1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri na ABDU MTULLYA

5 Februari 2007

Katika maoni yao,wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya ziara ya Kansela Merkel katika mashariki ya kati na juu ya ulinzi wa hali ya hewa.

https://p.dw.com/p/CHTo

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani anafanya ziara ya siku nne katika mashariki ya kati. Lengo la ziara hiyo ni kufufua mchakato wa kuleta amani katika eneo hilo.

Akizungumzia juu ya ziara hiyo mhariri wa gazeti la GENERAL-ANZEIGER la mjini Bonn anasema kuwa baada ya muda mrefu wa ukimya wanasiasa sasa wanazungumzia tena juu ya upenyo wa fursa ya kuleta amani katika mashariki ya kati .

Lakini anasema mhariri huyo wanasiasa hao wanazungumzia juu ya suala hilo wakati moto unawaka katika eneo la wapalestina.

Mhariri anatilia maanani kwamba wanasiasa hao wanaweza kuutafakari mgogoro baina ya wapalestina na waisraeli kadri wapendavyo, lakini suluhisho limo katika mikono ya wahusika wenyewe yaani wapalestina na waisraeli.

Naye mhariri wa gazeti la KÖLNISCHE RUNDSHAU anasema katika maoni yake kuwa rais Hosni Mubarak wa Misri amekigusa kitovu cha mgogoro huo kwa kusema kuwa mzozo wa mashariki ya kati una nyakati zake . Muda huo siyo wa mwezi mmoja ama mwaka mmoja. Mhariri anasema, pamoja na juhudi zote za dhati za Kansela Angela Merkel, kwa sasa haitawezekana kufikia suluhisho lolote. Kwa jinsi hali ilivyo sasa, jitihada hizo zitashindikana.

Katika kuzungumzia mgogoro wa mashariki ya kati mhariri wa gazeti la OSTSEE-ZEITUNG anamshauri bibi Angela Merkel awe na sifa za mashujaa wa kale. Mhariri anamtaka Kansela huyo awe na ubavu wa Hercules na uvumilivu wa Sisyphus aliepandisha jiwe mlimani kwa kulivingirisha. Mhariri huyo anatilia maanani kuwa mchakato wa kuleta amani katika mashariki ya kati ni mlolongo kizungumkuti.

Wahariri wengine , katika maoni yao wanaonya dhidi ya kuweka matumaini ya juu kuhusu juhudi hizo. Kwa mfano gazeti la ABENDZEITUNG linasema kuwa japo bibi Merkel anaweza kutumia sifa nzuri ya Ujerumani katika eneo hilo na hasa kutokana na msimamo wa Kansela aliemtangulia katika kupinga vita vya Irak, yeye mwenyewe hana ushauri mpya.

Mhariri wa gazeti hilo anasema kuwa bibi Merkel akiwa mwanyekiti wa sasa wa baraza la tume ya Umoja wa Ulaya anafanya bidii ya kuepusha makosa,lakini mtazamo huo hautoshi kwa mwanasiasa mwenye malengo ya juu.

Lakini mhariri wa gazeti la THÜRINGER ALLGEMEINE anampa moyo bibi Merkel kwa kusema kwamba japo ndoano yake haitavua kitu kwa sasa,uamuzi aliofanya juu ya kujaribu kusuluhisha katika mashariki ya kati ni sahihi kabisa, japo kabla yake wanasiasa wengine wenye uzito wa juu walishindwa kufikia shabaha zao.

Katika maoni yao wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo pia wanazungumzia juu ya suala la ulinzi wa hali ya hewa hasa kutokana na Umoja wa Ulaya kuitaka Ujerumani iwe mfano katika kuongoza juhudi za kulinda mazingira.

Mhariri wa gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU anaitaka serikali ya Ujerumani iwe na mkakati mujarabu katika juhudi hizo.

Anakumbusha kuwa Ujerumani ilikuwa na muda wa mwaka mzima kujitayarisha juu ya mambo mawili kuhusiana na suala la ulinzi wa hali ya hewa : kwanza uenyekiti wa Umoja wa Ulaya ,na pili ripoti ya kutisha iliyotolewa wiki jana na wataalamu wa Umoja wa Mataifa juu ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Lakini , anasema mhariri huyo, katika mambo hayo mawili serikali ya Ujerumani imefeli.

Mhariri huyo anaitaka serikali hiyo ijiulize iwapo miito tu ,na kiasi kidogo cha fedha inachotoa kwa ajili ya utafiti wa hali ya hewa kinatosha?

Naye mhariri wa gazeti la mjini Berlin TAGESZEITUNG anasema kuwa wanasiasa wanakubaliana na haja ya kulinda mazingira lakini hawataki uchumi wa nchi zao uathirike na ulinzi huo. Gazeti linaeleza kuwa undumakuwili huo unaweza kukomeshwa ikiwa mikataba ya kimataifa itaziwajibisha serikali bila ya kujali ni nani aliyetoa fedha kufadhili kampeni cha uchaguzi za wanasiasa hao.

Mhariri wa gazeti la STUTTGARTER ZEITUNG anasema kuwa haitoshi kwa Kansela Merkel kutoa ushauri juu ya kijihadhari na pedeli ili kupunguza matumizi ya petroli. Kinachotakiwa anashauri mhariri huyo ni mkakati kamambe juu ya kulinda mazingira na haliya hewa kwa jumla.