1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani.

Abdu Said Mtullya1 Juni 2011

Wahariri watoa maoni juu ya FIFA, Libya na Mkasa wa ndege baina ya Iran na Ujerumani

https://p.dw.com/p/11SMw
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: picture alliance/dpa

Ndege ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ilinyimwa ruhusa ya kuingia katika anga ya Iran wakati ikiwa angani kuelekea India. Juu ya kadhia hiyo mhariri wa gazeti la Volksstimme anasema Iran haikuonyesha heshima kwa Kansela wa Ujerumani. Mhariri anaeleza kuwa Kansela huyo hakuwa anaenda kubembea katika likizo bali,alikuwa anasubiriwa kuanza ziara nchini India.

Mhariri huyo anasema hatua ya Iran inaonyesha jinsi utawala wa nchi hiyo ulivyokuwa na wasiwasi,kwani utawala huo upo tayari kufanya lolote lile kwa ajili ya mpango wake wa silaha.!

Gazeti la Die Zeit linatoa maoni juu ya hatua zinazochukuliwa na nchi za magharibi nchini Libya. Gazeti hilo linaeleza kuwa nchi hizo zinakabiliwa na mtanziko kuhusu Libya. Jee zijiingize moja kwa moja kijeshi au hapana, wakati Gaddafi anaendelea kuwaua watu wake. Kwani katika upande mmoja pana hoja kwamba kutochukua hatua ni aibu,na kujiingiza kijeshi kunaweza kuwa na hatari ya kuzama katika vita bila ya kujua matokeo yake.

Shirikisho la Kandanda duniani FIFA, leo linafanya mkutano wake mkuu ambapo wajumbe wa bodi ya uongozi watamchagua Rais wa Shiriisho hilo kwa kipindi kingine cha miaka minne. Lakini uchaguzi huo unafanyika wakati imetolewa miito juu ya kuuahirisha kutokana na madai ya rushwa.

Mhariri wa gazeti la Berliner anazungumzia juu ya athari za tuhuma hizo za rushwa na anasema kuwa kwa mara ya kwanza pametolewa madai ya rushwa kutokea ndani ya kamati ya utendaji ya FIFA. Anasena kama ilivyokuwa kwa kamati ya Kimataifa ya Olimpiki, IOC,shinikizo sasa linaimarika, kutokea pande sahihi na muhimu ; kutoka kwa wafadhili wanaotoa mabilioni ya fedha. Kimbunga kimeanza, kinachoweza kumkumba siyo Rais wa FIFA peke yake bwana Blatter bali pia Qatar, itakayokuwa mwenyeji wa mashindano ya kombe la dunia.

Na mhariri wa gazeti la Hannoversche ansema ikiwa madai ya rushwa juu ya Qatar yatathibitishwa ,kweli patatokea Tsunami ya kandanda kama aliyvosema kiongozi mmoja wa FIFA hapo awali.

Mwandishi/Mtullya Abdu/Deustche Zeitungen /

Mhariri/- Abdul-Rahman