1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

.

Abdu Said Mtullya8 Januari 2015

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanatoa maoni yao juu ya shambulio la kigaidi lililofanywa kwenye osifi za gazeti la mjini Paris.Watu 12 waliuawa katika shambulio hilo

https://p.dw.com/p/1EHXi
Jarida la tashtiti "Charlie Hebdo"lashambuliwa mjini Paris
Jarida la tashtiti "Charlie Hebdo" lashambuliwa mjini ParisPicha: Jean-Francois Monier/AFP/Getty Images

Mhariri wa gazeti la "Rhein Zeitung" anasema shambulio la kigaidi la mjini Paris ni maafa kwa pande zote zenye nia njema. Waislamu wenye itikadi kali wanaonyesha mfano potovu utakaoimarisha hisia za kuupinga Uislamu barani Ulaya kote. Na sasa Waislamu wa dhati wamo katika hali ya shinikizo.

Mhariri wa gazeti la "Freie Presse"anakubliana kabisa na maoni hayo kwa kusisitiza kwamba vyama vinavyowapinga wahamiaji barani Ulaya kote sasa vimepata sababu ya kuchochea hofu miongioni mwa wananchi.

Busara inahitajika sasa

Mhariri huyo anaeleza kuwa hata nchini Ujerumani mjadala juu ya wakimbizi na dini ya Kiislamu utaendelea kupamba moto. Hata hivyo hakuna sababu ya kuwatuhumu Waislamu wote. Katika muktadha wa kadhia ya jana ,pana haja ya kutumia busara na kupambanua baina ya wale wanaotetea tunu za ,stahamala ,demokrasia na uhuru wa kutoa maoni na wale wanaoyapiga vita maadili ya nchi za magharibi.


Mhariri wa gazeti la "Nordwest" anahofia huenda shambulio la mjini Paris likachochea mjadala juu ya uhamiaji nchini Ufaransa lakini pia nchini Ujerumani. Mhariri huyo anasema tayari makundi fulani,ya wapinga wahamiaji yanaanza kuyatumia mashambulio hayo kwa shabaha zao.

Mhariri wa gazeti la "Nordwest" anaeleza kuwa wale watu wanaojitambulisha kuwa waokozi wa Ulaya -wanaoitwa Pegida ,sasa wanahisi kuwa wapo sahihi katika msimamo wao wa kuupinga Uislamu. Ni wajibu wa wote, anasema mhariri huyo kuhakikisha kwamba watu hao hawapati ushindi.

Waislamu wengi wanapinga ugaidi

Gazeti la "Sächsische" pia linahofia kushtadi kwa hisia za chuki dhidi ya wahamiaji na Uislamu kutokana na shambulio la jana mjini Paris ,lililofanywa kwa jina la Uislamu. Hata hivyo mhariri wa gazeti hilo anatilia maanani kwamba idadi kubwa ya Waislamu wanapinga ugaidi.

Na mhariri wa gazeti la "Flensburger Tageblatt" anawaambia magaidi waliofanya shambulio hapo jana, kwamba uhuru wa kutoa maoni ni muhimu kwa wato wote. Anasema kutokana na kujaa chuki katika nyoyo zao magaidi wanapuuza nguvu ya maneno na picha. Ni kutokana na uhuru wa kutoa maoni katika vyombo vya habari kwamba imewezekana kuwaangusha madikteta na kuwaumbua wale wanaotumia itikadi kuwahadaa watu. Magaidi waliofanya shambulio mjini Paris hawakuweza kuuvumilia ukali wa uhuru wa kutoa maoni katika vyombo vya habari.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Iddi Ssessanga