1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani.

5 Juni 2007

Katika maoni yao wahariri wa magazeti leo wanazungumzia juu ya mpango wa Marekani wa kuweka makombora ya ulinzi katika Ulaya ya mashariki .

https://p.dw.com/p/CHSn

Wahariri hao pia wanatoa maoni yao juu ya hatua zinazochukuliwa na polisi wa Ujerumani katika kuwakabili wapinzani wa sera za dunia utandawazi.

Gazeti la OLDENBURGISCHE VOLKSZEITUNG linasema katika maoni yake kuwa ni sawa kujadili juu mkakati unaotumiwa na polisi wa Ujerumani katika kuwakabili wapinzani hao wa sera za dunia utandawazi, wakati viongozi wa nchi nane tajiri wanajitayarisha kuanza mkutano wao katika kitongoji cha Heiligendamm kwenye mji maarufu wa bandari ya Rostock mashariki mwa Ujerumani

.Lakini anasisitiza kwa kusema kwamba la muhimu zaidi, ni kulishughulikia jambo hilo kwa matendo.Lazima hatua zichukuliwe.

Mhariri anaeleza kuwa wakati unayoyoma na yaelekea vijana hao wanashangilia ushindi, na yumkini wanaandaa ghasia zaidi.Anatamka kuwa ikiwa polisi hao wataendelea na makakati wanaotumia sasa basi watakuwa wanazembea.

Katika maoni yake gazeti la WESTFÄLISCHE RUNDSCHAU kutoka mji wa Dortmund kaskazini mwa Ujerumani linatoa onyo kwa kusema kuwa njia zinazotumiwa na polisi zinaelekea katika mkondo potofu : mahariri huyo anasema njia iliyobakia sasa ni kujaribu kupunguza kasi ya ghasia hizo. Hakuna mbadala lakini mhariri anasisitiza kuwa njia hiyo haimaanishi kuwaachia vijana hao waendelee na ghasia.

Mhariri huyo anashauri kuwa njia ya kufaa sasa ni kuwatenga wahuni na watupa mawe katika wakati mujarabu. Lakini mhariri anasikitika kuwa njia hiyo haijatumika. Matokeo yake ni kwamba polisi wamelazimika kutunisha misuli kiasi cha kuvuka mipaka.


Na gazeti la BERLINER ZEITUNG linasema katika maoni yake kuwa ghasia zinazofanywa katika mji wa Heiligendamm zinathibitisha udhaifu wa wapinzani wa sera za dunia utandawazi.Mhariri huyo anaongeza kwa kueleza kuwa hao wanaofanya ghasia hizo siyo kundi la kisiasa. Hivyo basi yapasa kujiuliza vipi imewezekana kwa polisi kushtukizwa na ghasia hizo?

Wahariri leo pia wanazungumzia juu ya mvutano baina ya Urusi na Marekani kuhusiana na mpango wa kuwekwa makombora ya kujihami katika nchi za Ulaya ya mashariki.

Mvutano huo umeshtadi kutokana na maneno makali yaliyotolewa na rais Vladimir Putin wa Urusi, kwani anahisi kuwa makombora hayo yatatishia usalama wa nchi yake na pia yatatibua urari wa nguvu za kijeshi. Putin ametishia kuweka makombora na kuyaelekeza barani Ulaya ikiwa Marekani itaweka silaha hizo katika Ulaya ya mashariki.

Juu ya hayo gazeti la HAMBURGER ABENDBLATT linatathmini kauli hiyo kuwa ni hatua ya rais Putin kujaribu kusimama katika ngazi ya usawa na Marekani.

Na mhariri wa gazeti la FINANCIAL TIMES la Ujerumani anasisitiza kwa kusema kwamba mgogoro huo siyo hasa juu ya makombora bali ni juu ya fahari ya Urusi iliyoshindwa katika vita baridi mnamo miaka ya nyuma. Gazeti linasema , anachotaka rais Putin ni kusikilizwa katika ulingo wa kimataifa.

AM.