1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo

Josephat Charo29 Agosti 2007

Licha ya upinzani wa jeshi Abdullah Gül amechaguliwa kuwa rais mpya wa Uturuki. Kwa mara nyengine tena bwana Gül ametoa matamshi ya upatanisho na kutambua misingi ya nchi hiyo ambayo inatenganisha dini na maswala ya taifa. Hata wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wana matumaini kwamba Uturuki itakuwa mfano mzuri wa kuigwa katika ulimwengu wa kiislamu.

https://p.dw.com/p/CHRz

Gazeti la Tagesspiegel la mjini Berlin linaona Uturuki sasa iko katika njia sawa. Mhariri anasema kuchaguliwa kwa Abdullah Gül kuwa rais wa nchi hiyo kunaiongezea nguvu Uturuki na kumaliza mgogoro uliokuwepo miezi michache iliyopita. Ana serikali iliyopewa jukumu jipya na wapigaji kura, ajenda ya kufanya mabadiliko na wabunge wengi bungeni. Hiyo ina maana kwamba Umoja wa Ulaya unatakiwa usahau wazo kwamba hali ya ndani ya kisiasa nchini Uturuki itaizuia kuwa mwanachama wa umoja huo.

Uturuki itawasilisha ombi jipya katika makao makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels, Ubelgiji. Lakini kwa wakati huu halitakuwa jambo la kusisimua kwa Umoja wa Ulaya tu, bali pia kwa Uturuki. Watu wengi katika eneo la Mashariki ya Kati wanaitazama Uturuki kwa mshangao mkubwa kwa sababu nchi hiyo inaonekana kuwa jaribio la daraja kati ya uislamu na demokrasia.

Nalo gazeti la Handelsblatt la mjini Düsseldorf linasema kuchaguliwa kwa Abdullah Gül kuwa rais ni hatua muhimu kuelekea kuikomboa Uturuki kutokana na ushawishi mkubwa wa jeshi la nchi hiyo. Hiyo ni hatua kubwa muhimu kuelekea kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya.

Lakini uchaguzi wa sasa wa rais nchini Uturuki una maana kubwa zaidi kwa kuwa unaweka kanuni mpya kwamba Uturuki itakuwa mshirika imara na muhimu wa nchi za magharibi katika eneo linalokabiliwa na hali tete, na itakuwa mfano mzuri wa upatanisho kati ya uislamu na mambo ya kilimwengu. Hali hii inaweza kuigwa na kuenea katika nchi nyengine za kiislamu.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linakumbusha mambo yaliyokuwa yakiendelea nchini Uturuki. Mhariri anasema katika miaka iliyopita kumekuwepo na mabadiliko ya utamaduni nchini humo. Wasomi wasiolemea dini nchini Uturuki wamekuwa wakijihisi wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kisiasa tangu kuundwa chama cha AK mnamo mwaka wa 2001.

Mhariri anasema kwa miongo kadhaa waliwekwa kando na sehemu kati yao wakashawishiwa kujiunga na chama cha waislamu wenye itikadi kali, cha aliyekuwa waziri mkuu wa Uturuki kwa kipindi kifupi, Necmettin Erbakan, ambamo walitafuta kujiimarisha kisiasa. Miongoni mwa waliojiunga na chama hicho ni waziri mkuu wa sasa wa Uturuki, Reccep Tayip Erdogan na rais Abdullah Gül. Kwamba sasa viongozi hao wamefaulu kuondokana na itikadi kali ya kiislamu na wanajaribu kufuata njia isiyoelemea dini, ni jambo litakalofuatiliwa kwa karibu sana na nchi nyengine za kiislamu.

Gazeti la Ostsee la mjini Rostock linasema kuchaguliwa kwa Abdullah Gül kuwa rais wa Uturuki si sababu ya nchi za kigeni kutoiamini nchi hiyo kupita kiasi. Bwana Gül anajulikana kuanzia mjini Berlin, Brussels hadi Washington. Ni mtu anayeunga mkono uislamu, demokrasia na mwenye mwelekeo wa nchi za magharibi. Pengine anaweza kutumiwa kama daraja kati ya ulimwengu wa kiislamu na mataifa ya magharibi.

Lakini kuchaguliwa kwake kunaupa changamoto Umoja wa Ulaya na hasa kansela wa Ujerumani, Bi Angela Merkel, kushikilia msimamo wa kutotaka Uturuki isiwe mwanachama kamili wa umoja huo. Tayari rais wa Ufaransa, Nicholas Sarkozy, polepole ameanza kulegeza msimamo wake kwa uangalifu.

Mhariri wa gazeti la Aachener anadhani hofu ya mapinduzi bado ipo na anaonya kwamba majenerali wa jeshi la Uturuki, ambao wanaona jukumu lao kubwa ni kuilinda katiba ya nchi, huenda kwa mara nyengine tena wakakosa kuelewa. Kwa hiyo bwana Gül akiwa mtu anayeonyesha urafiki, anahitaji kukubalika na jeshi. Ingawa misingi yake ni ya kidini, Abdullah Gül ni mtu asiye na msimamo mkali wa kidini.

Nchi za magahribi zinamsifu kwa kutobadili lolote wakati alipokuwa waziri wa mashauri ya kigeni. Pia watoaji maoni katika miji mikuu ya Ulaya na makao makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels wanatakiwa kuwafikiria majenerali wa Uturuki.