1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini.

Abdu Said Mtullya29 Juni 2009

Merkel atoa ahadi ya kupunguza kodi?

https://p.dw.com/p/IdLJ
Mwenyekiti wa chama cha CDU Angela Merkel atoa ahadi ya kupunguza kodi.Picha: Bundesregierung, Guido Bergmann

Vyama vya  kihafidhina  vilivyomo  katika serikali  ya Ujerumani vimetangaza programu ya uchaguzi  mkuu utakaofanyika  hapa  nchini  Ujerumani mnamo  mwezi   septemba .  Wahariri wa magazeti ya  hapa  nchini wanazungumzia  suala   hilo  katika maoni  yao  leo.

Wahariri hao pia wanazungumzia  juu ya utayarifu  wa Marekani katika kufanikisha  juhudi  za kupambana  na mabadiliko  ya  hali ya hewa.

Vyama  vya kihafidhina  vya  CDU na CSU vilivyomo katika serikali  ya  mseto hapa nchini vimeahidi kupunguza kodi ya mapato, kama sehemu ya kampeni ya  uchaguzi mkuu.

Juu ya kampeni hiyo gazeti  la Emder linasema vyama  vya CDU na  CSU vimekubaliana juu ya kupunguza kodi lakini  gazeti  linasema  vyama  hivyo havikutaja tarehe ya  kuanza  kutekeleza ahadi hiyo.

Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa ikiwa, vyama hivyo havitaji tarehe maalumu juu  ya  kutekeleza ahadi yao, itakuwa  vigumu  kwa wapiga kura kusema  ahadi  hiyo ni hadaa za kampeni   za uchagazi.  Baada ya uchaguzi  vyama hivyo vitakuwa na muda  wa kufikiria  juu  ya ahadi yao.

Mhariri  wa gazeti la Emder anasema iwapo wapiga kura watakubali hayo itaonekana  baada  ya uchaguzi.

Hatahivyo mhariri  wa  gazeti  la Sächsische anasema, ikiwa mtu alifuatilia  kwa makini hotuba  ya mwenyekiti  wa  chama  cha CDU Angela Merkel  ameweza  kutambua kwamba   mwenyekiti huyo  hakusema chochote.

Gazeti hilo linaeleza kuwa  hakuna mtu anaejua  kwa uhakika  ni lini Ujerumani itaondokana na  mgogoro  wa uchumi.Kwa  hiyo ahadi juu ya kupunguza kodi  haikufafanuliwa, vipi na lini itatekelezwa.


 Gazeti  la Münchner Merkur linasema katika  mazingira  magumu  ya  mgogoro wa  uchumi  ni vigumu  kuona ni lini  na vipi ahadi  ya  kupunguza kodi inaweza kutimizwa. Mhariri wa gazeti hilo anawaonya  wanasiasa  kuwa wasishangae  ikiwa wananchi watawakasirikia kwa kujaribu  kufikiri kwamba wao  ni wapumbavu.!

 Katika maoni  yake  mhariri  wa  gazeti la Neue Osnabrücker anazungumzia juu ya  ishara ya matumani  kutoka Marekani kabla  ya  kufanyika mkutano kuhusu mabadiliko  ya  hali ya  hewa .

Mhariri  huyo anasema  pana  ishara  ya matumaini  kutoka Marekani juu  ya mkutano  utakaojadili  mabadiliko  ya hali ya  hewa mjini Copenhagen.

Gazeti la Neue Osnabrücker linaeleza kuwa rais Obama  anatambua  kwamba nishati  endelevu  ziteleta  nafasi za kazi. Marekani imo mbioni kuwa wa kwanza katika tekinolojia ya nishati  ya upepo.Gazeti linasema hayo ni matumaini makubwa kutoka Marekani katika  kufanikisha  mkutano  juu  ya mabadiliko  ya hali hewa utakaofanyika mjini  Copenhagen mwishoni  mwa mwaka huu.

Mwandishi:Abdul Mtullya/Dt Agenturen

Mhariri:Abdul-Rahman