuweza kuleta sheria kali za kuwaadhibu wanaozikiuka taratibu za kudumisha nidhamu ya bajeti na hasa wale wanaoitwa wanachama wadogo katika Umoja wa Ulaya.

Juu ya hayo,gazeti la Financial Times Deutschland linamtaka Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, azingatie misingi ya Umoja wa Ulaya badala ya kufuata misingi inayotumika ndani ya nchi.Gazeti hilo linamtaka Kansela wa Ujerumani, kwenye mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya alhamisi ijayo, ahakikishe kwamba hayatokei mabadiliko yoyote ya mkataba wa Umoja wa Ulaya.

Mwandishi: Abdu Mtullya /Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Miraiji Othman