1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini.

Abdu Said Mtullya6 Januari 2010

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanasema Obama hajasema vipi atang'oa mizizi ya ugaidi.

https://p.dw.com/p/LMTC
Rais Barack Obama akifafanua hoja juu ya suala la ugaidi.Picha: AP

Wahariri  wa magazeti ya  Ujerumani  leo wanatoa maoni  yao juu ya  rais  Obama, ugaidi,  na juu  ya  hali ya ajira nchini Ujerumani.

Gazeti la Osnabrücker linakumbusha kwamba   katika mwaka 2008 takriban kila suala  lilifungamanishwa  na  kuondoka madarakani   kwa  rais George  Bush ambae hakuwa maaruf  duniani. Kuondoka kwake pia kulifungamanishwa na uwezekano wa kumalizika kwa  ugaidi.


Gazeti hilo  linasema matumaini hayo yalitiwa rutuba na  uamuzi  wa  kumpa  rais  Barack Obama  tuzo  ya amani  ya  Nobel.Lakini mhariri  wa  gazeti  la Osnabrücker anatamka kuwa hali halisi ni nyingine.

Anaeleza kuwa magaidi  wa Al-Qaeda bado wanaendelea kuangamiza watu.Idadi kubwa ya  vifo nchini  Afghanistan  vya  askari  wa Marekani  na  wa nchi nyingine  za Nato, pamoja  na  jaribio la shambulio la kigaidi nchini Marekani; hayo  yamewafanya  watu watambue hali halisi ambayo  siyo ya kufurahisha.

Gazeti Osnabrücker linatilia maanani kwamba,  nchini Marekani pia, ghafla umezuka mjadala  mkali juu ya  njia za kupambana na ugaidi na  juu   ya suala la Afghanistan.

Gazeti hilo linasema pamoja  na kuongeza idadi   ya wanajeshi  mara tatu nchini Afghanistan, rais Obama  sasa anazungumza kama George Bush.   Sasa anazungumzia juu ya vita dhidi  ya  mtandao  wa kigaidi. Lakini mhariri  wa gazeti la Osnabrücker anatilia  maanani kwamba  rais huyo   bado hajatoa jawabu thabiti  ,kujibu swali,vipi ataweza kupambana na mizizi ya ugaidi.

Gazeti la  Rheinische Post leo linazungumzia juu   ya uamuzi  wa Kansela  Angela Merkel wa  Ujerumani  wa kuunda  kamati ya baraza la mawaziri  itakayoshughulikia suala la Afghanistan.

Gazeti hilo linasema hatua hiyo inathibitisha kwamba kiongozi huyo wa Ujerumani ameliweka  suala  la Afghanistan moyoni. Gazeti hilo pia   linatilia maanani  kwamba Kansela  Merkel  ameunda  kamati hiyo ya watu  wenye utaalamu, watakaotayarisha mwongozo  wa  pamoja, kabla  ya kufanyika mjini London, kwa mkutano wa kimataifa juu ya Afghanistan.

Gazeti la General -Anzeiger limenukuu usemi wa mtaalamu  Robert Baden  Powel aliesema  "jitayarisheni".

Gazeti hilo limenukuu usemi huo kuhusiana na  hali ya  ajira nchini Ujerumani. Gazeti limeeleza  kuwa watu  nchini Ujerumani walijitayarisha    kuona idadi  ya wasiokuwa na ajira ikipanda   hadi kufikia milioni nne na laki moja. Lakini gazeti  linasema hali hiyo haijatokea.

Mhariri wa gazeti la Landeszeitung  anaunga mkono kwa kusema kwamba hakuna alietarajia kuona ukakamavu  huo katika soko la ajira katika mazingira ya mgogoro mkubwa  wa uchumi.

Hatahivyo, mhariri  wa  gazeti hilo anaelezea msingi  wa ukakamavu huo- Idara kuu ya ajira ilitenga kiasi cha Euro  bilioni 5 kwa ajili ya kulipa mishahara ya watu wanaofanya kazi kwa saa  pungufu. ....

Mwandishi/Mttullya  Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Othman, Miraji