1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani.

Abdu Said Mtullya24 Machi 2010

Pamoja na kuzungumzia juu ya uhusiano wa Marekani na Israel wahariri wa magazeti ya Ujerumani pia wanakumbusha kwamba kifua kikuu bado ni maradhi ya hatari.

https://p.dw.com/p/MbBd
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.Picha: AP

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanatoa maoni juu ya uhusiano baina ya Israel na Marekani na juu ya siku ya maradhi ya kifua kikuu duniani.

Mhariri wa gazeti la Hannoversche Allgemeine anatilia maanani kwamba katika ziara yake nchini Marekani waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesisitiza msimamo wa serikali yake juu ya kujenga makaazi ya walowezi wa kiyahudi mashariki mwa Jerusalem.

Gazeti la Hannoversche Allgemeine linasema bila shaka rais Obama na waziri wake wa mambo ya nje walizungumza na mgeni wao, Waziri Mkuu wa Israel,juu ya suala hilo. Lakini gazeti linasema ,Obama na waziri wake wameyafanya hayo kwa faragha.

Mhariri wa gazeti hilo anafafanua kuwa hatua ya Obama haina manufaa makubwa kuhusiana na hali ya Mashariki ya Kati bali mazungumzo ya Obama na Netanyahu yalihusu zaidi siasa za ndani ya Marekani.

Mhariri wa Hannoversche Allgemeine anatilia maanani kwamba mnamo siku zilizopita wanasiasa wa Marekani walikuwa wanatoa kauli kali dhidi ya Israel, yaani nchi iliyofungamana nayo kwa uthabiti. Kauli hizo hazikupokelewa vizuri na wamerekani. Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anatumia mtazamo wa wamerakani hao kwa manufaa yake.

Na mhariri wa gazeti la Münchner Merkur anasema mtu anaweza kumtuhumu Waziri Mkuu wa Israel Netanyahu mambo mengi. kwa mfano, kutokana na msimamo wa Israel suluhisho la nchi mbili katika Mashariki ya Kati linashindikana.Pia suluhisho la nchi moja haliwezekani kwa sababu Israel haiwezi kukubali kuwa chini ya wapalestina wengi. Na hivyo basi wapalestina watawekwa mbali na chini ya shinikizo. Lakini mhariri anasema ugaidi utakaotokana na hali hiyo, utakaotumiwa kama mwao ,hautaishia katika Ukanda wa Gaza tu.

Shirika la afya duniani WHO, leo linaadhimisha siku ya maradhi ya kifua kikuu duniani.Na gazeti la Volksstimme linatumia wasaa huo kukumbusha kwamba shirika hilo liliitangaza siku ya leo miaka kadhaa iliyopita. Gazeti linasema maradhi ya kifua kikuu hayamo katika mwamko wa vijana tokea muda mrefu. Lakini gazeti hilo linakumbusha kwamba ugonjwa huo unaendelea kuwamaliza watu katika sehemu mbalimbali za dunia.

Mhariri wa gazeti la Volksstimme anaeleza kuwa mnamo miaka ya 70 watu walifikiri, binadamu alifanikiwa kuutokomeza ugonjwa huo. Lakini gazeti linaeleza, leo wataalamu wameingiwa wasiwasi kwa sababu maradhi hayo yamejenga usugu dhidi ya dawa zilizopo.Na kutokana na idadi kubwa ya watu walioambukizwa maradhi hayo duniani,pana hatari ya ugonjwa huo kulipuka katika kiwango kikubwa kuliko kile cha mafua ya nguruwe!

Mwandishi/Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri/Abdul-Rahman