1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo

Josephat Nyiro Charo2 Juni 2010

Mada zilizoangaziwa ni hatua ya Israel kuishambulia meli ya misaada iliyokuwa ikielekea Gaza na juhudi za kumtafuta rais mpya wa Ujerumani

https://p.dw.com/p/NfXe
Wanajeshi wa Israel wakiwa kwenye meli ya UturukiPicha: AP

Hatua ya Israel kuishambulia meli ya misaada iliyokuwa njiani ikielekea Ukanda wa Gaza, ni mada iliyohanikiza kwenye magazeti ya Ujerumani hii leo.

Gazeti la Braunschweiger Zeitung linasema Israel imejidhihirisha kama adui asiyejali anayetaka kuchokozi utawala wa chama cha Hamas katika Ukanda wa Gaza bila kuzingatia kumaliza hatua yake ya kuuzingira ukanda huo. Kwa kuishambulia meli ya misaada,Israel imetumia funzo ililopata wakati wa vita vyake na wanamgambo wa Hezbollah nchini Lebanon mnamo mwaka 2006 - kutoonyesha udhaifu. Inahuzunisha kwamba watu tisa waliuwawa katika operesheni ya jeshi la Israel.

Gazeti la Reutlinger General-Anzeiger linasema Israel imetumia nguvu kupita kiasi na kuvuka mipaka kwa kuishambulia meli hiyo. Mhariri anasema ingefaa kama uchunguzi wa meli hizo ungefanywa na shirika la msalaba mwekundu, ili kuepusha mapambano baina ya wanaharakati wa amani na wanajeshi wa Israel.

Kuhusu juhudi za kumtafuta rais mpya wa Ujerumani gazeti la Der neue Tag kutoka Weiden linasema serikali ya mseto ya muungano wa vyama vya CDU-CSU pamoja na chama cha FDP, inakabiliwa na changamoto kubwa ya kurejesha uaminifu uliopotea. Mhariri wa gazeti hilo anasema katika juhudi hizo msaada mpana kutoka kwa wananchi wa Ujerumani utakuwa na umuhimu mkubwa, ili kuweza kufanikisha lengo hilo.

Gazeti limeendelea kuandika kuwa Wajerumani hawataki tu mtu mwerevu na mwenye busara achukue wadhifa huo muhimu humu nchini, bali pia wanataka awe mtu shupavu anayeweza kufuatilia na kutizama, si kwa karibu sana wala kwa mbali, jinsi karata za kisiasa zinavyochanganywa katika ulingo wa kisiasa hapa Ujerumani.

Nalo gazeti la Badische Neuste Nachrichten la mjini Karlsruhe linasema kitendo cha kukatisha tamaa cha rais Köhler kuacha wadhifa wake hivi hivi tu, hatua ambayo imewakasirisha watu wengi waliokuwa na matumaini makubwa na kiongozi huyo, kingeweza kuisambaratisha kabisa serikali ya mseto mjini Berlin.

Lakini kwa kuwa jambo hilo halikutokea, na hakujatokea mpasuko mkubwa ndani ya serikali, hiyo ndiyo chembe pekee ya matumaini ambayo kansela wa Ujerumani Angela Merkel na naibu wake Guido Westerwelle, pamoja na rais mpya mtarajiwa, wanayoweza kuitegemea, ili kwa ufanisi kuweza kuendesha shughuli za serikali.

Bundeskanzlerin Angela Merkel Rücktritt Horst Köhler
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: AP

Gazeti la Süddeutsche Zeitung linasema kansela Angela Merkel analazimika kupendekeza jina la mtu mwenye ushawishi na anayeweza kuungwa mkono na idadi kubwa ya watu. Mhariri anauliza, "Ni nani atakayechukua nafasi iliyoachwa na rais Köhler?" Kuna majina mengi yanayofikiriwa, ni kama mchezo wa karata. Kwa kuwa nchi iko katika mtihani mkubwa, watu wengi wanatazamia muujiza utendeke.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung limeonya juu ya kutafutwa ufumbuzi wa haraka na utakaokubalika na wengi ili kuagua kitendawili kilichopo katika kasri la rais la Bellevue mjini Berlin.

Likitugeuzia mada gazeti la Volksstimme kutoka Magdeburg limeandika kuhusu mkasa mkubwa wa kuvuja kwa mafuta katika ghuba ya Mexico.

Mhariri wa gazeti hilo anasema kumeshawahi kutokea ajali wakati wa uchimbaji na usafishaji wa mafuta na kila mara maeneo ya pwani huchafuliwa na wanyama kufa. Lakini mkasa unaondelea katika ghuba ya Mexico hauna mithili. Athari zake zinajitokeza kila siku. Sio tu kwa mimea, wanyama, sekta ya uvuvi na utalii katika majimbo ya kusini mwa Marekani, bali pia kutakuwa na athari za muda mrefu kwa misitu ya mikoko, jambo ambalo litaathiri maeneo ya hifadhi kwenye pwani za Marekani. Mhariri anahoji kwamba hata rais wa Marekani, Barack Obama, mwenyewe hataweza kuhimili janga hili bila kupata madoa doa.

Mwadishi: Josephat Charo/Inlandspresse/DPA

Mhariri: Abdul-Rahman