1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magaeti ya Ujerumani

Nyiro Charo, Josephat30 Juni 2008

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo hii katika maoni yao wanazungumzia fainali ya kombe la Ulaya na kuapishwa kwa rais Robert Mugabe wa Zimbabwe kuiongoza nchi hiyo kwa miaka mingine mitano.

https://p.dw.com/p/ETGU

Tunaanza na kushindwa kwa Ujerumani na Uhispania katika fainali ya kombe la kandanda barani Ulaya. Gazeti la Neue Osnabrücker Zeitung linasema hatua ya mwisho ya Wajerumani iliambulia patupu. Mradi wa mageuzi katika timu ya Ujerumani haukufaulu kuiwezesha kushinda kombe la Ulaya.


Mhariri wa Osnabrücker Zeitung anasema kama Ujerumani ingeshinda fainali dhidi ya Uhispania, ushindi huo ungemuimarisha kocha Joachim Löw, lakini sasa kocha huyo analazimika kuzowea kuishi na wazo kwamba mbinu zake zinazokabiliwa na shinikizo la kila siku zitatiliwa shaka.


Bila shaka hilo lingekuwa kosa kwani mfumo wa mchezo anaotumia Joachim Löw, hauwezi kubadilishwa na umeisadia timu ya Ujerumani kusonga mbele. Timu hiyo imecheza mchezo wa kasi ya kisasa ambao katika mashindano haya ya kombe la Ulaya wachezaji wameutumia kusonga mbele hadi kufika fainali. Mhariri wa Gazeti la Osnabrücker Zeitung anasisitiza kwamba vile Wajerumani walivyocheza ni muhimu zaidi kuliko kushinda kombe la Ulaya.


Kuwa bingwa wa Ulaya ni fursa kubwa kwa taifa kutangaza mambo yake, na timu karibu zote zilizoshiriki kwenye mashindano ya kuwania kombe la Ulaya mwaka huu ziliitumia nafasi hiyo. Hayo ni maoni ya gazeti la Berliner Zeitung.


Mhariri wa gazeti hilo anasema Poland, Chechnya na Russia katika kusakata kabumbu zimeonyesha bidii kubwa kama vile katika juhudi zao za kiuchumi. Zimo njiani kuelekea kucheza kiwango cha juu cha soka na kuondokana na mchezo unaochezwa kwa kawaida na timu za kanda ya mashariki mwa Ulaya.


Gazeti la Berliner Zeitung pia limesema nchi ambazo si wanachama wa Umoja wa Ulaya zimetoa mchango mkubwa katika wazo la kuwa na jamii ya kirafiki.


Wachezaji wa timu za Uturuki na Russia walionyesha umahiri wao katika soka na kushangiliwa na washabiki wengi nchini mwao, hivyo kuziongezea nafasi nchi zao kuukaribia Umoja wa Ulaya. Mhariri anamalizia kwa kusema ingawa nchi zilizoyaandaa mashindano ya mwaka huu ya kombe la Ulaya, Austria na Uswisi, ziliondolewa kwenye mashindano hayo mapema, kelele za kushangilia kila mechi hazikupungua viwanjani hadi fainali ya mashindano hayo hapo jana.


Likitukamilishia maoni kuhusu fainali ya jana, gazeti la Heilbronner Stimme linasema hatua ya washabiki hapa Ujerumani kutazama mechi kwa pamoja katika maeneo ya raia imedhihirisha kwamba soka ni mchezo unaoweza kutumiwa kama chombo muhimu cha kuleta maingiliano katika jamii. Hata hivyo halitakuwa jambo la busara kuongeza shinikizo dhidi ya mchezo huo na wachezaji. Matatizo ya kisiasa hayawezi kutatuliwa wakati wa muda wa mapumziko kama katika soka.


Kuhusu kuchaguliwa na kuapishwa kwa rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, gazeti la Die Welt, linazungumzia kuhusu `Laana ya Zimbabwe´


Mhariri anasema dikteta Mugabe hawezi kusonga mbele kwa haraka. Duru ya pili ya uchaguzi wa rais, kuhesabiwa kwa kura na hatimaye kuapishwa, yote katika siku muda wa siku mbili. Mugabe na utawala wake ulihitaji zaidi ya wiki sita katika uchaguzi wa mwezi Machi kutangaza matokeo.


Wakati huu hakuna malalamiko wala taswishi dhidi ya ushindi wa rais Mugabe, ambaye vikosi vyake viliwalazimisha raia kwenda kupigia kura. Mhariri wa gazeti la Die Welt anasema uchaguzi wa Zimbabwe ni kichekesho kwani mpinzani wa rais Mugabe alilazimika kujiondoa kutokana na matukio yaliyokuwa yakiendelea.


Gazeti la Süddeutsche Zeitung linaueleza uchaguzi wa Zimbabwe kuwa aibu. Wengi wanamueleza Mugabe kama mzee asiyejali, lakini hili halisaidii tena. Ulimwengu unatakiwa kumpinga Mugabe ambaye anaifanya nchi yake kuwa katika hali ya utumwa na kuruhusu mateso na machafuko. Mugabe ni muongo na hatari, na sharti jumuiya ya kimataifa imchukulie hatua kali zaidi kuliko zile ilizomchukulia mpaka sasa.


Gazeti la Dresdner Neuesten Nachrichten linasema mchezo unaoendelea nchini Zimbabwe unaweza kumalizwa tu na bara la Afrika pekee. Ikiwa hili litatokea, itategemea mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika huko Sharm el Sheikh nchini Misri unaozileta pamoja nchi 53 wanachama. Je umoja huo utatambua kuchaguliwa tena kwa rais Mugabe au kuendelea kumheshimu kama mpiganaji wa zamani dhidi ya ukoloni wa nchi za magharibi. Lakini hata kwa nchi za magharibi utakuwa wakati wa kujiepusha naye.


Gazeti la Handelsblatt linaamini nchi za magharibi licha ya ushawishi wake kuwa na mipaka, unapaswa pia kulaumiwa kwa hali ilivyo nchini Zimbabwe.


Gazeti linasema wanasiasa wa magharibi kwa mara chache wamekuwa wakiwakumbusha waafrika kuhusu jukumu lao. Kwa muda mrefu nchi za magharibi zimekuwa na matumaini na Mugabe, hatua ambayo mhariri anasema imechangia katika kujidanyaganya wenyewe.