1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti

23 Julai 2007

Wahariri wa magazeti yote leo wanazungumzia juu ya mkasa wa mjerumani alietekwa nyara na kuuawa nchini Afghanistan .

https://p.dw.com/p/CHSL

Juu ya mkasa huo wa kusikitisha gazeti la HESSICH/NIEDERSÄCHSICHEN ALLGEMEINE linasema yote ni mamoja iwapo mjerumani huyo alikufa kutokana na ugonjwa wa moyo uliosababishwa na uchovu ama kutokana na kupigwa risasi.

Mhariri anasema ni jambo la kusikitisha kuwa mjerumani huyo aliekuwa mhandisi amepoteza uhai wake kwa sababu tu alitaka kuwasaidia watu wa Afghanistan.

Mhariri huyo pia anasema kuwa mataliban wametumia mkasa huo kwa shabaha za propaganda , kwa mafanikio , kiasi kwamba idadi ya wajerumani wanaopinga majeshi ya nchi yao kuwapo nchini Afghanistan inaongezeka.


Gazeti la NORDKURIER kutoka jimbo la Neubrandeburg linasema, kuwa hali inazidi kuwa mbaya nchini Afghanistan , lakini nchini hiyo inahitaji misaada ya nchi za magharibi. Gazeti linasema, baadhi ya watu wanashauri kuwaachia watu wa Afghanistan wenyewe wajiendeshee nchi yao.

Lakini Mhariri huyo anatilia maanani kuwa hali ya usalama inazidi kuwa mbaya kila panapokucha na kwamba nchi hiyo haiwezi kusimama bila ya misaada kutoka nchi za magharibi.

Hivyo basi gazeti linaeleza kuwa, ikiwa nchi za magharibi zitaondoa majeshi kutoka Afghanistan na kuwaachia watu wa nchi hiyo waendeshe maisha yao peke yao, matokeo yake yatakuwa kurejea tena kwa mataliban.

Katika maoni yake gazeti la BERLINER ZEITUNG linauliza juu ya lengo la jukumu la Ujerumani nchini Afghanistan.

Gazeti linasema,kuwa yanayosikika kutoka kwa serikali za magharibi ni yaleyale, kwamba serikali hizo hazikubali kushinikizwa na kuwa hazitaondoa majeshi yao kutoka Afghanistan.

Lakini mhariri anauliza jee nini hasa ni lengo la jukumu la Afghanistan? Na vipi litafikiwa.? Na vipi itawezekana kuepuka maafa nchini humo.?

Gazeti hilo la BERLINER ZEITUNG linazishauri nchi za magharibi ziachane na ujuvi .Lazima nchi hizo zitathmini vizuri sera zao juu ya kuleta demokrasia kwa kutumia nguvu za kijeshi.Ziangalie wapi sera hizo zimeshindikana na zijifunze kutokana na makosa, siyo tu nchini Afghanistan bali pia kwenye Ukanda wa Gaza na kuhusu Iran.

Lakini mhariri wa gazeti la HANDELSBLATT anasema pamoja na uovu wa kutekwa nyara raia wa nchi za magharibi wanaosaidia katika ujenzi mpya wa Afghanistan , haitakuwa sawa kufunga virago na kuondoka.

Japo gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU linazishauri nchi za magharibi juu ya kuwa na mkakati wa kuijengea serikali ya Afghanistan uwezo wa kudhibiti nchi ili nchi za magharibi ziondoke Afghanistan haraka.

AM.