1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya Syria na Ukraine

Abdu Said Mtullya23 Aprili 2014

Wahariri wanatoa maoni juu ya uchaguzi wa Rais nchini Syria, hali ya nchini Ukraine na kurudi kwa timu ya FC Cologne kule ambako inastahili kuwapo, katika Ligi Kuu ya Ujerumani

https://p.dw.com/p/1Bm2W
Rais wa Syria Bashar al-Assad
Rais wa Syria Bashar al-AssadPicha: Reuters

Gazeti la "Märkische Oderzeitung" linatoa maoni juu ya uchaguzi wa Rais nchini Syria. Serikali ya nchi hiyo imetangaza kwamba uchaguzi huo utafanyika tarehe tatu ya mwezi Juni.

Mhariri wa gazeti la "Märkische Oderzeitung" anasema kubabaika kwa nchi za magharibi katika kuushughulikia mgogoro wa nchini Syria ,kutamwezesha Rais wa sasa Bashar al-Assad aibuke kidedea kama kiongozi mpya kwa kuchaguliwa kwa zaidi ya asilimia 90 ya kura.Mhariri wa gazeti hilo anasema ikiwa jumuiya ya kimataifa inadhamiria kuleta utulivu nchini Syria, hakuna njia nyingine ila kuzungumza na Rais Assad. Mhariri huyo anasema Bashar al- Assad siye mfano wa kiongozi wa kidemokrasia, yeye ni dikteta.Hata hivyo yeye siye dikteta wa pekee duniani. Lakini siasa ya busara lazima itumike ili kuwaletea maendeleo watu wa Syria.

Acheni kujiingiza Ukraine

Gazeti la "Neue Osnabrücker" linauzungumzia mgogoro wa nchini Ukraine katika muktadha wa makubaliano yaliyofikiwa mjini Geneva juu ya kuutatua mgogoro huo

.Mhariri wa gazeti hilo anahoji kwamba ni rahisi kusema kuliko kutenda. Imethibiti kuwa vigumu kuyatekeleza yale yaliyokubaliwa mjini Geneva juu ya kuituliza hali ya nchini Ukraine.

Hakuna hali ya kuaminiana miongoni mwa pande zote zinazohusika na mgogoro wa nchi hiyo,zile za kitaifa na za kimataifa.Lakini ni wazi kwamba Ukraine inahitaji kupewa nafasi ya kuufungua ukurasa mpya.Na ili hatua hiyo iweze kufikiwa ni lazima makundi ya wenye silaha yanyang'anywe silaha hizo. Lakini pia ujiingizaji wote kutoka nje ukomeshwe. Amani haina maana tu ya kutosikika milio ya mizinga!

FC Köln yarudisha hadhi ya daraja la kwanza


Timu maarufu ya kandanda ya mji wa Cologne, FC Köln imerejea tena katika Ligi kuu ya Ujerumani baada ya kuichapa timu ya VFL Bochum mabao matatu kwa moja. Ilikuwa furaha iliyoje kwa FC Köln kurejea kule inakostahiki kuwapo-katika Bundesliga.

Juu ya ushindi huo gazeti la "Kölner Stadt-Anziger linasema katika maoni yake kwamba timu ya FC Köln haikuwa inacheza kwa kusisimua sana lakini imeonyesha ukakamavu mbele ya timu nyingine.

Kilichotokea kinawafiki na hali ya miezi iliyopita. Kuishinda timu ya Bochum ni kilele cha muda tu cha juhudi za kulifikia lengo la kupanda daraja. Mwaka jana,bila ya kocha na ikiwa na mifuko mitupu, haikuoenekana kana kwamba timu hiyo ingelipanda daraja.Timu ya FC Köln imeyafanya mengi sahihi kati ya mwaka wa 2013 na 2014. Timu hiyo imerejea inapostahili kuwapo. Hongera !

Mwandishi:Mtullya Abdu./Deutsche Zeitungen

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman