1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo

Charo Josephat1 Julai 2009

Uamuzi wa mahakama ya katiba ya Ujerumani na kuondoka kwa wanajeshi wa Marekani kutoka Irak

https://p.dw.com/p/IenA
Majaji wa mahakama ya katiba ya KarlsruhePicha: AP

Kwa mtazamo wake gazeti la Süddeutsche Zeitung linasema uamuzi wa mahakama ya katiba ya Ujerumani ni wa "Ndiyo Tunaweza!"

Ndiyo tunaweza kuijenga Ulaya. Ndiyo tunaweza kuuendeleza muungano wa Ulaya. Ndiyo tunaweza kuiimarisha Ulaya. Lakini tunaweza tu kufanya hivyo kwa kuzingatia misingi ya demokrasia ambayo katika kitovu chake ndiko dhamira ya raia wa Ulaya iliko. Huo ndio ujumbe wa uamuzi mkubwa wa mahakama ya katiba ya Ujerumani mjini Karlsruhe.

Uamuzi huu wa kustaajabisha na wa busara umefaulu kutozuia mchakato wa maingiliano barani Ulaya na vilevile hatua ya Ujerumani kusita kuudhinisha mkataba wa Lisbon imewezesha uamuzi wa kidemokrasia kuchukuliwa, linasifu gazeti la Süddeutsche Zeitung.

Gazeti la Berliner Zeitung linauona uamuzi wa mahakama ya katiba ya Ujerumani kuwa mzuri na unaofaa. Haufuji mkataba wa Lisbon bali unatoa mwelekeo wa misingi ya kuundwa Umoja wa Ulaya na mpango wa kujenga Ulaya yenye demokrasia.

Mhariri wa gazeti la Berliner Zeitung anasema ujumbe muhimu unaojitokeza kufuatia uamuzi wa mahakama ya Karlsruhe ni kwamba bara la Ulaya ni muhimu mno kuliachia taasisi za Ulaya pekee. Kwa matatizo ya ruzuku ya kilimo na matatizo mengine, makao makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels yana kazi muhimu ya kufanya, lakini bara la Ulaya kama mfano wa siku za usoni kwa mataifa ya Ulaya na raia wake, liko katika ajenda ya sera za kitaifa.

Kwa uamuzi wake mahakama ya katiba ya Ujerumani inaifanya sera ya kuleta maingiliano barani Ulaya kuwa mada yenye kipaumbele katika sera za ndani, linakamalisha maoni yake gazeti la Berliner Zeitung.

Majeshi ya Marekani yaanza kuondoka Irak

Likitugeuzia mada gazeti la Esslinger Zeitung linatathmini kuondoka kwa wanajeshi wa Marekani kutoka miji ya Irak. Mharriri wa gazeti hilo anasema kufikia mwishoni mwa mwaka 2011 majukumu yote ya kulinda usalama nchini Irak yanatakiwa kukabidhiwa kwa polisi na wanajeshi wa Irak.

Irak / US-Truppenabzug
Vikosi vya Irak vikuchukua madaraka kuilinda miji ya IrakPicha: AP

Lakini mhariri pia anasema ukweli ni kwamba mashambulio ya umwagaji damu ya hivi karibuni yaliyosababisha vifo vya watu wengi yanadhihirisha wazi dhahiri shahiri kwamba vyombo vya usalama nchini Irak bado havijakomaa vya kutosha kuweza kudhibiti usalama. Bado ni dhaifu kuweza kudumisha amani nchini kote na kuzuia machafuko ya kikabila kati ya waislamu wa madhahebu ya Sunni, Washia na Wakurdi, linakumbusha gazeti la Esslinger Zeitung.

Wimbi la mashambulio ya kigaidi ya hivi karibuni yaliyofanywa na kundi la al Qaida yanaonyesha kwamba Irak mpya ina maadui wengi ndani na nje ya mipaka yake, linasema gazeti la Neue Osnabrücker Zeitung.

Mhariri wa gazeti hilo anasema wanajeshi wa Marekani na Uingereza walitumia uwezo wao wote kupambana na kuyashinikiza makundi yote yenye msimamo mkali wa kidini likiwemo pia kundi la al Qaeda, kiasi cha kuweza kuboresha hali jumla ya usalama nchini Irak. Ni maoni ya kawaida barani Ulaya kuwa sio rahisi kuvishinda vita dhidi ya ugaidi na wapiganaji wa chini kwa chini.

Ukuaji wa kiuchumi, shughuli za kuendeleza mifumo ya elimu na afya na aina mbalimbali ya vyombo vya habari vinaeleza hadithi tofauti kabisa. Lakini pamoja na hayo yote hali nchini Irak haitakiwi kusifiwa kuwa nzuri, ingawa nafasi za kuiboresha Irak zimezidi vitisho na hatari zilizopo. Hivyo ndivyo gazeti la Neue Osnabrücker Zeitung linavyokamalisha maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.

Mkusanyaji :Josephat Charo/dt zeitungen

Mhariri:M.Abdul-rahman