1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri pia juu ya uchumi wa Ujerumani

Abdu Said Mtullya14 Novemba 2013

Wahariri wanazungumzia juu ya uchumi wa Ujerumani,mgogoro wa Mashariki ya kati na juu ya kesi inayomkabili aliekuwa Rais wa Ujerumani Christian Wulff.

https://p.dw.com/p/1AHQt
Aliekuwa Rais wa Ujerumani Christian Wulff
Aliekuwa Rais wa Ujerumani Christian WulffPicha: picture-alliance/dpa

Gazeti la "Stuttgarter Nachrichten" linazijibu lawama na Umoja wa Ulaya juu ya uchumi wa Ujerumani. Umoja huo unalalamika kwamba Ujerumani inauza bidhaa nje, zaidi kuliko inavyoagiza .Umoja wa Ulaya unahoji kwamba hali hiyo inaweza kuziathiri kanuni za ushindani wa kibishara.

Juu ya malalamiko hayo mhariri wa gazeti la hilo anakiri kwamba, ziada katika biashara ya nje ya Ujerumani maana yake ni nakisi kwa nchi nyingine.Lakini mhariri huyo anasema ziada hiyo haitokani na njama zozote.

Naye mhariri wa gazeti la "Braunschweiger" anasema Halmashauri ya Umoja wa Ulaya inapaswa kuviangalia vigezo vilivyoleta mafanikio ya uchumi nchini Ujerumani. Mhariri huyo anakumbusha kwamba nchi nyingine zinapinga kuleta mageuzi ya kiuchumi.

Ujenzi wa makaazi ya walowezi wa kiyahudi

Gazeti la "Säschsiche" linatoa maoni juu ya suala la ujenzi wa makaazi ya walowezi wa kiyahudi katika maeneo ya Wapalestina.Linasema sera ya Israel juu ya ujenzi wa makaazi ya walowezi wa kiyahudi ndicho kipimo cha kuonyesha iwapo nchi hiyo inayo dhamira ya kuutatua mgogoro wa Mashariki ya Kati. Kwani hata mshirika wake mkuu,Marekani ,anaizingatia sera hiyo ya Israel kuwa ni mzizi wa matatizo.

Kujenga makaazi ya walowezi katika maeneo ya Wapalestina yanayokaliwa ni kukiuka sheria za kimataifa. Na hicho ni kizingiti kirefu katika kuleta uelewano na Wapalestina.Na swali la kuuliza ni vipi Wapalestina wanaweza kukubali kuwepo kwa makaazi ya walowezi katika nchi yao inayopaswa kuwa huru?

Gazeti la "Eisennacher Presse" linatoa maoni juu ya msimamo wa Israel kuhusu mazungumzo baina ya Iran na Marekani na pande nyingine, juu ya mpango wa nyuklia wa Iran. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba kwamba mgogoro wa kidiplomasia kuhusiana na Marekani ulipamba moto kiasi kwamba, msimamo wa Israel juu ya mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran haukuwa na dhima yoyote tena.Tahadhari zilizotolewa na wizara ya mambo ya nje ya Marekani kwa Israel zimethibiti kuwa na athari.

Kesi ya Christian Wulff

Kesi ya aliekuwa Rais wa Ujerumani Christian Wulff inaanza leo hapa nchini. Anakabiliwa na madai ya rushwa. Juu ya kesi hiyo mhariri wa gazeti la "Thuringische Landeszeitung" anasema kila mwananchi anapaswa kuwa sawa mbele ya sheria pia wanasiasa. Na gazeti la "Mannheimer linasema Wulff hakuwa Rais mzuri na yumkini yeye mwenyewe alitambua. Lakini sawa na mtu mwengine yeyote yeye pia anastahili kufanyiwa kesi ya haki.

Mwandishi: Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Mohammed Khelef