1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani

Josephat Charo26 Aprili 2007

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani ambao leo hii wamejishughulisha na mgogoro katika kampuni ya Siemes kufikia kilele kufuatia kujiuzulu kwa mkurugenzi wake, Klaus Kleinfeld. Wahariri pia wamejadili mivutano mipya ndani ya serikali ya mseto ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/CHT7

Kuhusu kujiuzulu kwa mkurugenzi wa kampuni ya Siemens, bwana Klaus Kleinfeld, gazeti la Südwest Presse la mjini Ulm limesema kampuni ya Siemens ilikuwa zamani kampuni iliyojumulisha ufundi wa uhandisi wa Ujerumani na kazi ya thamani. Lakini kwa wakati huu kampuni hiyo ni kitovu cha ufisadi, mivutano ya kibinafsi na mitafaruku. Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Heinrich von Pierer, alilazimika kujiuzulu na pia kiongozi aliyechukua nafasi yake Klaus Kleinfeld amelazimika kung´atuka.

Mhariri wa gazeti la Südwest Presse ameendelea kusema huo ulikuwa mchezo usio na maana. Si kwa sababu cheo hicho cha juu ndicho kinachobeba dhamana kwa kuitetemesha misingi ya kampuni ya Siemens. Mambo mengi yanayofanana na hayo yaliyotokea yanamfanya mtu kutilia shaka utendaji wa baadhi ya mameneja wanaosimamia kampuni ya Siemens. Hatua ya bwana Kleinfeld kutangaza hadharani kujiuzulu kwake kumeishusha hadhi yake.

Gazeti la Nordbayerische Kurier la mjini Bayreuth linaongeza kusema kwamba sio lazima kumhurumia bwana Klaus Kleinfeld kupita kiasi wakati yeye mwenyewe ndiye aliyemua kuacha wadhifa wake. Sasa bwana Kleinfeld ameingia matatani ingawa hakuna makosa dhahiri aliyoyafanya. Aliyoyafanya bwana Pierer yalimshinikiza Kleinfeld hata kabla kuweza kuanza upya kufanya kazi yake.

Kwa hiyo mtu anaweza kusema kwa uhakika kabisa kwamba bwana Kleinfeld hatakaa muda mrefu bila kupata kazi nyengine nzuri na yenye mshahara mnono. Lakini hata hivyo kujiuzulu kwa Kleinfeld kwa njia ya uchungu kama hiyo, bila shaka imemtia baridi na kumdhoofisha mkurugenzi huyo, akamalizia mhariri wa gazeti la Nordbayerische Kurier.

Gazeti la Tageszeitung la mjini Berlin limechambua kwa kusema meneja Kleinfeld amelazimika kujiuzulu kwa sababu sifa, hadhi na taswira ya kampuni ya Siemens imeharibika. Haya yamelazimu mageuzi katika makampuni makubwa duniani. Kwa kuwa imeendelea kuwa rahisi zaidi kupata bidhaa nyengine kama zile zinanazotengenezwa na kampuni ya Siemens, ni muhimu kuchukua hatua za kuzilinda bidhaa zake. Kwa njia hiyo kampuni ya Siemens itakiuka maadili na kuumiza hisia za wafanyakazi wake huku maadili yake yakizingatia ufanisi wa kiuchumi.

Tukigeukia mpasuko mpya ndani ya serikali ya mseto mjini Berlin ambao umesababishwa na matamashi ya kiongozi wa chama cha SPD, bwana Kurt Beck, na kiongozi wa wabunge wa chama hicho bungeni, Peter Struck, kuhusu muungano, gazeti la Financial Times Deutschland limesema malumbano ya sasa yana mizizi yake katika ulingo wa siasa. Bwana Peter Struck na Kurt Beck, walikutana faraghani kuzungumzia mshirika wao serikalini. Mhariri anasema mazungumzo hayo yalionekana kuwa ya malumbano lakini kufikia sasa vyama viwili serikali bado viko mbali kufikia mgogoro mkubwa unaoweza kuihatarisha serikali.

Mhariri wa gazeti la Frankfurter Allgemeine amesema swala hivi sasa halihusu nani aliye na haki katika tofauti mpya ndani ya serikali. Mwaka mmoja uliopita chama cha SPD na chama cha CDU/CSU havikutofautiana sana kuhusu mageuzi ya sheria za ubaguzi na magaezi ya mfumo wa afya. Lakini sasa bwana Beck anazungumzia tofauti ya maneno kwa sababu mbunge mmoja tu wa chama cha CDU ametilia shaka kodi ya mirathi.