1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo

Josephat Charo5 Desemba 2007

Wahariri wa magezeti ya Ujerumani leo wamejishughulisha na mpango wa nyuklia wa Iran.

https://p.dw.com/p/CXMt
Rais wa Iran Mahmoud AhmadinejadPicha: AP

Mhariri wa gazeti la Tageszeitung la mjini Berlin anasema maafisa wa ujasusi wa Marekani wametoa taarifa kwamba Iran ilisitisha mpango wake wa nyuklia miaka minne iliyopita.

Taarifa hii inazipa nafasi kubwa na pengine ya mwisho serikali za Marekani, Ufaransa na Ujerumani kurekebisha sera zao za hatari dhidi ya serikali ya Iran mjini Tehran. Kwa kufanya hivyo zitapunguza hatari ya kutokea vita. Lakini hakujatokea dalili za hilo kutokea.

Serikali za mjini Berlin, Paris, London na Washington zinaonekana kushikilia msimamo wao wa kuendeleza sera ya malubambano dhidi ya Iran na kuiongezea vikwazo.

Hisia zilizojitokeza kufuatia kutolewa kwa ripoti kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran zinadhihirisha kwamba serikali ya rais Bush inaweza kuuendeleza mzozo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran. Ukweli uliopo lakini ni kwamba lengo kubwa ni kuleta mabadiliko ya utawala mjini Tehran hata ikiwa ni kwa kutumia harakati ya kijeshi ikilazimu.

Gazeti la Offenburger Tegesblatt linauliza ni kitu gani kitakachofuata sasa baada ya ripoti ya Marekani. Je Iran inatengeneza silaha za kinyuklia au la? Habari za kutatanisha kutoka Marekani na Israel zinasababisha utata na matokeo yake ni kwamba karata za kisiasa zinachanganywa kuambatana na hofu ya wakristo dhidi ya itikadi kali ya kiislamu.

Wajinga katika swala zima hilo ni wananchi ambao wamekuwa wakilipa kodi kwa ajili ya mpango wa nyuklia ambao haupo. Makampuni ya silaha ya kimarekani ndiyo yalifaidi katika vita vya Irak na kwa kazi ya ujenzi wa taifa hilo uchumi umeanza kuimarika. Hilo ni shinikizo la kutumia fedha. Na hapa nchini Ujerumani waziri wa mambo ya ndani, Wolfgang Schäuble, akitumia itikadi kali ya kiislamu kama sababu anaizika haki ya raia. Uchunguzi utakaofanywa katika mtandao utakuwa chanzo tu.

Gazeti la Berliner Kurier linamhukumu rais wa Marekani, George W Bush. Mahariri anasema mpango wa Iran kutaka kutengeneza bomu la nyuklia umejitokeza kuwa wa uongo. Rais Bush anaonekana kuwa mjinga katika hilo. Kutokana na kitisho cha viongozi wa Iran kwa majuma kadha yaliyopita rais Bush amekuwa akitishia kuzuka vita vya tatu vya dunia, na pia kuanzisha mpango wa kujenga mifumo ya ulinzi dhidi ya makombora mashariki mwa Ulaya.

Sasa kitisho cha rais Bush kinasambaratika kwa urahisi namna hiyo, kama kilichomkuta katika vita vya Irak. Sababu zote alizozitoa rais Bush zilikuwa aidha za kubuni, kutilia chumvi au za uongo. Sasa rais Bush anatakiwa ajiulize ikiwa misingi ya sera zake za kigeni iko katika makosa au uongo.

Gazeti la Tagesspiegel la mjini Berlin linaonya kuwepo na uangalifu mkubwa. Mhariri anasema Iran zamani ilikuwa dola lenye nguvu na uwezo na mpaka leo ndivyo lilivyo. Rais Mahmud Ahmadinejad si mkaidi tu katika maneno bali hata katika vitendo. Anataka kuliangamiza taifa la Israel, anaendeleza shughuli za urutibishaji wa madini ya uranium ingawa nchi yake ina utajiri mkubwa wa mafuta. Akitaka anaweza kuubadili mpango wa nyuklia wa Iran ambao ni wa matumizi ya amani, kuwa wa kivita.

Kitisho cha serikali yake si kikubwa sana kama inavyofikiriwa. Hizi ni habari nzuri lakini ingekuwa bora zaidi kama hakungekuwa kabisa na kitisho chochote kutoka kwa Iran. Mhariri wa gazeti la Tagespiegel la mjini Berlin anamalizia kwa kusema furaha ya mtu anayeshangilia kushindwa kwa mtu mwingine huja kabla yeye mwenyewe kushindwa.